Monday, January 25, 2016

AFYA: JUA ZAIDI KUHUSU SARATANI (CANCER)

Richard Edward | 12:05:00 PM |
Cancer

Ni wakati mwingine wa kujumuika nanyi katika afya, na tutanza kuzungumzia magonjwa ya kansa.Ypo imekuwa tishio n kukatisha tamaa watu wengi katika jamii zetu.

Katika vipindi vyetu kadhaa vinavyofuata tutakuletea  magonjwa ya saratani tukiwa na matumaini kuwa tutawafaidisha watu wote ili waweze kuimarisha afya zao na ya jamii kwa ujumla. 


Kabla ya kuanza kuchambua aina tofauti za saratani, kwanza kabisa tujue nini maana ya kansa.

Kansa au saratani
ni kundi la magonjwa yanayosababishwa na mgawanyiko usio sawa na usiodhibitika wa seli na kuunda uvimbe unaovamia na kuzidhuru tishu. Kuna aina zaidi ya 100 za kansa kwa kuzingatia ni kiungo gani cha mwili kimeathirika.

Hata hivyo aina zote hizo za kensa zina sifa 3 zinazofanana ambazo ni, ukuaji usiodhibitika wa seli, uwezo wa kuvamia na kushambulia tishu nyingine na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine mwilini kupitia mishipa ya damu au mikondo ya limfu. 


Kansa isiyotibiwa inaweza kuwa ugonjwa unaoshambulia tishu nyingine mwilini na kusabisha kifo. Kansa huusababishia mwili madhara pale inapoharibu seli na kuzifanya zigawanyike bila kudhibitika na kuwa uvimbe wa tishu unaojulikana kama tumor, isipokuwa katika saratani ya damu ambapo kansa huzuia utendaji wa kawadia wa damu kwa kuzifanya seli ziwe na mgawanyiko usio wa kawaida katika damu.

Mwili wa binadamu umeundwa kwa trilioni ya seli ambazo hukuwa, kugawanyika na kufa kwa mpangilio maalumu. Mwenendo huo ulioratibiwa vyema unasimamiwa na vinasaba au DNA vilivyo ndani ya seli. 


Wakati mtu anapokuwa mtoto mdogo au bado akiwa ndani ya tumbo la mama, seli hujigawanya kwa haraka ili kumfanya akue. Baada ya mtu kukua, seli nyingi hugawanyika kwa ajili ya kuchukua nafasi ya zile zilizozeeka na kufa au kwa ajili ya kukarabati majeraha.

Saratani huanza wakati seli katika sehemu mojawapo ya mwili zinapoanza kukua bila kudhibitiwa. Ukuaji wa seli za kansa hutofautiana na ukuaji wa kawaida wa seli za mwili, na badala ya kufa pale zinapozeeka huendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida. Seli za satarani pia hushambulia kwa kuingia ndani ya tishu nyingine jambo ambalo halishuhudiwi katika seli za kawaida. Kukua kusikodhibitiwa na kusiko kwa kawaida kwa seli na tabia ya kuzishambulia tishu nyingine ndiko husababisha seli za kansa.

Seli hugeuka na kuwa seli za kansa kwa sababu ya kuharibika DNA au vinasaba. DNA zinapatikana katika kila seli na huongoza matendo yote yanayofanywa na seli. Katika seli ya kawaida, wakati DNA inapoharibika seli huikarabati au seli hufa. Lakini katika seli za kansa, DNA iliyoharibika huwa haiwezi kukarabatiwa, na seli huwa haifi kama inavyotakiwa. Badala yake huendelea kutengeneza seli nyingine ambazo hazitakiwi na mwili, na seli hizo mpya zote huwa na DNA isiyokuwa ya kawaida tofauti na seli salama.

Watu huweza kurithi DNA isiyokuwa ya kawaida, lakini mara nyingi uharibifu wa DNA husababishwa na makosa yanayotokea wakati seli ya kawaida inapotengenezwa au kutokana na sababu za kimazingira. Ingawa inajulikana wazi kuwa, kuna baadhi ya vitu  vinavyoweza  kuharibu DNA na kusababisha kansa kama vile kemikali, uvutaji sigara, kuchomwa na jua na kadhalika lakini bado hakuna uhakika wa moja kwa moja kuhusiana na kinachosababisha kansa.

Kama tulivyosema awali, seli za kansa husababisha uvimbe au tumor, isipokuwa mara chache katika saratani ya damu au Leukemia. Kwa kawaida seli za kansa husambaa katika sehemu nyingine za mwili ambako huko nako huanza kukua na kuunda uvimbe au tumor mpya na baada ya muda kupitia tumor hizo huchukua nafasi ya tishu mpya. Kitendo cha kansa kusambaa mwilini kupitia mkondo wa damu na limfu huitwa metastasis. 

Kuna aina tofauti za kansa na majina yake hutokana na eneo la mwili ugonjwa huo unapoanzia. Kwa mfano kansa ya matiti au breast cancer iliyoenea hadi kwenye ini huitwa metastatic breast cancer yaani kansa ya matiti iliyoenea hadi kwenye ini na haiitwi kansa ya ini.

Au kansa ya tezidume iliyoenea hadi kwenye mifupa huitwa, metastatic prostate cancer na haiitwi kansa ya mifupa. Saratani tofauti huwa na viashiria tofauti kwa mfano kansa ya mapafu ni ugonjwa unaotofautiana na kansa ya ngozi. Magonjwa hayo hujidhihirisha kwa jinsi tofauti na huuathiri mwili pia kwa kasi tofauti na kwa ajili hiyo matibabu yake pia hutofautiana.

Sio kila tumor au uvimbe ni kansa, bali kuna aina ya tumor ambazo si saratani nazo huitwa benign tumors. Uvimbe huu usiokuwa saratani unaweza kuleta matatizo kama vile kukua sana na kuvibana viungo na tishu nyingine mwilini. Ingawa uvimbe usiokuwa saratani unaweza kuwa hatari kwa afya lakini hauwezi kuzishambulia seli nyingine au kusambaa katika viungo vingine mwilini. Tumor za aina hii mara nyingi hutibika na huwa hazihatarishi maisha.

Si vibaya kufahamu kuwa hii leo mamilioni ya watu duniani wanasumbuliwa na magonjwa ya saratani. Nchini Marekani pekee inakadiriwa kuwa, nusu ya wanaume wote na wanawake wote wa nchi hiyo watapatwa na magonjwa ya kansa katika maisha yao. Wataalamu wanatuambia kuwa, hatari ya kupatwa na kansa inaweza kupungua kwa kubadilisha muundo wa maisha ya mtu binafsi kwa mfano, kujiepusha na uvutaji sigara, kujiepusha kukaa juani kwa muda mrefu, kula lishe bora na kufanya mazoezi.

Baadhi ya kansa pia huweza kutambuliwa mapema kwa kufanya vipimo. Kutambuliwa mapema saratani kunamaanisha kuwepo fursa nzuri ya kuanza matibabu mapema na wataalamu wa tiba wanatuambia kuwa njia hiyo inaweza kuokoa maisha ya maelfu ya watu kila mwaka.

Kuna aina tofauti ya magonjwa ya kansa kwa kuzingatia eneo la mwili linaloshambuliwa. Baadhi ya saratani huwashambulia zaidi wanawake na kuna baadhi ambazo huwashambulia zaidi wanaume.

Baadhi ya kansa huwashambuliwa watu wa kundi fulani katika jamii kutokana na muundo wao wa maisha au kazi wanazozifanya na hali kadhalika kuna baadhi ya saratani zinazoshambulia watoto zaidi kuliko watu wazima. Katika mfululizo wa vipindi vyetu, tutazungumzia baadhi ya kansa ambazo ni maarufu katika jamii  ili tuweze kupata ufahamu wa kutosha wa kujilinda na magonjwa hayo na pia kupata ushauri wa daktari na kutibiwa mapema iwapo tutasumbuliwa na magonjwa hayo.

Wapenzi wasikilizaji kwa kuwa mwezi wa Novemba ni mwezi wa kupambana na ugonjwa wa saratani ya matiti, kipindi cha afya kinachukua fursa hii kuzungumzia ugonjwa huu.  Saratani ya matiti au Breast Cancer ni aina ya saratani ambayo hutokea katika seli za matiti. 


Kwa kawaida kansa ya aina hii hushambulia sehemu ya kutengenezea maziwa inayojulikana kama lobules na katika mishipa inayozunguka sehemu hiyo pamoja na chuchu za titi. Seli za saratani ya matiti huweza kusambaa katika sehemu nyingine za mwili. Saratani ya matiti inayoanza katika sehemu ya kutengenezea maziwa huitwa lobular carcinoma na ile inayoshambulia sehemu ya ya matiti lakini ugonjwa huu huwashambulia zaidi wanawake. 

Asilimia 16 ya wanawake wote hupata kansa ya matiti na asilimia 18 ya vifo vinavyosababishwa na kansa duniani husababishwa na saratani ya matiti. Imeonekana kuwa ugonjwa huu hushuhudiwa sana katika nchi zilizoendelea ikilinganishwa na zinazoendelea.


 Kwa kawaida wanawake wenye umri mkubwa hupata zaidi saratani ya matiti huku wanawake katika nchi tajiri wanaopata ugonjwa huu wakiishi zaidi ikilinganishwa na wale walioko kwenye nchi masikini. Pengine hilo husababishwa na tofauti ya hali ya kimaisha ya sehemu hizo. 

Taasisi ya Saratani ya Marekani imeripoti kuwa, kila mwaka wanawake 233,000 na wanaume 2,240 hupatwa na saratani ya matiti nchini humo na ugonjwa huo husababisha vifo 39,620.

Naam mpenzi msomaji tuna mengi tuliyowandaliwa kuhusiana na ugonjwa wa saratani ya matiti,endelea kutembelea blog yetu hii basi  na ujue mengi kuhusu afya yako.

   
By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 

Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.

0 comments:

 
Content By Chief Hope | Facebook | Twitter | Copyright ©2016 TIM HEAVEN