Wednesday, May 18, 2016

UNAJUA MAANA YA UPENDO KWENYE MAHUSIANO

Richard Edward | 8:57:00 AM |
MAANA YA UPENDO KWENYE MAHUSIANO
Ni jambo la kawaida kujiuliza kama unampenda Fulani au kama Fulani anakupenda. Katika tafakari hii, wengi hujikuta wakipata tafakari tofauti. Uzoefu wangu unanifanya niamini kuna maana tofauti kuu 3 zinazojitokeza miongoni mwetu wakati wa kutafakari swala la upendo katika mapenzi.
 

Soma:Wanaume tuzingatie Haya Kuhusu Wapenzi Wetu

Jiunge nami katika tafakari hii kwa kusoma jinsi watu wanavyotafsiri tofauti neno Upendo katika mahusiano:’-

1.Kujali:
Kuna wanaoamini kuwa kujali tuu inatosha kuonyesha kuwa unampenda fulani, au fulani kuonyesha anakujali basi hiyo ndio maana halisi ya upendo. Wengi hujikuta wakitumia muda mwingi kutafuta zawadi na surprises za ‘nguvu’ kama sehemu kuu ya kuonyesha upendo wao. Aina hii ya upendo inahusika sana hasa kwa watu waliopo mashuleni na vyuoni. Wengi wanaoamini maana hii ya upendo, husisitiza sana kuogopwa/kunyenyekewa kama sehemu ya kuonyeshwa kuwa nao wanapendwa.

2. Kujitoa kafara:
Katika maana hii, upendo ni swala la jinsi gani unavyojitoa kwa mwingine ili kuona anakuwa na furaha na ajihisi kuwa salama kutokana na uwepo wako. La msingi katika aina hii ya upendo ni kupenda kumfahamu vema mwenzi wako, kujua shida zake, na ndoto zake, na kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha anaona uwepesi katika shida zake, na kuwa anakuwa na matumaini ya kuwa ndoto zake zitatimia. Upendo wa namna hii huwa na subira, na huonekana zaidi kwa waliokomaa kifikra, na wenye kujiheshimu wao wenyewe.
 

Soma:Zijue Changamoto za Mahusiano ama Ndoa
 

3.Kuvutia:
Kwa wengine upendo ni namna gani wanavyovutiwa kimapenzi na mtu husika, au vile wanavyojisikia kuwa salama mbele ya mtu fulani.  Utakuta mtu anasema anampenda kaka fulani kwakuwa tuu amevutiwa na uhodari wa kijana husika katika masomo, kujiheshimu kwa kijana husika, sifa au umaarufu alionao mhusika. Na kwa upande mwingine, mtu anaweza kuvutia kwa uzuri wa sura au umbile la mtu fulani. Kutokana na mvuto wa hisia kama hizo na wakati mwingine hisia hizi za mvuto huwa kali sana, basi mtu akadhani hiyo ndiyo maana halisi ya Upendo. Wenye tafakari hii ya upendo wengi wao hawana subira na ukichukua muda mrefu kutafakari hisia hizi, unaweza kukuta ni za muda mfupi tuu.

Hitimisho:
Pamoja na ukweli kuwa mvuto wa kimapenzi kwa mtu unayejenga nae mahusiano ni muhimu. Na kwamba kujaliana na kunyenyekeana ni vigezo muhimu katika kujenga mahusiano yenye furaha, mambo hayo pekee hayatoshi kusema kuna upendo. Upendo ni jambo lisilo na ubinafsi, haliangii nafsi yako inataka kunufaika kiasi gani, bali unataka kuinufaisha nafsi ya mwingine kwa kiwango gani. Hivyo kwa upande wetu, maana ya upendo tunayoipendekeza ni Kujitoa Kafara, kama tulivyoielezea hapo juu.
Yote katika yote, inakupasa utambue kuwa upendo pekee hautoshi kujenga mahusiano yenye furaha na yenye kudumu. By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.

0 comments:

 
Content By Chief Hope | Facebook | Twitter | Copyright ©2016 TIM HEAVEN