• Isikupite Hii

  August 23, 2016

  Madhara anayopata mtoto asipo shiriki michezo na wenzake

   MADHARA ANAYOPATA MTOTO ASIPO SHIRIKI MICHEZO NA WENZAKE
  Wazazi wengi nchini na jamii nyingine wanapenda kuwaona watoto wao wakiwa kama wao walivyokuwa enzi hizo.Kwa maana nyingine wanataka kuwaona watoto wao wakiwa kama nakala zao.


  Watoto wa umri kati ya miaka 3-12(ni umri kabla ya kuanza shule na kuanza shule) huonyesha tabia za kutaka kufanya vitu wenyewe bila kuzuiliwa na mtu yeyote. 

  Hupenda kujifunza lugha, na ishara mbalimbali kwa kasi isiyo ya kawaida. Hapa wazazi wengi huwachukulia watoto wao kuwa ni watundu na wasumbufu,la hasha! Ni umri wao kutaka kujifunza kuhusu mambo yanayowazunguka.

  Kama mwanasaikolojia, Maria Montessori alivyoainisha kuhusu makuzi ya watoto, anasema kuwa watoto wa  rika hili hupenda kuwa na urafiki na watoto wa rika lao. 

  Pia kuhusu kuwaruhusu watoto wafanye vitu wanavyoweza kufanya na si kulazimisha kuwasaidia.Alisema, "Never help a child with a task at which he feels he can succeed." Yaani “Usimsaidie mtoto kufanya kazi iliyo kwenye uwezo wake.”

  Kiuhalisia makuzi ya watoto hutegemea sana mazingira, mfano mtoto aliyekulia mazingira ya shida na duni kiuchumi anatofautiana sana kiutendaji na yule aliyetokea mazingira ya raha na furaha na uchumi mzuri.

  Tofauti hii ambayo inahusisha saikolojia ya makuzi ya mtoto, ina uwezo mkubwa sana wa kushusha au kuongeza/kuimarisha utendaji wa mtoto afikiapo utu uzima.

  Nitazungumzia tofauti za watoto katika mazingira hayo mawili katika makala nyingine.Leo napenda uungane nami katika kuyajua madhara (8) ya kumzuia mtoto wako kushiriki michezo ya kawaida na wenzake...

  Mwanasaikolojia maarufu duniani Erick Erickson 1956 aliainisha hatua nane(8) za maendeleo ya makuzi ya binadamu kijamii na kihisia kuanzia kuzaliwa hadi utu uzima.Alisisitiza kuwa kila hatua ina vipingamizi vyake ni muhimu kupitia kila hatua na kuondoa vipingamizi hivyo kabla ya kwenda hatua nyingine. 

  Nitapenda kujikita hasa kwenye makuzi ya watoto ambayo yana mchango mkubwa kwa utu uzima wa mtu.Nikizingatia hatua mbili za makuzi ya mtoto yaani hatua ya 2 na hatua ya 3 za maendeleo ya ukuaji wa mtoto kama alivyozielezea Erickson;

  Katika hatua ya pili (2) umri wa mtoto kabla ya kuanza shule (chekechea), aliangalia mambo mawili yanayopingana yaani “Kujifunza mwenyewe Vs Aibu (miaka 3-4)”.Akimaanisha kuwa mtoto wa umri huu hupenda kufanya mambo mwenyewe na hujisikia aibu pale anapokatazwa kwa kuambiwa “Usi…” Mtoto aliyekuzwa vizuri hujisikia vizuri bila kuwa na aibu yoyote.

  Pia katika hatua ya tatu (3) umri wa kuanza shule (baada ya chekechea), umri wa michezo, mtoto hupambana na vitu viwili yanayopingana yaani Kujianzishia kujifunza Vs Kujilaumu/Hatia.(miaka 4-12). Akimaanisha kuwa mtoto aliyekuzwa vizuri kwa kupewa uhuru wa kujifunza (1) hujiona fahari kuwa na wenzake,(2) hupenda kushirikiana na wenzake, (3) hupenda kuongoza pia kuongozwa.

  Kwa upande mwingine, mtoto aliyekuzwa mazingira ya kubanwa hujihisi kuwa na hatia hivyo (1) huwa muoga (2) hujitenga na wenzake (3) anakuwa tegemezi sana kwa wazazi (4) anakuwa amekosa mbinu za michezo na uwezo wa ubunifu.

  Nitayajumuisha madhara (8) ayapatayo mtoto wako kwa kukosa kushiriki michezo ya kitoto na wenzake kama ifuatavyo;

  1. Mtoto kukosa uwezo wa kujiamini mbele ya hadhara 

  Ukifuatilia michezo ya watoto kama mpira,kukimbizana, na mingine mingi utagundua kuwa watoto ni waongeaji na watendaji hasa wakiwa na watoto wa rika lao.

  Endapo mtoto wako atakosa fursa ya kukutana na wenzake, kwanza atakuwa na hofu-kwasababu hajawazoea, pili atajihisi mnyonge mbele ya wenzake.Hivyo kuanza kuijenga tabia ya kutokujiamini tangu utotoni.

  2. Kukosa uwezo wa kuongoza 

  Kutokana na hofu aliyojingea tangu utotoni, ni dhahiri kuwa atakuwa hana mbinu za kuwasiliana kama kiongozi, pia atakuwa na aibu iliyopitiliza mbele ya watu anaotakiwa kuwaongoza.

  3. Kuwa mtegemezi wa maamuzi mbali mbali kwa wazazi hata yaliyo kwenye uwezo wake

  Tatizo hili ni kubwa, limepelekea vijana wengi kushindwa kuamua mambo yao wenyewe, eti “labla nimuulize baba na mama”, kazi lazima achaguliwe na wazazi/walezi.

  Hili ni tatizo lililokuwa tangu utotoni, yaani kukosa uwezo wa kuamua kufanya hasa baada ya kuambiwa “Usi…” na kutopata nafasi ya kuona watoto wengine wakijaribu kufanya jambo fulani.

  4. Mtoto hujitenga na jamii 

  Kwa kuwa mzazi au mlezi ulimtenga mtoto na jamii kwa kumfungia ndani wakati wote, na kumwachia mtoto wako awe na urafiki mkubwa na Televisheni na michezo yake pekee, usitegemee kuona mtoto wako akiwa mbali na jamii hasa afikapo ujana na hata utu uzima.

  5. Kukosa uwezo na mbinu za kuwasiliana

  Kama nilivyoeleza awali, watoto wa umri huu hupenda kujifunza lugha na ishara mbali mbali za mawasiliano wakiwa na watoto wa rika lao.

  Hivyo basi, kama utamfungia mtoto wakati wote asikutane na wenzake, tambua kuwa unamwandaa mtoto ambaye atakuwa hana uwezo mzuri kimawasiliano.Ujuzi huu ni muhimu sana katika shughuli mbali mbali za kijamii.

  6. Kuwa na viungo dhaifu na kukosa uchangamfu wa mwili 

  Itafahamika kuwa uimara wa viungo vya mtoto haujengwi na vyakula pekee, bali mazoezi ya viungo hasa kwa michezo ya kitoto ya kukimbizana hapa na pale.

  Kisaikolojia, mtoto huathirika sana anapoona watoto wengine wakicheza kwa furaha wakati yeye anazuiliwa ama kwa kupigwa na kukaripiwa.Hii humfanya mtoto kunyongea na kukosa uchangamfu.

  7. Humpelekea mtoto kujitengenezea tabia ya kutoroka ili atimize hisia zake 

  Hapa ndipo utukutu na tabia mbaya zinapoanzia.Mtoto anaamua kujitengenezea mbinu ili aweze kushiriki kwenye michezo ya kitoto.

  Mtoto anapofikia hatua hii, wazazi wengi hulaumu sana kuwa watoto wa siku hizi hawatulii, wakiwa wamesahau kuwa wenyewe ndiyo chanzo cha kuwafanya watoto watoroke kwasababu ya ulinzi mkali nyumbani. 

  Mtoto hawezi kutoroka nyumbani kama anapata upendo na kueleweshwa mema na mabaya kwa vitendo, pia kwa kumpa na kukubaliana utaratibu wa michezo.

  8. Mtoto kukosa ubunifu wenye tija ya kupambana na changamoto za maisha

  Ubunifu wa mtoto unachangiwa na kuwepo kwa ushirikiano wake na watoto wenzake.Ni hapo kipaji cha mtoto kinapojidhirisha. Kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, wazazi wengi wamewaachia watoto wao kutazama televisheni na komputa na si kwenda kucheza na watoto wengine.

  Naomba nitoe rai kwa wazazi wa karne hii ambao mnakumbana na changamoto mbali mbali za mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kiasi kwamba mnakuwa hamna muda wa kukaa na watoto, ila ni kutoa amri kuwa hairuhusiwi mtoto kutoka nje.

  Pia ni vizuri kufuatilia kila hatua ya ukuaji wa mtoto na kuhakikisha yale mahitaji ya hatua husika yanafikiwa, kinyume na hapo tusishangae kuona watoto wetu wamekuwa vile tusivyotarajia.