• Isikupite Hii

  December 31, 2016

  Anza mwaka 2017 kwa kujiwekea malengo haya.

   ANZA MWAKA 2017 KWA KUJIWEKEA MALENGO HAYA
  1: Malengo ya Biashara na Uwekezaji.
  Yawezekana ulivyosoma aina hiyo ya malengo umejisikia vibaya kutokana na wewe ni mtu husiyependa masuala ya biashara au hautegemei kufanya biashara kabisa katika maisha yako. Lakini ukweli ni kwamba unahitaji kutambua ili uweze kufikia uhuru wa kweli wa kifedha na utajiri wa kudumu unahitaji kuwa mfanyabiashara na mtu mwenye tabia ya kuwekeza, basi hata kama hutofanya biashara ni vizuri ujifunze kuwekeza. Ndio maana nimeyaita malengo ya biashara na kuwekeza. Unaweza kuwekeza pasipo kufanya biashara, unaweza kuwekeza ukiwa bado umeajiriwa.

  Isikupite Hii: Somo La Fursa Kutoka Kwa Watu Waliofanikiwa

  Kwa mfano mzuri wa malengo haya: Kama wewe ni mtu uliyeajiriwa au ni mtu uliye na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa hapo badae ni muhimu uwe na malengo yanayoweza kukufikisha katika kutimiza ndoto yako ya kuwa mfanyabishara mkubwa.

  2: Malengo ya Ki-familia.
  Unahitaji uishi wapi? Unahitaji kuoa au kuolewa na nani? Unahitaji uwe na watoto wangapi? Unahitaji familia yako iwe kwenye mfumo upi (family life style)?  nakadhalika. Ni muhimu sana ufahamu ni nini unachokitaka juu ya maisha yako binafsi na familia yako kiujumla. Hebu fikiria kama hautopanga wewe kuhusu mfumo fulani unaoutaka katika maisha yako ni nani mwingine atakayekupangia mfumo huo wa maisha? Jifunze kuweka malengo kwa ajili ya familia yako na kuyafatilia mara kwa mara. Hata kama hauna familia muda huu ila weka malengo yatakayokuongoza kujua ni familia ya namna gani unayoitaka itakayoendana na ndoto na kusudi la Mungu katika maisha yako.

  3: Malengo ya Ki-afya.
  Jiulize ni aina gani ya mwili unaoutaka? Unataka uwe namna gani kiafya miaka mitano kutokea sasa? Si watu wengi sana wana tabia ya kujiwekea malengo kwa ajili ya afya zao, na hii ndio sababu watu wengi wamekwama kutokana kuegemea zaidi upande wa malengo ya fedha na mali na kusahau kuwa hauwezi kutafuta fedha au mali kama hauna afya iliyo imara. Brian Tracy mwalimu wa masuala ya maendeleo ya mtu binafsi aliwahi kuuliza swali, “How would your health be different if it was perfect in every way?” Ni muhimu sana uweke afya yako kama kipaumbele cha kwanza katika maisha yako, kwani utakapokuwa na afya njema ndio utakapoweza kufanya mambo mengi ya maendeleo.

  Isikupite Hii: Vitu 24 Vya Kuvikumbuka Mara Zote

  Ni vizuri ufahamu vyakula unavyopendelea kula ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kujenga afya yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayoyataka na si kula kila chakula unachokutana nacho. Mtu mwenye maono makubwa katika maisha yake huwa si mtu wa kupenda kula kila kitu, kwa sababu si kila chakula kinaweza kuleta hatima njema juu ya maisha yako ya badae. Kama leo hautoweza kuwa makini juu ya afya yako na ukaishia kuwa mlevi, mvutaji, kula vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi kama vile soda, keki, nakadhalika; uwe na uhakika kwa kufanya hivyo ni vigumu sana kufikia malengo yako mapema na unaweza kupata magonjwa yanayoweza kuwa sababu ya kuzuia kuona mafanikio uliyokuwa ukiyatarajia maishani mwako.

  Kama wewe ni mtumiaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi ni vizuri uweke malengo ya kuanza kupunguza taratibu vitu hivyo na badae unaweza kuacha kabisa ili uweze kutengeneza nafasi nzuri ya kufikia ndoto zako maishani. Amini inawezekana kama ukiamua kuchukua hatua leo hii, mimi niliweza kufanya na nikaweza kwa nini wewe ushindwe! Amini inawezekana na linda afya yako kwa faida ya maisha yako ya badae na ndoto uliyonayo.

  4: Malengo ya kifedha na mali.
  Ni kiasi gani cha fedha unachotaka umiliki miaka mitano kutokea sasa? Ni kiwango gani cha mali au utajiri unachotaka kuwa nacho miaka mitano kutokea sasa? Usipojua fedha unazotaka kumiliki huwezi kupata fedha hizo kwa sababu hata ukipata fedha nyingi utaona nyingi na utashindwa kufanyia chochote kwa sababu haukuweka lengo linalokuongoza katika fedha zako unazohitaji. Kuwa na malengo ya kifedha ni muhimu sana kwa kutokea mwezi hadi mwaka, miaka mitano nakuendelea. Unapokosa malengo ya kifedha ni rahisi sana kuona una fedha nyingi pale unapozipata kumbe si nyingi kama unavyofikiri.

  5: Malengo ya Hekima, Maarifa na Ufahamu.
  Naamini watu wengi ndio wanaosikia aina hii ya malengo mahali hapa. Lakini ukweli ni kwamba unahitaji kuwa na aina hii ya malengo kama unahitaji kukua kiufahamu, kuongeza maarifa ndani yako na kufanya mambo yako kwa ufanisi na umakini katika maisha yako. Mwaka 2007 nilianza tabia ya kujisomea sana vitabu hasa vitabu vya kiroho zaidi, lakini nilikuwa ni mtu niliyekuwa nasoma vitabu pasipo malengo kwa kipindi hicho. Kitabu kimoja nilikuwa nakisoma kwa mwezi mzima hata miezi miwili na badae sisomi tena hadi nitakapopata hamu nyingine ya kusoma. Lakini muda si mrefu baada ya kukutana na ushuhuda wa Warren Buffett tajiri nambari tatu duniani, nilipokuwa nikifatilia historia ya maisha yake nikakuta yeye ni mtu anayesoma kurasa 80 hadi 100 kwa siku, jambo hili lilinishangaza sana. Nikajiuliza huyu mtu ni tajiri sana duniani na bado anasoma kurasa 80 hadi 100 kwa siku, mimi ni nani na hali niliyonayo nasoma kitabu kimoja kwa mwezi tena kwa uvivu mkubwa?

  Isikupite Hii: Utajengaje Tabia Bora Na Za Kudumu Katika Mafanikio Yako!!

  Hapo ndio maisha yangu ya kusoma yakabadilika na hii ni baada ya kujiwekea malengo kuwa kila mwezi nisome vitabu 4 ambapo kwa mwaka visipungue vitabu 48 hadi 50. Nikaamua kuweka malengo na maudhui ya vitabu gani vya kusoma, nikawa ni mtu wa kusoma vitabu vya kiroho, vitabu vya watu waliofanikiwa, maendeleo ya mtu binafsi, fedha na uwekezaji, biashara na ujasiriamali, nakadhalika. Leo hii ufahamu wangu wa miaka hii ni tofauti sana na ufahamu wangu wa miaka ile ya 2007 nilipokuwa nasoma huku sina malengo maalum ya kusoma kwangu. Maarifa niliyopata yamekuwa na matokeo makubwa sana katika maisha yangu kuliko maelezo ninayoweza kutoa hapa siku ya leo kwani ni mengi sana hayatoisha. Amini nawe unaweza kama ukiamua kufanya hivyo, unapaswa kuelewa maarifa ni muhimu sana kuliko fedha unayopata. Mtu mwenye maarifa anaweza kuja kwako na akabeba fedha zako ulizonazo kwa kitu kidogo sana ambacho na wewe ungeamua kuchukua hatua ya kujifunza ungekifahamu na ukalinda fedha yako. Si lazima urudi darasani kusoma tena, ila ukiamua kujifunza utajifunza tu hata katika mazingira yoyote yale yanayokupa maarifa katika dunia hii ya leo.

  6: Malengo ya Kitabia.
  Jiulize ni tabia gani uliyonayo inayokufanya usipige hatua mbele na kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji? Je, unapenda kulala sana? Je, unapenda sana kushinda vijiweni na kusema watu wengine? Je, unapenda sana kuangalia tamthilia, movie au TV, kuchati kwenye simu na mitandao ya kijamii kuliko kusoma vitabu? Je, unapenda sana kusafiri hata safari zisizo na maana zinazokupotezea fedha? Je, unapenda sana kula na kunywa vitu vyenye sukari nyingi kama vile soda, keki, ( na vingine kama vile ice cream, candy bars, processed meat au soseji, low-fat yogurt, nakadhalika)? Je, wewe ni mvivu sana wa kujituma hata katika majukumu yako uliyonayo? Je, una hasira au wivu mbaya kwa wengine? Kwa tabia hizo nilizotaja na nyingine nyingi ambazo sijaandika hapa ni vizuri uangalie ni tabia gani inayokusumbua leo hii na kukufanya usifanikiwe katika kufikia mafanikio unayoyataka.

  Isikupite Hii: Njia Kuu Nne Za Kuweka Akiba

  Weka malengo ya kuamua kuacha tabia zote mbaya zinazokusumbua ili uweze kufanikisha malengo na ndoto yako kubwa uliyonayo maishani mwako. Ni vigumu sana kwa mtu yoyote kufanikiwa kama ataendelea kuwa kwenye tabia zinazomfanya kuwa kwenye kundi la watu wasiofanikiwa, kama unahitaji mafanikio ni vizuri uanze kujenga tabia nzuri zinazoweza kukufanya uwe miongoni mwa watu walio kwenye njia ya kutimiza ndoto zao na waliofanikiwa. Kwa mfano kama wewe ni mtu mwenye hasira sana na mtu mwenye kupenda kutangaza mambo yako ovyo kwa watu wengine, ni vizuri uanze kujenga tabia ya kujizuia kufanya hivyo, tafuta maarifa yanayoweza kukufanya uondokane na tabia hizo leo hii na kidogo kidogo amini utaweza na utafanikiwa.

  7: Malengo ya kiroho.
  Malengo haya nimeyaweka mwishoni nikiwa na maana kubwa sana, kumbuka wa mwisho atakuwa wa kwanza. Ndio. Malengo haya ni muhimu sana kwako kuliko malengo mengine yoyote yale maishani mwako na hii ndio sababu ya kuyaweka mwishoni ili uweze kuyakumbuka utakapomaliza kusoma makala hii. Watu wengi sana ni wepesi wa kujiwekea malengo ya kifedha, mapato, mahusiano, biashara, uwekezaji, nakadhalika; lakini si watu wepesi wa kujiwekea malengo ya kiroho ambayo ndio muhimu zaidi kwa ajili ya maisha yao hapa duniani. Nataka nikuambie tunaishi duniani tukitumikia kusudi na ndoto zetu tulizonazo, lakini ni muhimu kuelewa kuwa kuna maisha baada ya maisha haya tunayoishi sasa, hivyo ni vyema niwe wazi kwako kuwa unahitaji kuwa na malengo kwa ajili ya maisha yako ya badae baada ya kuondoka duniani.

  Isikupite Hii: Unazijua Sala Muhimu Unazopaswa Kusali Kila Siku!!

  Haina haja ya kutafuta fedha na mali nyingi kisha wewe binafsi ukaishia maisha mabaya baada ya kufa. Ni muhimu kuweka malengo yako ya kiroho na imani juu ya maisha yako. Kumtumikia Mungu ni sehemu ya baraka na amani katika maisha yako ya sasa na ya badae. Hivyo basi, ni muhimu sana tena sana kuwa na malengo kwa ajili ya hali yako ya kiroho ya sasa na ya badae. Jiulize unataka uwe wapi kiroho baada ya miaka mitano kutokea sasa? Je, unataka utumike wapi kiroho au kwenye nafasi ipi? Je, una malengo gani kuhusu ibada kwa siku za jumapili na ijumaa au jumamosi? Kuna watu ni wepesi sana kutafuta fedha ila si wepesi kumtafuta Mungu na kuwa na ibada nae mara kwa mara. Nakushauri ni vizuri uwe ni mtu mwenye malengo ya kiroho kuhusu maisha yako ya sasa na badae kwani pamoja na kutafuta maisha mazuri leo hii lakini bado hatujui siku wala saa ya kuondoka kwetu.

  Isikupite Hii: Misemo 6 Inayokwamisha Ndoto Na Mafanikio Yako.

  Hizo ndio aina saba za malengo nilizokuandalia leo hii katika makala hii. Aina nyingine za malengo unazoweza kuwa nazo ni pamoja na malengo ya mapato yako (income), malengo ya kazi na huduma, malengo ya mahusiano (networking), malengo ya kijamii na kuendeleza kipaji, nakadhalika, kutokana na wewe utakavyojiwekea. Ila nimeona nikuandalie zile aina saba ikiwa ni malengo muhimu sana kwa ajili ya kukusukuma kuchukua hatua kwa ajili ya kuanza kuifata ndoto yako. Unaweza kuongeza na aina nyingine nilizokutajia kama sehemu ya malengo yako.

  By Richard Edward 

  Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
  Kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari, makala juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.