Featured Posts

October 13, 2016

Hasara za kulipiza kisasi - Mwalimu Christopher Mwakasege.

Usilipize Kisasi! Unasikia? Hata ikiwa umefanyiwa ubaya wa namna gani, Biblia inafundisha na inakusihi usilipize kisasi kwa huyo aliyekufanyia ubaya. Biblia inasema hivi:

"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena Bwana" (Warumi 12:19)

Kuna hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo! Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".

Lakini ikiwa utaona ya kuwa Mungu hawezi kukusaidia na ukaamua kujichukulia madaraka ya kujilipiza kisasi hasara zifuatazo hakika zitakupata!

Hasara ya Kwanza "UTASHINDWA!"
Katika jambo lolote lile lililokukasirisha - liwe la kidini, au kikabila, au kifamilia, au kikazi, na kadhalika ukiamua kulipa kisasi utashindwa wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili! Tunasema hivi kwa sababu katika 2 Wakorintho 10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".

Soma: Tabia 8 Za Watu Wapole - Dr. Chris Mauki.

Tena katika kitabu cha Waefeso 6:12 imeandikwa hivi: "Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".

Uwanja wa mapambano uliyonayo ni "katika ulimwengu wa roho" na mapambano uliyo nayo "si juu ya damu na nyama" - ingawa unaona ya kuwa ni watu na ni binadamu kama wewe wanaokusonga - lakini fahamu hili ya kuwa wanatumiwa tu na ibilisi!

Mbinu mojawapo ya shetani anayotumia akitaka kukuangamiza ni kukufanyia kitu kitakachokukasirisha ili uamue kujibu au kushindana kimwili kwa sababu anajua ukishindana "kimwili" au katika mwili utashindwa hakika, maana vita hivyo si vya mwili wala silaha ambazo Mungu amekupa si za mwili!

Hasara ya Pili "MATATIZO HAYATAKWISHA!"
Kumbuka imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 6:7; "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote ampandacho mtu. Ndicho atakachovuna".

Ikiwa umeamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule aliyekufanyia - ubaya hautakwisha, kwa sababu utavuna ulichopanda.Ndiyo maana imeandikwa hivi:"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya hayataondoka nyumbani mwake" (Mithali 17:13)

Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako - Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.

Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue hakika mabaya hayataondoka nchini mwako. Hili ndilo lililowapata wenzetu wa nchi za Burundi na Rwanda - kulipizana kisasi - matokeo ni uhasama usiotaka kupotea - pamoja na juhudi zote za kimataifa kutafuta suluhisho.

Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa kazini kwako - fahamu mabaya hayataondoka kazini kwako. Ikiwa ni shuleni - mabaya hayataondoka hapo shuleni.

Tena hali ya mwisho inakuwa mbaya zaidi,kila wakati kisasi kinapoendelea kupandwa. Kwa sababu ukiwapa watu ubaya - nawe utapewa ubaya kwa; "kipimo cha kujaa na kushidiliwa, na kusukwa sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile upimacho ndicho mtakachopimiwa" (Luka 6:38)

Soma: Jifunze Kusamehe - Mwalimu Christopher Mwakasege

Kumbuka ubaya haushindwi na ubaya mwingine, bali unashindwa na wema kama vile dawa ya chuki si chuki bali upendo! Ndiyo maana Warumi 12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".


By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 

Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.