May 2, 2015

SOMO: KIFO CHA MTU ALIYEOKOKA - ASKOFU ZACHARY KAKOBE

Askofu Zachary Kakobe
Kuna mambo mengi sana ya kujifunza katika Kitabu cha YOHANA. Leo, tunaendelea kujifunza Kitabu hiki katika Biblia zetu, kwa kutafakari kwa makini YOHANA 11:1-16. Katika mistari hii, tunasoma juu ya kifo cha Lazaro, na hivyo kujifunza juu ya KIFO CHA MTU ALIYEOKOKA. Hata hivyo, kuna mafundisho mengi yanayoambatana, tunayojifunza hapa. Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi na moja:-


1. UPENDO WA KINDUGU KATIKA UGONJWA (MST. 1-3)

Lazaro alikuwa hawezi, yaani alikuwa mgonjwa. Mtu huyu alikuwa anakaa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Siyo kwamba mji huu ulikuwa mali ya Mariamu na Martha, bali lugha hii ilitumika kueleza kwamba mji huo ndiyo pia walipokuwa wanakaa Mariamu na Martha (YOHANA 1:44). Mariamu huyu, ndiye aliyempaka Yesu marhamu (YOHANA 12:3). Akina dada hawa walipoona kaka yao Lazaro anaumwa, walihusika sana na ugonjwa wake na wakapeleka ujumbe kwa Yesu. Sisi nasi kama watu tuliookoka, inatupasa kuhurumiana na kupendana kama ndugu, kwa kuonyesha upendo wa kindugu kivitendo, katika magonjwa ya ndugu zetu katika Kristo (1 PETRO 3:8; WARUMI 15:1). Katika makanisa yetu ya Nyumbgani, tunapaswa kuangaliana sisi kwa sisi katika hali za ugonjwa, na kumpelekea Yesu ujumbe, na kumweleza juu ya kaka na dada zetu katika Kristo wanaoumwa kwa kuwaombea (WAEBRANIA 10:24; 2 WAFALME 8:29; MST. 3). Ndiyo maana ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujiunga na Kanisa mojawapo la Nyumbani ili kupata nafasi ya kuonyesha upendo huu kivitendo. Yesu, anahusika sana na ndugu zetu wanaoumwa tunapomwomba (MARKO 1:29-31).


2. KUUGUA KWA WATU WALIOOKOKA (MST. 3)

“Yeye umpendaye hawezi“. Yesu alikuwa anampenda Lazaro, kudhihirisha kwamba Lazaro alikuwa ameokoka (YOHANA 14:21). Hata hivyo, hapa tunaona kwamba Lazaro alikuwa anaumwa. Kuugua kwa mtu aliyeokoka, siyo jambo la ajabu (2 WAKORINTHO 5:2-4; 2 TIMOTHEO 4:20; WAFILIPI 2:25-27). Hata hivyo, kwa kuwa Yesu anatupenda, tukimwita katika ugonjwa, ataitika na kutuponya sawasawa na ahadi zake (YEREMIA 33:3; 30:17).


3. UGONJWA HUU SI WA MAUTI (MST. 4)

Ugonjwa wa mtu aliyeokoka, hata kama ni wa kutisha kiasi gani, si wa mauti; kwa maana kwamba, si wa MAUTI YA MILELE, maana juu yake huyo, mauti ya pili au ya milele, HAINA NGUVU (UFUNUO 20:6). Kwa hali hii, Shetani hapaswi kutubabaisha, kwa kututishia kutuua. Tunajifunza pia hapa kwamba siyo kila ugonjwa unaokuja kwetu unakukja kutuua (YOHANA 9:1-2). Magonjwa mengine anayoleta Shetani kwetu, hatimaye humletea Mungu utukufu mkubwa pale anapotuponya kwa miujiza.


4. UTUKUFU WA MUNGU HUONEKANA KATIKA MATATIZO (MST.4)

Hatuna haja ya kuogopa kukutana na matatizo au majaribu katika maisha yetu ya kimwili na kiroho. Kwa kutumia matatizo yanayotukabili, Mungu hujipatia utukufu, na kutuonyesha jinsi alivyo na uwezo wa kutupigania. Tukimwomba Mungu halafu akatushindia kwa kututoa katika matatizo hayo, tunajengewa imani zaidi ya kumtumaini na kuwa karibu naye. Uweza wa Mungu, huonekana sana pale tunapokuwa na matatizo au udhaifu na ndipo tunapojengeka kiimani. Kwa sababu hii, Paulo Mtume, hakuogopa matatizo, bali alipendezwa nayo! (2 WAKORINTHO 12:9-10). Bila Bahari ya Shamu, tutauonaje uwezo wa Mungu wa kuigawa bahari? Bwana atupe neema ya kutokubabaishwa na matatizo katika Jina la Yesu.5. UPENDO WA MUNGU KATIKA KUCHELEWA KUSHUGHULIKA NA MATATIZO 

YETU (MST. 5-6)

Pamoja na Yesu kumpenda Martha na umbu lake yaani, dada yake Mariamu, pamoja na kaka yao Lazaro, hata hivyo, hakushughulikia tatizo lao haraka! Yesu alijua wakati mzuri zaidi wa kujipatia utukufu mkubwa zaidi. Akangoja Lazaro afe, ili amfufue, badala ya kumponya. Angemponya tu katika ugonjwa wake, usingekuwa muujiza mkubwa wa kumpa utukufu mkubwa. Tunapoona Mungu amechelewa kutujibu, siyo kana kwamba hatupendi au tumekosea, la hasha. Yeye anajua wakati mzuri zaidi wa kutupa majibu ya mahitaji yetu, kwa utukufu wake (ISAYA 54:7-8). Wakati tunapoona matumaini yetu yametupotea, ndipo Yesu anapotujulisha kuwa ndiye BWANA muweza yote (EZEKIELI 37:11,13).6. KUSAMEHE NA KUSAHAU (MST. 7-8)

Wakati huu, ilikuwa yapata miezi miwili, tangu Yesu Kristo alipotafutwa kupigwa kwa mawe na Wayahudi. Yesu alikwisha kuwasamehe na kusahau, lakini kwa wanafunzi wa Yesu, mambo ya miezi miwili iliyopita, wanayita ya JUZIJUZI! Ndivyo walivyo watu wengi, wanakuwa wagumu kusamehe na kusahau! Tuige mfano wa Yesu na kumwomba atuwezeshe kuwa kama yeye.7. MTU AKIENDA MCHANA, HAJIKWAI (MST. 9-10)

Wanafunzi walimwuliza Yesu, “unakwenda huko tena walipotafuta kukupiga kwa mawe?“ Akajibu, mtu akienda mchana hajikwai maana aiona nuru! Maana yake ni kwamba, alikuwa anakwenda kwa sababu alipokea neno, agizo, au ufunuo wa kufanya hivyo kutoka kwa Baba yake. Neno hili, lilikuwa nuru au taa na mwanga wa njia yake, hivyo asingeweza kujikwaa! (ZABURI 119:105). Tukipata ufunuo halisi wa neno kutoka kwa Mungu (RHEMA), neno hilo hutupa imani inayotuhakikishia kutokujikwaa. Ni muhimu kuutafuta uso wa Mungu kabla ya kuamua kwenda mahali pa hatari.8. YESU KWETU NI RAFIKI (MST. 11)

Rafiki yetu Lazaro! Yesu, ni rafiki yetu (YOHANA 15:14-15). Kwa kuwa Yesu ni rafiki yetu, anatupenda sana (YOHANA 15:13). Anatupenda katika dhiki zetu, na kutaka kutusaidia. Siyo hilo tu, rafiki hupenda mazungumzo na rafiki yeake. Hivyo Yesu anahuzunika kutuona hatuzungumzi naye katika maombi, ikiwa Yesu kwetu ni rafiki inatukumbusha kufanya yanayompendeza ili tusimwudhi rafiki yetu.9. KIFO CHA MTU ALIYEOKOKA (MST. 11)

Lazaro AMELALA! Kufa kwa mtu aliyeokoka, ni sawa na KULALA! Kulala, ni kupumzika baada ya taabu za mchana kutwa. Vivyo hivyo, kufa kwa mtu aliyeokoka, ni kupumzika baada ya taabu za dunia (UFUNUO 14:13). Hatupaswi kuogopa kifo tunapokuwa tumeokoka. Mtu aliyeokoka, anapokufa, roho yake HUMIMINWA na kuwekwa kwenye mwili mzuri sana wa mbinguni, kama mafuta yanayomwagika, yanavyotolewa kwenye chombo kibovu na kumiminwa kwenye chombo kizuri (2 TIMOTHEO 4:6; 1 WAKORINTHO 15:40). Hata hivyo, mtu ambaye hajaokoka haendi kupumzika anapokufa, bali anakwenda kuumizwa kwenye mateso! (LUKA 16:24-25). Wayunani, waliyaita makaburi, “KOIMETERIA“. Kutokana na neno hili tunapata neno la Kiingereza, DORMITORIES au mabweni, mahali pa kulala au kupumzika.


11. UWEZEKANO WA WANAFUNZI WA YESU KUTOKULIELEWA NENO LA 

MUNGU (MST. 12-14)

Yesu aliposema Lazaro amelala, alikuwa anatumia lugha ya Biblia, inayomaanisha amekufa (MWANZO 47:29-30; KUMBUKUMBU 31:16; 2 WAFALME 8:24; MATENDO 7:59-60; 8:2). Hata hivyo, pamoja na wanafunzi wa Yesu kusoma Agano la Kale, hapa hawakumuelewa Yesu. Wakasema ikiwa amelala, atapona. Waliwaza kwamba “Ikiwa Yesu anasema amelala, huenda sasa amepata nafuu ya kuweza kupata usingizi, maana inaelekea mwanzoni, hali ilikuwa mbaya kiasi ya kwamba alikuwa halali“. Hapa tunajifunza uwezekano wa wanafunzi wa Yesu kutokulielewa neno la Mungu. Inatupasa kumwaomba Yesu atufunulie akili, ili tupate kulielewa Neno la Mungu (LUKA 24:44-45).12. WAJIBU WA KUTIANA MOYO KUSONGA MBELE (MST. 15-16)

Wanafunzi wa Yesu, walijua kwamba suala la Yesu kwenda Uyahudi tena, ilikuwa kwenda kufa, hivyo hawakuwa na utayari. Hata hivyo, baadaye Tomaso anawaambia wenzake “Twendeni na sisi ili tufe pamoja naye“. Anawatia moyo wenzake kusonga mbele bila kujali majaribu yaliyo mbele yetu. Jina Tomaso linatokana na jina la Kiebrania “THOMIM“, lenye maana “PACHA“.

………………………………………………………………………

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!! 

Source: Gospel Kitaa