Featured Posts

August 26, 2015

NEWS: SHERIA MPYA YA MITANDAO NCHINI NA ADHABU ZAKE. (CYBER CRIME LAW)


Tarehe moja mwezi wa Tisa mwaka huu (2015) sheria mpya ya makosa ya mtandao inatarajiwa kuanza kutumika rasmi. Ni vizuri kuifahamu sheria hii mapema ili kujiepusha na adhabu mbalimbali zitakazotokana na ukiukwaji wa sheria hiyo. Ikimbukwe kwamba kutokujua sheria si sababu itakayokufanya usichukuliwe hatua.

kwanza swali la muhimu kujiuliza ni kwamba sheria hii ya makosa ya mtandao inamuhusu nani? Sheria hii kwa kifupi inamuhusu mtu yoyote anayetumia mtandao wa intaneti kupitia kifaa chochote ikiwemo kompyuta, simu za mikononi, luninga na vingine vya namna hivyo.


Watumiaji wa mitandao kama Face book, Whats app, Instagram, Twitter, barua pepe (emails), blogu na nyinginezo za aina hiyo wanapaswa kuwa makini sana na sheria hii ya makosa ya mtandao. 

Kwa leo nitaorodhesha makosa machache ambayo ni muhimu ukayaepuka pindi tu sheria hii itakapoanza kufanya kazi mnano mwezi septemba 1, 2015

Epuka kutengeneza na kusambaza ujumbe, picha zenye taarifa za uongo- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kifungo cha miezi sita ama vyote kwa pamoja.

Epuka kumtusi/kumkebehi mtu kutokana na utaifa wake, rangi yake, kabila ama dini yake- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kifungo kisichopungua mwaka mmoja ama vyote kwa pamoja.

Epuka kutengeneza na kusambaza taarifa za ubaguzi wa rangi/utaifa- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua kiasi cha shilingi milioni tatu au kifungo kisichopungua mwaka mmoja ama vyote kwa pamoja.Epuka kusambaza picha/video za ngono ama zinazoashiria vitendo vya ngono- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kifungo kisichopungua miaka saba ama vyote kwa pamoja.

Epuka kuchapisha taarifa ambazo zinaweza kusababisha umwagaji damu ama vitendo vingine visivyo vya kibinadamu- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua kiasi cha shilingi milioni kumi au kifungo kisichopungua miaka mitatu ama vyote kwa pamoja.

Epuka kutumia taarifa/jina la mtu mwingine huku ukijifanya wewe ni yeye- adhabu ya kosa hili ni pamoja na faini isiyopungua kiasi cha shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua miaka mitano ama vyote kwa pamoja. 


Hayo ni baadhi tu ya makosa ambayo tunapaswa kujiepusha nayo pindi sheria hii ya makosa ya mtandao itakapoanza kufanya kazi rasmi tarehe moja mwezi wa tisa mwaka huu (2015). Kwa kifupi jiepushe na kutengeneza ama kusambaza ujumbe/picha ambazo ni kinyume na maadili pamoja na zile zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani ama kuleta madhara/karaha kwa watu wengine.