August 27, 2015

NEWS: FAMILIA YATEKETEA KWA MOTO DAR.


Hii ni nyumba iliyoteketea kwa moto maeneo ya Buguruni Malapa


Watu tisa wa familia moja wameteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo huko Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, mashuhuda wamethibitisha.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Mtaa wa Ulam ambapo, bibi, watoto watatu wa kike na wajukuu watano waliokuwa wanaishi nyumba namba 40 wameteketea.

Mashuhuda wa tukio hilo wameliambia Mwanannchi Digital kuwa baba wa familia hiyo amenusurika kwa kuwa hakuwepo nyumbani, na kwamba alirejea baada ya kupigiwa simu na majirani kuelezwa kuzuka kwa moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao walishtuka usingizini kati ya saa nane na saa tisa usiku baada ya kusikia kelele za kuomba msaada toka kwa wanafamilia hao.

“Tulipotoka nje tulikuta moto umeshamiri na kuenea karibu nyumba nzima. Hata tulipojaribu kufanya jitihada za uokoaji tulishindwa kabisa kufanikisha jukumu hilo” walisema, kuongeza;
“Kibaya zaidi baba mwenye nyumba hakuwepo nyumbani, alikuwa kazini kwake bandarini kwani ni mwajiriwa wa kampuni ya huduma za makontena bandarini” walisema.

Mashuhuda hao walisema, wanafamilia hao wamekutwa wamekufa kwenye chumba kimoja hali inayoashiria kuwa wakiwa katika harakati za kujiokoa walijikusanya pamoja.
Majirani wamesema maofisa wa Polisi na Zimamoto walifika eneo la tukio asubuhi leo na kwamba wameanza uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo

Source; Mwananchi