September 11, 2015

Somo: Jihadhari na wajumbe walioko mwilini mwako.

King Mwangasa mchungaji kiongozi kanisa la Ufufuo na Uzima mkoani Kilimanjaro.

Hesabu 13:25-33, 14:1-10 (Yameandikwa chini ya ujumbe)

Wanasayansi wametuambia kuna milango mitano ya fahamu na hiyo hutumika kutuletea taarifa mbalimbali katika maisha yetu. Milango hii ni macho, masikio, pua, ulimi/kinywa n.k. ambavyo vyote hutumika kuleta taarifa mbalimbali ziwe njema au mbaya. Kwa bahati mbaya masikio yanapokea chochote kinachoongelewa, macho yanaona pia chochote kinachotokea mbele yako kiwe chema au kibaya, vivyo kwa mdomo hutamka chema au kibaya n.k.

Kwa wapelelezi 12 waliotumwa na Musa kwa bahati mbaya 10 kati ya 12 wajumbe walioko kwenye miili yao ikiwa ni macho 20, masikio 20, midomo 10, pua 10 n.k. wakachukua taarifa mbaya ya kujiona hawafai na hawawezi kuimili nchi wakasahau taarifa zote njema alizowapa Mungu na kwa kuona tokea Misri.
Vivyo kwa maisha yetu kuna taarifa mbaya tunazisikia kutoka kwa wajumbe tulionao katika maisha yetu na kwa kushindwa kutambua ni njia za shetani zimeleta madhara kwenye maisha yetu na hata zinafuta taarifa njema.

Mungu alijua wachawi wa Misri wanatamba kwa uchawi wa nyoka na pengine wangetaka kucharaza Musa kwa hao nyoka, lakini nyoka wa Musa akawameza nyoka wote wa wachawi wa Misri yaani wakanyang'anywa silaha zao wote na wakabaki bila silaha.

Hofu kubwa ya watu huja kutokana na majina na taarifa walizosikia kuhusu majina ya matatizo yao, lakini nina taarifa njema zisikie katika masikio yako kwamba Mungu ndiye mwenye hatima yako, anajua jibu la tatizo lako, amebeba majibu ya uhutaji wako na huyo ndiye aliyekuumba na haijalishi kuna shida gani katika mwili wako, au umepungukiwa nini katika maisha yako maadamu Muumbaji wako yupo basi ana spea ya kile kilichoharika kwako, ana spea ya kile kichochoka, ana spea ya kila unachokihitaji.

Joshua na Kalebu walijihadhari na wajumbe wavunjao Moyo walioko ndani ya miili yao, wakakaibeba taarifa njema ya Bwana Muumbaji wao, aliyewatoa Misri kwa ishara na maajabu, wakakumbuka namna Mungu alivyowaokoa na mikono ya wamisri,namna Mungu alivyowaua majeshi ya Wamisri bahari wakakumbuka kwamba Mungu amewapa nchi hiyo wakaimiliki naamu wakakataa kuzisajili taarifa mbaya katika mioyo yao.

Leo kuna ushindi wako kwa kukataa ujumbe wa wajumbe walioko mwilini mwako na madhara yao, ziondoe kila taarifa mbaya zilizoingia moyoni mwako na ruhusu taarifa njema za ushindi wako, baraka na hatima yako njema kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareth.

Hes 13:25-33, 14:1-10
"........... Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 


Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.
Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali."

Tuombe pamoja maombi haya 
"Katika jina la Yesu Kristo wa nazareth nafuta kila taarifa mbaya zilizokaa katika Moyo wangu, taarifa za kunivunja moyo, taarifa za kutopona ugonjwa nilionao, taarifa zilizonifanya niwe mtu wa kuhuzunika na kila taarifa zilizoniambia sitapata hitaji langu nazifuta kwa damu ya mwana Kondoo, taarifa za mizimu, wachawi, watu wa karibu, na maadui wote wanaotumiwa na shetani kunivunja moyo ili nisiamini taarifa njema ya Yesu Kriso nazifuta, na napokea taarifa njema za uponyaji wa ugonjwa ulinisumbua, napokea taarifa ya kushinda kila silaha zilizofanyika na zinazofanyika kwangu, napokea taarifa njema ya kuishi kwa jina la Yesu kriso, napokea taarifa ya kuishi mema aliyonikusudia Mungu, napokea taarifa ya kazi nzuri, napokea taarifa ya biashara yangu kustawi, napokea taarifa ya kufaulu masomo yangu na napokea taarifa ya kufanikiwa na kupokea majibu ya uhitaji wangu wote nilionao maana Bwana ndiye mtoaji wangu na kwake ninapata yale ninayohitaji na ninapokea baraka ya kubarikiwa nitokapo na niingiapo kwa jina la Yesu Kristo wa nazareth aliye hai. Amen"