October 21, 2015

BARUA KWAKO MPIGA KURA MWEZANGU.


Kwako ndugu mpiga kura,

Natumaina kwamba wewe pamoja na kadi yako ya kupigia kura wote mu wazima wa afya. Mimi pamoja na kadi yangu ya kupigia kura tu wazima na buheri wa afya, hofu na mashaka ni kwako ndugu mpiga kura.

Dhumuni la barua hii ni kutaka kukujuza kwamba uchaguzi wa mwaka huu sio uchaguzi wala ushabiki tu, naomba ujue ni zaidi ya hapo. Uchaguzi wa mwaka huu ni kipimo cha uwezo na akili zetu sisi kama watanzania. Ndugu mpiga kura naomba nikurudishe nyuma kidogo, ukague na uangalie kule tuliko toka na hapa tulipo, angalia raslimali pamoja na vitu ambavyo Mungu ameweka katika taifa letu kwa ajali yetu sisi watanzania, vitu ambavyo mataifa makubwa dunia kama marekani na uchina wanapigania. 

Swali langu kwako ndugu mpiga kura ni je! kuna huiano wowote kati muda tuliotumia, raslimali tulizo nazo na hapa tulipo? 

Ndugu mpiga kura wenzangu, siko hapa kukuambia ni nani anafaa kuwa rais wa nchi hii kwa miaka 5 ijayo. Niko hapa kukukumbusha kwamba sisi ndio wale watanzania ambao kwa miaka mingi tumekuwa tukilia na kulalamika juu ya ubovu wa miundo mbinu, matumizi mabaya ya mali/pesa za uma na huduma mbaya za jamii. Hizo pesa, Kofia, madela, vikoi, matisheti, matangazo, bendera, chumvi, bia za ofa pamoja na ahadi zote za uongo, ambazo wote tunajua kwamba hazita tekelezwa, zisitufanya tukasahau mateso ambayo tumekuwa tukiyapitia sisi kama watanzania. Ndugu mpiga kura, unapoenda kupiga kura hakikisha unafuata utaratibu na kanunu zote ili kura yako isiharibike, kumbuka kura yako ndio nguzo na msingi wa mabadiliko katika taifa hili. 

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRICA.

Asante sana. Wako ndugu mpiga kura mwezako.