October 8, 2015

NEWS: MCHUNGAJI MSIGWA APANDISHWA KIZIMBANI NA KUSOMEWA MASHTAKA.


Mgombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa na watu wengine watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Iringa jana na kusomewa mashtaka manne, ikiwemo la uvunjivu wa amani.

Hata hivyo, wengine sita hawakuweza kufika mahakamani hapo jana lakini mahakama hiyo imeelezwa kuwa washitakiwa hao wataunganishwa katika kesi hiyo.

Mbali na uvunjifu wa amani, mwanasiasa huyo machachari na wenzake wanakabiliwa na makosa mengine yakiwemo kuharibu mali na kujeruhi polisi.

Hata hivyo, Msigwa na wenzake wameyakana mashtaka yote waliyosomewa jana na kuachiwa baada ya kukidhi vigezo vyote vya kupewa dhamana. Kesi yao itatajwa tena Novemba 2, mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mchungaji Msigwa alikuwa ni miongoni mwa wafuasi 64 wa Chadema walitiwa mbaroni na kulala rumande usiku mmoja.

Source: Mwananchi