October 5, 2015

NEWS: MCHUNGAJI MTIKILA AFARIKI KWA AJALI YA GARI CHALINZE.


Mchungaji Christopher Mtikila (65) amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mtikila alifariki dunia jana saa 11.45 alfajiri akitokea mkoani Njombe kurejea Dar es Salaam kwa shughuli za kampeni baada ya gari aina ya Toyota Corrolla alilokuwa akisafiria pamoja na wenzake watatu kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alisema ajali hiyo ilichangiwa na mwendokasi wa gari hilo.

Alisema Mchungaji Mtikila alikuwa amekaa kiti cha mbele bila kufunga mkanda na hivyo kusababisha arushwe nje ya kupitia kioo cha mbele na gari kumlalia kifuani na kupoteza maisha papo hapo huku abiria wengine wawili na dereva wakijeruhiwa.

Mwili wa marehemu na majeruhi walipelekwa Hospitali ya Tumbi. Wengine waliojeruhiwa ni Mchungaji Patrick Mgaya (57) na Ally Mohamed (42) wote wakazi wa Dar es Salaam na dereva wa gari hilo, George Steven (31) mkazi wa Mbezi Beach aliyekuwa amekodiwa na Mchungaji Mtikila.

Source: Mwananchi.co.tz