October 19, 2015

Waziri mkuu mh. Pinda atubu na kuomba msamaha.

Jana katika Ibada ya Shukrani iliyofanyika katika Parokia ya Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimshkuru Mungu kwa kumwezusha kulitumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 15 na kuwaomba Watanzania wamsamehe kwa matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi, huenda yaliwakwaza baadhi yao.

Pinda ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa, Waziri kwa miaka miwili na nusu na Naibu Waziri kwa miaka mitano, alisema anasikia fahari kumaliza uongozi wake kwa furaha na amani.

“Katika ibada hii ya shukrani, nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi kujua. 

“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa naibu waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.

Moja ya kauli tata zilizowahi kutolewa na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma alipoviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kauli nyingine tata ni ile ya mwaka 2009 baada ya kuwaeleza wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe hawana budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.

Pinda alisema katika utumishi wake kwa umma amejifunza mambo mengi lakini kikubwa zaidi ni kujua jinsi ya kuishi na watu.

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 

Kupitia FacebookTwitterInstagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.