• Isikupite Hii

  October 13, 2015

  NEWS: MAKANISA KUFANYA IBADA JUMAMOSI KWA SABABU YA UCHAGUZI.


  Wakati zikiwa zimesalia siku kadhaa kwa Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, baadhi ya makanisa nchini Tanzania yametoa ruhusa maalum kwa viongozi wa kanisa kuendesha ibada zao Jumamosi Oktoba 24 badala ya Jumapili tarehe 25 ili kutoa nafasi kwa waumini wao kushiriki shughuli kubwa ya upigaji kura.

  Makamu wa rais wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, amesema kuwa ibada haipaswi kuzuia haki ya kimsingi na kikatiba ya waumini .

  “Si utaratibu wa kawaida kwa sababu kama baraza hatujakaa, lakini kila askofu anawajibika ndani ya jimbo lake, hivyo anaweza kutoa fursa hiyo.

  “Hata mimi katika jimbo langu la Rulenge Ngara, nimetoa kibali hicho kwa makanisa yote,'' amenukuliwa akisema Askofu Severin.

  Hadi sasa tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1961 imeongozwa na marais wanne, wa kwanza akiwa baba wa taifa hilo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akafuatiwa na Al Haji Hassan Mwinyi, baadaye Benjamin William Mkapa.

  Rais Jakaya Mrisho Kikwete anayeelekea kukamilisha muhula wake wa pili atampisha rais wa tano kuchukua madaraka mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba.

  Source: Bbc