• Isikupite Hii

  October 5, 2015

  AFYA: VIROBA HUCHANGIA SARATANI YA KOO KWA WANAUME.


  Daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa ya saratani katika Kitengo cha Patholojia, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Henry Mwakyoma na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa wameeleza hayo jijini Dar es Salaam.

  Walisema kuwa ingawa bado hakuna visababishi kamili vya saratani hiyo, asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani ya koo wamekuwa na historia ya uvutaji sigara, unywaji pombe kali kama viroba na kula aina za vyakula vilivyochomwa ikiwamo nyama na samaki, ulaji pilipili, ndimu, ‘chilisosi’ na unywaji wa vitu vya moto kupita kiasi.

  “Ongezeko ni kubwa, asilimia 90 ya wagonjwa tuliowapokea hapa wana historia ya kutumia vilevi vikali, sigara, pilipili kwa wingi na aina nyingine na vitu vinavyosababisha saratani hii,” anasema Dk Kahesa.

  Anasema kuwa Saratani ya Koo ni mbaya zaidi ukilinganisha na saratani za aina nyingine.

  Anaeleza: “Saratani ya Koo ni mbaya ukimwona mgonjwa unaweza kulia, hawezi tena kula na ikibidi huingiziwa mipira maalumu ili kupitisha chakula, lakini kuna wakati hata mipira huziba, hivyo huishi kwa dripu ya chakula pekee.”

  Naye Dk Mwakyoma anaeleza kuwa Saratani ya Koo hushambulia seli zinazotanda koo na kutengeneza uvimbe katikati ya koo ambao huanza kuleta madhara taratibu.

  “Ukiwa na Saratani ya Koo, itakuchukua muda mrefu sana mpaka kuanza kuona viashiria mbalimbali, awali mgonjwa huanza kupata shida kumeza chakula. Wengi hufika hapa wakiwa wamechelewa na tunavyofanya vipimo huwa katika hatua mbaya sana,” anasema Mwakyoma.

  Anazitaja aina kuu mbili za Saratani ya Koo kuwa ni: “Oesophagus Carcinoma na Squamous cell carcinoma, ambazo hutofautiana kulingana na jinsi seli zake zinavyoonekana kwenye darubini.

  Hata hivyo, pamoja na tofauti hizo za mwonekano, utambuzi na matibabu ya aina hizi za Saratani ya Koo hufanana.”

  Anabainisha kuwa aina zote mbili huanza kwa kuathiri seli zilizo katika utando wa ndani wa ukuta wa koo, uitwao ‘mucosa’ kabla ya kusambaa maeneo mengine.

  Kwa upande wake Dk Kahesa anasema kuwa katika hatua za awali, mgonjwa mwenye Saratani ya Koo anaweza asionyeshe dalili zozote. Hata hivyo, kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuanza kuona dalili.

  “Dalili ya kwanza ya mgonjwa wa saratani ni chakula kukwama kwenye koo, siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate.

  Maumivu wakati wa kumeza chakula, hasa chakula kigumu, maumivu kwenye kifua au mgongoni, kupungua uzito, kiungulia na sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili,” anasema.

  Hata hivyo Dk Mwakyoma anasema kuwa wapo wanaopata Saratani ya Koo kulingana kwa kurithi kutoka kwa wazazi wao pamoja na umri kuwa mkubwa aliosema pia huchangia tatizo hilo.

  “Wapo waliopata saratani kufuatana na urithi na hata umri, lakini tatizo hili pia limeshamiri sana maeneo ya Kilimanjaro, kama tunavyosema mtindo wa maisha nao unachangia. Watu wa mkoa huo wana utamaduni na kunywa pombe kali na nyama choma.”

  Anautaja mkoa unaofuatia kwa waathirika wengi wa saratani kuwa ni Dar es Salaam, ambako alisema wanapatikana watu wenye umri kuanzia miaka 45.

  “Hawa kwa makadirio huwa wameanza kukumbwa na tatizo hili wakiwa kati ya miaka 30, ambapo kadri siku zinavyosonga ndivyo saratani inavyozidi kukua, lakini mtu huyu akichelewa kupatiwa matibabu hufa haraka tofauti na aliyewahi,” anasema Mwakyoma.

  Utafiti wa Saratani ya Koo nchini

  Taasisi ya Afya ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mara ya kwanza ilifanya utafiti wa Saratani ya Koo mwaka 1983 hadi 1992 ambapo ilibaini kuwa kati wagonjwa 546 waliopimwa kulikuwa na wastani wa wagonjwa 116 wanawake huku 430 wakiwa ni wanaume.

  Utafiti huo ulifanywa na Dk Henry Mwakyoma kwa kushirikiana na Dk N Mbebati, Dk M Aboud, Dk J Kahamba na Dk C Yongolo uliokamilika Juni 1, 1994, ulibaini ukuaji wa Saratani ya Koo Kanda ya Kaskazini kwa watu wenye umri kati ya miaka 50-59.

  Dk Mwakyoma anasema kuwa licha ya utafiti huo kufanyika kwa watu wenye umri kuanzia miaka 21 hadi 90, wagonjwa wengi walikuwa wenye umri wa miaka 50-59 hali ambayo ni tofauti na sasa.

  “Wakati tunafanya utafiti huo hapa Muhimbili, ugonjwa huu ulikuwa unawakumba watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 - 59, hivi sasa vijana wadogo wa miaka 40 tunawatambua tayari wana Saratani ya Koo, ambayo hata hivyo bado ni ngumu kutibika tofauti na saratani za aina nyingine,” anasema Mwakyoma.

  Watumiaji wa vilevi

  Amos (si jina lake kamili) anasema kuwa anatumia pombe kali aina ya Konyagi, lakini si kila siku.

  “Natumia Konyagi, lakini huitumia kwa lengo la kuongeza nguvu za kiume, nikinywa huwa nahisi nguvu zinaongezeka,” anasema na kuongeza: “Lakini pombe hii ni chungu, nikinywa huwa nahisi moto katika koo langu, ikishapita huhisi ahueni.”
  Mwanamume mwingine anayevuta sigara (Hamisi) anasema kuwa hawezi kumaliza saa tatu bila ya kuvuta sigara.

  “Najisikia kukwanguliwa na kero kubwa kooni mwangu, hivyo nalazimika kutumia sigara kila wakati, nilijaribu kuacha, lakini nikahisi nitakufa, naendelea mpaka leo na nipo vizuri tu,”alisema.

  Amos alipoulizwa kuhusu ufahamu wake katika ugonjwa wa Saratani ya Koo alisema: “Mh, unaniogopesha, sijawahi kupata elimu hii ingawa nafahamu kwamba inaharibu mapafu, ila hii inanitisha. Nikipata tiba nitaacha kutumia sigara.”

  Matibabu ya Saratani ya Koo

  Dk Kahesa anasema kuwa uchaguzi wa aina gani ya tiba itumike hutegemea zaidi eneo lililoathiriwa na saratani hiyo.

  “Iwapo saratani imeshambulia viungo vilivyo karibu na koo na kusambaa hadi kufikia kwenye tezi au viungo vingine vya mwili, yaweza kutibiwa kwa kufanya upasuaji, kutumia mionzi, kutumia kemikali maalumu, au yote matatu.”

  Kwa upande wa upasuaji anasema kuwa upo wa aina tofauti ukitegemea sehemu saratani ilipo na kwamba wakati wa upasuaji sehemu iliyoathiriwa au koo lote vinaweza kuondolewa.

  Hata hivyo anafafanua kuwa kabla upasuaji haujafanyika, daktari hujadiliana na mgonjwa wake kumweleza ni aina gani ya upasuaji utakaofanyika, faida na hasara zake, na nini cha kutarajia kutokana na upasuaji huo.

  “Kuna aina ya tiba inayotumia mionzi yenye nishati kubwa kuua seli zilizoathiriwa na saratani. Kwa kawaida tiba ya mionzi huathiri seli zilizo katika eneo linalotibiwa tu.

  Pia tiba ya mionzi inaweza pia kutumika kuua seli za saratani zilizobakia mara baada ya kufanyika kwa upasuaji,” anasema.

  Anaitaja aina ya tatu kuwa ni tiba ya kemikali (Chemotherapy), akisema: “Tiba hii hutumia kemikali kuua seli zenye saratani. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa njia ya sindano kupitia kwenye mshipa wa damu wa vein.”

  Tafiti nyingine duniani

  Tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali zimeonyesha kuwa India ndiyo nchi inayoongoza kwa Saratani ya Koo kuua watu wengi kwa mwaka hali inayoelezwa kutokana na aina za vyakula vinavyoliwa na jamii hiyo, ikiwamo pilipili kwa wingi.

  Tafiti zinaeleza kuwa watu 17,460 kutoka nchini humo kati yao 13,950 wanaume na 3,510 wanawake, wamekufa mwaka 2012 kutokana na Saratani ya Koo.

  Source: Mwanacnhi.