November 23, 2015

NEWS: SHERIA ZA MAKOSA YA UKATILI WA KIJINSIA ZINA WALAKINI - ASKOFU PENGO.


Dar es Salaam. Wakati kesho Tanzania inazindua kampeni ya kuzuia ukatili wa kijinsia, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amesema sheria dhidi ya makosa hayo zina walakini ambao unahitaji kufanyiwa marekebisho ili kumlinda mtoto wa kike.

Pengo alisema licha ya sheria, pia mila na desturi zinachangia hali hiyo, hivyo ni wajibu wa jamii kubadilika na kuzikataa taratibu zote ambazo zinaondoa usawa wa kijinsia kwa wanajamii, hususan katika masuala ya elimu.

Akizungumzia msimamo wa kanisa kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanawake alipotembelewa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) nyumbani kwake Kurasini, Dar es Salaam juzi, alisema ukatili ni dhambi.

Askofu huyo alisema sheria ambazo zimetungwa kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake hazijitoshelezi na zina walakini mkubwa.

Kardinali Pengo alitoa mfano kuwa, inapotokea mtoto wa kike anapopata ujauzito na kufukuzwa shule, basi na yule wa kiume anapaswa kufukuzwa.

Alibainisha kuwa, iwapo msichana anatakiwa kujifungua na kulea mtoto wake na baadaye kurudi shule, iwe hivyo pia kwa yule wa kiume asitishwe masomo hadi mwenzake atakapojifungua na kama aliyempa mimba ni mwalimu au mtu mzima, sheria ifuate mkondo wake.

“Kwanini tumwadibu mtoto wa kike peke yake aliyempa ujauzito yupo wapi?” alihoji na kuongeza kuwa, hata msichana akirudi shuleni baada ya kujifungua miaka miwili aliyokaa akimlea mtoto, itamfanya awe nyuma hatua nyingi kitaaluma.

Alisema mbaya zaidi msichana ambaye wakati huo ni wazi alikuwa na wadogo zake nyumbani, hataweza kuwa na utulivu wa kufuatilia masomo kama alivyokuwa awali, jambo ambalo ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.

Pengo alisema kipindi hiki cha maadhimisho kuelekea kilele Novemba 28, mwaka huu, kuna haja ya jamii kutafakari na kuchukua hatua kukomesha mambo ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Alisema mila na desturi nyingi zinatoa kipaumbele cha elimu na mambo mengine kwa mtoto wa kiume kuliko wa kike na kwamba, ni mambo ambayo yamepitwa na wakati na hayana nafasi kwa sasa.

Awali, akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwanasheria wa WLAC, Asimwe Kabanywanyi alisema uzinduzi wa maadhimisho hayo utafanyika leo na kampeni za kupinga hali hiyo zitaendelea nchi nzima na kilele ni Novemba 28 katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Amani nyumbani, duniani, elimu sawa kwa wote’.