• Isikupite Hii

  November 18, 2015

  NEWS: BOMOABOMOA KUISAFISHA DAR.


  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi leo inaanza kubomoa nyumba zilizojengwa bila kufuata utaratibu kwenye maeneo ya wazi na hifadhi za barabara katika Manispaa ya Kinondoni kuanzia kesho.

  Hatua hiyo pia itakuwa ni utekelezaji wa kilio cha muda mrefu cha Rais John Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi cha kutaka watu wafuate sheria katika ujenzi.

  Dk Magufuli kwa muda mrefu, amekuwa akisema kama mtu amejenga kwenye hifadhi ya barabara au mahali pengine panapokiuka sheria, dawa yake ni moja tu, “kubomolewa na kudaiwa gharama za utekelezaji wa sheria hiyo.”

  Katika uongozi wake kwenye wizara hiyo bomoabomoa ilifanyika katika maeneo mengi nchini ili kupisha hifadhi ya barabara na kuwezesha ujenzi wa mtandao wa barabara nyingi zinazoonekana sasa.

  Kamishna wa Ardhi wa wizara hiyo, Dk Moses Kusirika alisema nyumba zilizojengwa katika maeneo yaliyotengwa mijini kwa matumizi ya umma, zitabomolewa ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa. Dk Kusiruka alisema maeneo yanayokusudiwa ni pamoja na yale ya wazi na njia za miundombinu na huduma za umma ambazo mara kwa mara huvamiwa na waendelezaji binafsi na kukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa.

  Alisema ubomoaji huo utahusisha nyumba zote zilizojengwa bila kibali cha ujenzi, bila kufuata michoro ya mipango miji wala kufuata matumizi ya ardhi, hasa kwa maeneo ya wazi. Kwa mujibu wa Dk Kusiruka, maeneo ambayo yatahusika na operesheni hiyo ni Mbezi, Tegeta, Bunju, Mwenge na Kinondoni Biafra.

  “Kazi ya ubomoaji inatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho (leo) na itaendeshwa na Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi ambayo itasimamia kuhakikisha sera za ardhi na taratibu za uendelezaji zinafuatwa,” alisema Dk Kusiruka.

  Kamishna huyo alisema shughuli hiyo itaendelea kwenye manispaa za Ilala na Temeke na baadaye nchi nzima. Alisema mpango huo ni utekelezaji wa tamko namba 6.6 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 linalosema kuwa “Serikali itahakikisha kwamba maeneo yote mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yalindwa ili yasivamiwe.”

  Kamishna huyo pia alinukuu tamko namba 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 linalosema, “Serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao.”                                                                                             
  Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya aliwataka wananchi wajenge kwa ajili ya maendeleo kwa kufuata sheria za ardhi zinavyoonyesha. Mkuya aliwashauri waende kwenye halmashauri ya manispaa hiyo kwa ajili ya kupewa vibali vya ujenzi na siyo kujichukulia mamlaka ya kujenga kiholela bila mpangilio.

  “Kila mwezi tunatoa vibali vya ujenzi, hivyo tunawakaribisha wananchi wote kwenye ofisi zetu wapewe vibali, waachane na ujenzi holela,” alisema Mkuya. Alisema manispaa hiyo ilishatoa taarifa kwa watu waliovamia maeneo ya umma na kujenga nyumba zao ikiwataka wahame mara moja kabla ya ubomoaji huo.

  Juzi, Halmashauri ya Temeke ilibomoa nyumba 45 kati ya 161 baada ya kutoa tangazo la kuwataka wananchi kuhama ili kupisha shughuli za maendeleo. Kurasini kweupe Siku ya pili ya utekelezaji wa bomobomoa ya nyumba kupisha uwekezaji, eneo la Kurasini wilayani Temeke, limebaki jeupe huku nyumba chache zenye kesi mahakamani zikinusurika.

  Mwenyekiti wa Mtaa Kurasini, Rajabu Nkumilwa alisema Serikali inatakiwa kuunda timu kuchunguza kama kuna ufisadi Manispaa ya Temeke katika kuliwapa wananchi fidia ya uhamisho wa makazi. “Watu zaidi 108 walipeleka malalamiko juu ya malipo yaliyotolewa, tathmini ilifanyika kwa watu 78, kati yao 34 hadi jana hawakuwa wanajua hatima yao, huku fedha zikiwa zimelipwa tofauti na tathmini ya mali zao,” alisema.

  Mwenyekiti huyo alidai kuwa kuna madai uchakachuaji kupitia vitabu vya malipo ya wananchi vilivyosainiwa na watu wawili tofauti. Nkumilwa alisema kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawana pa kuishi huku wengine wakishindwa kuhama kutokana na kutolipwa baadhi ya fedha zilizotolewa na mwekezaji kwa ajili ya usafirishaji mali.

  Source: Mwananchi.