• Isikupite Hii

  November 9, 2015

  NDOTO YA PAPA FRANCIS ILIKUWA NI KUUZA NYAMA.

  Papa Francis

  Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amesema hakufikiria kuwa kiongozi wa kanisa hilo katika maisha yake bali alikuwa na ndoto ya kuwa muuzaji maarufu wa nyama.

  Papa alisema haijawahi kutokea hata siku moja kuwafikiria kuwa kiongozi wa Kanisa hilo kwani haikuwa ndoto yake.

  “Nakumbuka karibu na nyumbani kulikuwa na soko lenye maduka ya nyama na matunda kila siku nilikuwa nikienda kununua vitu sokoni nikiwa nimeambatana na mama pamoja na bibi yangu. Aliongeza wakati huo nilikuwa nina miaka minne bado nilikuwa mdogo lakini nakumbuka kila nikifika sokoni macho yangu yalikuwa yakiwaangalia wauzaji wa nyama na namna wanavyozipima na kuwafungia wateja niliwatamani sana,’’ alisema.

  Akizungumza akiwa nchini Argentina, kwenye Jiji la Buenos Aires Papa alisema, kila siku mama na bibi yake walipomuuliza kwamba angependa kuwa nani akiwa mkubwa aliwajibu muuza nyama. Habari hizo zilitolewa katika mahojiano na gazeti la Uholanzi “Straatnieuws”, ambalo huuzwa na wasiokuwa na makao katika Jiji la Utrecht.

  Papa ambaye ni wa kwanza kutoka Latin Amerika pia alifichua kwamba anapata tabu kwa sasa hivi kwa sababu hapati nafasi ya kutembea barabarani. Alieleza kuwa akiwa Buenos Aires, kulikuwa na sehemu na alicheza kandanda ingawaje hakuweza kucheza mchezo huo.

  Papa alieleza sababu ya kukataa makazi rasmi ya Papa yenye vyumba 10 na kusema kuishi sehemu kama hiyo ni sawa na kujitenga licha ya kuwa kubwa ukilinganisha na anapokaa.

  “Kuishi eneo kama lile inamaanisha kwamba ndiyo nimejitenga na jamii. Nilifikiria sana na nikaona siwezi kuishi pale,” alisema Papa Francis. Badala yake Papa aliamua kuishi katika nyumba ya vyumba viwili katika makazi ya Domus Sanctae Marthae, ambapo anaweza kupokea wageni na kula na watu wengine katika kantini.

  Kiongozi huyo anatarajiwa kutembelea nchi za Afrika zikiwamo Jamhuri ya Afrika ya Kati licha ya kuwa na machafuko pamoja na Kenya na Uganda. Kiongozi huyo ametoa tahadhari ya mapokezi yake na kusema hataki kupokelewa kifahari kama viongozi wengine na ameahidi kula vyakula vya asili akishirikiana na wazee na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kwenye nchi hizo.