November 20, 2015

NEWS: BOMOABOMOA YAKUMBA KANISA LA ANGLIKANA DAR. (+VIDEO)

Dar es Salaam. Kanisa la Anglikana la Mtaa wa Kisanga B, Mivumoni Kinondoni, limekumbwa na operesheni ya bomoabomoa inayoendelea Dar es Salaam. Bomoabomoa hiyo iliyoanza juzi katika manispaa za Temeke na Kinondoni, inahusisha ubomoaji wa nyumba zilizojengwa maeneo ya wazi na hifadhi za barabara kinyume cha sheria.

Tangu kuanza kwa operesheni hiyo katika Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nyumba za makazi na biashara 38, gereji tatu na sehemu ya kuoshea magari vilivyokuwa vimejengwa kinyume cha sheria vimebomolewa.

Hivi karibuni, Kamishna wa wizara hiyo, Dk Moses Kusirika alitangaza kuanza kwa operesheni ya kubomoa nyumba hizo na kuwa baada ya Kinondoni, watahamia wilaya nyingine na mikoani. Katika Mtaa wa Kisanga B, Wazo – Mivumoni nyumba tatu likiwamo kanisa hilo la Anglikana, zilibomolewa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisanga B, Mivumoni ambaye pia ni muumini wa kanisa hilo, Enock Kaisi alisema hawakuwa na taarifa kuhusu operesheni hiyo na kwamba walishangazwa kuona tukio hilo. “Nimeshangaa napigiwa simu saa 1.00 asubuhi kuwa kuna tingatinga na polisi wanabomoa nyumba tatu na kanisa letu. Nilipofika eneo la tukio nikaambiwa tumelijenga kwenye eneo lisiloruhusiwa kisheria, japo kulikuwa na kibali cha kuendesha kanisa,” alisema.

Mmoja wa wakazi wa mtaa huo aliyekumbwa na mkasa huo, Rehema Sudi alilalamikia hatua hiyo akisema hakupewa taarifa. Hata hivyo, alisema eneo lake halikustahili kuguswa kwa sababu ana vielelezo vyote vinavyoonyesha yupo kihalali na hakuvamia eneo hilo kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inavyodai.

“Wamekuja saa moja asubuhi bila kunipa taarifa nikawauliza kosa langu nini mbona nina uthibitisho unaonyesha eneo hili siyo la wazi, wakanijibu nimevamia na ndani ya dakika 10 nitoe vyombo vyangu. “Binafsi ninawashangaa kwa sababu ninamiliki eneo hili kihalali tangu mwaka 2000... lakini nashangaa leo (jana ) ninaambiwa niondoke,” alisema Sudi huku akiwaonyesha wanahabari vielelezo alivyodai vinaonyesha kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Aliiomba Serikali kumpatia eneo mbadala baada ya kumvunjia kwa kuwa hana mahali pa kuishi na familia yake: “Nina familia sijui leo (jana), tutalala wapi naomba Serikali iniangalie kwa jicho la tatu.” Kutokana na mshtuko wa ubomoaji huo, wapangaji wawili mmoja akiwa mjamzito ambao hawakujulikana majina yao walizimia na kupelekwa hospitali.

Akizungumzia kanisa, Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni anayesimamia ubomoaji huo, Baraka Mkuya alisema: “Tumebomoa kanisa moja ambalo halikuwa kubwa kwa sababu lilijengwa kwenye hifadhi ya mto katika eneo la Kisanga B.” Alisema hawakuwa na sababu ya kutoa taarifa kuhusu operesheni hiyo kwa maelezo kwamba wavamizi wa maeneo hayo hawakutoa taarifa wakati wakifanya ujenzi huo kinyume cha sheria. Alisema katika eneo la Mbezi Jogoo, manispaa hiyo ilibomoa nyumba moja na sehemu ya kuoshea magari.

Basihaya – Bunju Katika eneo la Basihaya – Bunju, baadhi ya wakazi, walianza kubomoa nyumba zao baada ya kupata taarifa juu ya kuwapo kwa operesheni hiyo ili kuokoa samani za ndani, bati, madirisha, milango na mbao. Mwenyekiti wa mtaa huo, Malinusi Ndule alisema nyumba 15 zilibomolewa na wananchi wenyewe na kwamba, tingatinga lilipofika liliambulia nyumba tatu.

“Tulipata tetesi kuwa watakuja kwa hiyo wananchi wakaanza kubomoa ili kupisha eneo la barabara walilokuwa wamevamia,” alisema. Mhandisi Mkuya alisema wakazi wa eneo hilo walikuwa wamelipwa fidia mwezi mmoja uliopita na kutakiwa wahame. Baadhi ya wamiliki wa nyumba kwenye eneo hilo walisema kuwa walibambikiwa maeneo hayo na wamiliki wa zamani, baada ya kubaini kuwa eneo hilo ni barabara. Source: Mwananchi