• Isikupite Hii

  November 24, 2015

  MWANANCHI: LOWASSA AWAPA POLE YA SH 2 MILION WALIOKOLEWA MGODINI.


  Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amewatembelea watu wanne waliokuwa wamefunikwa na kifusi katika mgodi wa Nyangalata na kumpa kila mmoja pole ya Sh500,000.

  Watu hao ambao walifukiwa ndani ya mgodi huo kwa siku 41 kabla ya kuokolewa, wamelazwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama wanakopata matibabu.

  Lowassa aliyekuwa ameambatana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba, alifika katika hospitali hiyo akifuatana na umati wa watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Ukawa na alipofika hospitalini hapo aliwapa pole waathirika kila mmoja kiasi cha Sh 500,000.

  Akiwa katika wodi namba mbili ambayo watu hao wanne wamelazwa baada ya mwenzao mmoja Onyiwa Moris kufariki juzi hakuzungumza lolote zaidi ya kuwapa fedha hizo ambazo jumla yake ni Sh2 milioni.

  Mmoja wa waathirika hao Joseph Burule alisema kufika kwa Lowassa katika eneo hilo licha ya kuwafariji pia kumewaongezea huzuni ya kukumbuka kuondokewa na mwenzao aliyefariki juzi saa sita mchana hali ambayo nao imewatia hofu ya kuendelea kuishi.

  Burule alisema kitendo cha Lowassa kuwatembelea hospitalini hapo kimewapa moyo kwa kuwa tangu waokolewe na kuanza kupatiwa matibabu hakuna kiongozi mkubwa ambaye amefika kuwajulia hali pamoja na kuwapa pole zaidi ya viongozi wa wilaya na mkoa.

  “Kifo cha mwenzetu kimetupa hofu kubwa na tulipatwa na mshituko hivyo, juzi mngetuuliza kuhusiana na hilo huenda tungezimia kwani tuliishi shimoni kwa siku 41 na kuokolewa wote tukiwa hai, tukipewa chakula tulikuwa tukila kwa pamoja huku tunataniana kwamba vipi kule,” alisema Burule.

  Naye Chacha Wambura alisema hali yake hairidhishi hivyo anaiomba Serikali iangalie uwezakano wa kuwahamishia katika Hospitali ya Rufaa Bugando ili wachunguzwe zaidi.

  Mbunge Salome Makamba aliwatuliza wananchi waliokuwa wakimshangilia Lowassa kwa kumuita Rais huku akiwataka wasifanye fujo katika mazingira ya hospitalini bali wamsubiri mbunge huyo wa zamani wa Monduli atoke katika mazingira hayo ili azungumze nao.


  Hata hivyo, Lowassa hakuzungumza nao baada ya kutoka katika hospitali hiyo badala yake alianza safari ya kuelekea jijini Mwanza kuendelea na majukumu mengine ya msiba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.