Featured Posts

December 10, 2015

JENGENI UTAMADUNI WA USAFI - RAIS MAGUFULI.


Rais John Magufuli jana aliwaongoza  Watanzania kufanya usafi na kuwataka kujenga utamaduni wa kudumisha utamaduni huo mara kwa mara.

Kufanyika kwa usafi kumetokana na hatua ya Rais Magufuli ya kufuta Maadhimisho ya Sherehe za miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika na badala yake, siku hiyo itumike kufanya usafi kwa lengo la kupiga vita ugonjwa wa kipindupindu ulioikumba baadhi ya mikoa nchini.

Pia, aliagiza Sh4 bilioni zilizokuwa zigharamie maadhimisho hayo, zitumike kwenye upanuzi wa barabara ya Morroco – Mwenge iliyopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika kusisitiza agizo lake ambalo lilipata mwitikio mkubwa katika maeneo mengi nchini, Magufuli  alifanya usafi kwa muda wa dakika 50 katika eneo la Feri lililopo ufukwe wa Bahari ya Hindi jirani na Ikulu kwa kushirikiana na mkewe, Janet, wafanyakazi wa Ikulu na wavuvi.

Wavuvi hao takribani 100 ambao waliwapa wakati mgumu walinzi kutokana kutaka kumshika mkono Rais na kuimba nyimbo mbalimbali za kumsifu, kama  ‘tingatinga limeingia’, ‘Hapa Kazi Tu’, ‘mafisadi wamekwisha’, ‘Rais wa wanyonge kaingia’, waliona ajabu Rais kushiriki kufanya usafi na wananchi.

Source: Mwananchi.