December 8, 2015

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU SIKU YA UHURU.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue


Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu namna ya kuadhimisha siku ya Uhuru ya tarehe 9/12/2015 na kusema kuwa siku hiyo sio siku ya mapumziko.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari imesema kuwa kesho ni siku ya kazi kama ilivyoelekezwa na Rais Dk John Magufuli kwa mamlaka aliyonayo kisheria.

Katika Ufafanuzi huo, Balozi Sefue amesema kuwa kwa wale wafanyakazi ambao watakuwa na kazi muhimu za kufanya katika ofisi zao wanaweza kwenda kazini.

‘’endapo wafanyakazi watakuwa na kazi muhimu za kufanya katika ofisi zao wanaweza kwenda kazini kama kawaida, vinginevyo washiriki kufanya usafi katika maeneo wanayoishi au maeneo yanayozunguka sehemu zao za kazi’’ imesema taarifa ya Balozi Sefue.

Aidha Balozi Sefue amesisitiza kuwa kampeni ya usafi itafanywa nchi nzima na kuwasihi viongozi katika mamlaka za serikali za mitaa kulisimamia zoezi hilo kikamilifu.

Siku chache baada ya kuingia Ikulu, Rais Magufuli alitangaza kufuta sherehe za Uhuru za mwaka huu zinazofanyika Disemba Tisa badala yake akaagiza siku hiyo itumike kufanya usafi wa mazingira.

Source: Mwananchi