Featured Posts

January 14, 2016

Maendeleo na ukuaji wa mtoto mpaka miezi miwili '2'

two month baby
Baada ya kuzaliwa mpaka miezi 2, mtoto hupitia hatua mbalimbali za ukuaji na maendeleo. Mwili wake unakua, uzito huongezeka na kiasi cha unyonyaji wake huongezeka kadri siku zinavyoenda. Baada ya muda anaanza kutabasamu au kukutazama. Haya ni baadhi ya maendeleo ya ukuaji wa mtoto akiwa na miezi 2.

Maendeleo na ukuaji wa mtoto wa miezi 2 huwa kama ifuatavyo:
Kijamii

 •     Huanza kutabasamu anapoangalia watu au unapocheza nae. Hasa watu wa karibu anaokaa nao kila siku.
 •     Anaweza kujituliza mwenyewe kwa kuleta mkono wake mdomoni na kuunyonya.
 •     Anaweza kuanza kutazama wazazi au mlezi wake.

Kimwili

 •     Anaweza kumfuata mtu kwa kugeuza kichwa
 •     Kwa kiasi kidogo anaweza kukaza shingo, pale anapoinuliwa kwa mikono.

Kuongea na Lugha

 •     Huanza kutoa sauti ndogo ndogo kama anacheka (cooing and gurgling)
 •     Anaweza kugeuza kichwa kuelekea upande sauti inapotoka.

Kiakili

 •     Anaweza kuanza kutambua uso. Atapendelea zaidi nyuso za watu aliowazoea.
 •     Anaanza kufuata vitu kwa macho. Anaweza akapendelea kutazama upande wenye televisheni au vitu vingine.
 •     Atalia iwapo hajisikii vizuri au hafurahii kitu kinachofanyika.

Katika kipindi hiki uwezo wa mwili wa mtoto kudhibiti joto la mwili ni mdogo sana, hivyo ni muhimu mtoto afunikwe kwa nguo zinazotunza joto bila kusahau kufunika kichwa, mikono na miguu. Mtoto asipofunikwa vizuri, anaweza kupoteza joto sana na hivyo kuhatarisha maisha yake.

Tegemea mabadiliko yafuatayo kadri mtoto wako anapoendelea kukua kufikia miezi 2:

Uzito

Wiki ya kwanza baada ya kuzaliwa mtoto hupungua uzito kidogo inaweza kufika asilimia 10 ya uzito aliozaliwa nao) kutokana na kupungua maji mwili. Mpaka wiki ya pili uzito wake unarudi kawaida na hata kuzidi ule aliozaliwa nao, na kuongezeka kwa wastani wa gramu 30 kwa siku. Kwa wastani mpaka kufikisha miezi 2 atakuwa ameongezeka sio chini ya kilo 1.

Unyonyaji

Inashauriwa umnyonyeshe maziwa ya mama pekee. Mpaka umri huu mfumo wa chakula wa mtoto hauwezi kumeng’enya vizuri vyakula vingine kama uji, juisi n.k. Chakula bora na kamili ni maziwa ya mama.
Unaweza kumnyonyesha kadri mtoto atakavyotaka, lakini si chini ya mara 10 ndani ya saa 24.

Kupata Choo

Baada ya kuzaliwa atakuwa anapata choo mara kwa mara hasa baada ya kunyonya. Hakuna kiasi maalum cha kupata choo katika umri huu, ila unaweza kubadilisha nepi au pampasi mara 7 au zaidi. Mara chache bila tatizo lolote mtoto anaweza asipate choo kwa siku kadhaa. Ingawa inaweza kuwa kawaida, onana na daktari haraka pale unapoona hapati choo kwa siku 1 au zaidi. Pia iwapo utaona mabadiliko katika rangi ya choo kama kuwa cheusi au chekundu, tumbo kujaa gesi au kuvimba, analia wakati anajisaidia onana na daktari haraka.

Ulalaji

Kulala ndo kitu kikubwa atakuwa anafanya miezi yake ya mwanzoni ya maisha yake. Akishanyonya mara nyingi kitakachofuata ni kulala. Kwa sasa hatakuwa na ratiba maalum, anaweza kulala au kuamka wakatai wowote. Anaweza kukufanya ukeshe usiku mzima halafu mchana akalala safi tu.

Kinga ya Mwili

Kipindi hiki mtoto bado hajaweza kutengeneza kinga yake mwenyewe vya kutosha. Kwa kiasi hutegemea kinga kutoka kwa mama kupitia maziwa na mgusano wa mwili wake na mama. Chanjo hutolewa Ili kuhakikisha mtoto anakingwa na magonjwa hatarishi yanayoweza tishia uhai wake.


Dalili Za Hatari


Endapo mtoto wako atapata dalili zifuatazo mpeleke hospitali haraka bila kuchelewa:

 •     Anapata joto kali
 •     Anatapika kila anaponyonya
 •     Anapata degedege
 •     Anapata rangi ya manjano kwenye macho na mwilini
 •     Anashindwa kunyonya au hanyonyi vizuri
 •     Anapumua kwa shida au haraka haraka huku kifua kikibonyea ndani
 •     Anapoteza fahamu
 •     Tumbo kujaa

Ikiwa unaona mabadiliko mengine ambayo huyaelewi basi wasiliana na daktari haraka. Vingevyo nikutakie malezi mema!