January 11, 2016

ASKOFU AFUKUZWA KWA UBADHILIFU WA SH500 MILIONI.


Wachungaji wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi Askofu wa Dayosisi hiyo, Boniface Kwangu kwa madai ya kuhusika na ubadhilifu wa Sh500 milioni.

Hii si mara ya kwanza kwa wachungaji wa kanisa hilo kumkataa Askofu Kwangu, baada ya mpango kama huo kushindikana Septemba 2012 walipomtaka ajiuzulu kwa sababu mbalimbali.

Akisoma tamko la kumfukuza kazi askofu huyo jana mbele ya waumini wa kanisa hilo, Mwenyekiti wa wahudumu wa kanisa, Mchungaji Andrew Kashilimu alidai askofu huyo amekikuka viapo vyake, Katiba ya Jimbo hilo, Katiba ya DVN, utumiaji mbaya wa madaraka, mali na fedha za kanisa, kanuni na maadili ya kanisa hilo.

Mchungaji Kashilimu alidai baada ya kikao cha wachungaji kilichofanyika Septemba mwaka jana kilithibitisha kwamba askofu huyo hafuati kanuni na taratibu za kanisa Anglikana Tanzania na amekuwa akiendeleza matabaka ndani ya wahudumu na waumini na utoaji ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.

“Baada ya kuchanganua mambo yote kwa ujumla, kikao kikaridhia Askofu Boniface Kwangu ajiuzulu kwa ajili ya afya ya Kanisa la Mungu. Taarifa zilifika Jimbo Kuu Anglikana Tanzania na Jimbo kupendekeza iundwe Tume ya kushughulikia mgogoro wa DVN,” alisema Mchungaji Kashilimu na kuongeza:

“Baada ya kuundwa kwa tume hiyo, taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya shule ya Isamilo ambayo inamilikiwa na kanisa ilibainisha kwamba kulikuwa na upotevu wa zaidi ya Sh500 milioni. Katika hili Askofu Kwangu alihusika na ufisadi huo.”

Kashilimu alidai askofu huyo aligundulika kufungua akaunti binafsi katika benki ya Mkombozi anayotumia kujipatia fedha kutoka kwa wahisani kwa kutumia jina la dayosisi hiyo.

Source: Mwanachi.co.tz


By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.