• Isikupite Hii

  January 27, 2016

  AFYA:MAANA YA CHANJO NA UMUHIMU WAKE.

  Chanjo 
  CHANJO ni kitu kilichotengenezwa kitaalamu kwa mbinu za kibiolojia ili  kuupa mwili kinga dhidi ya maradhi.

  Huwa na chembe chembe zinazofanana sawa na vimelea vinavyosababisha maradhi hayo.

  Tofauti ni kuwa vinapunguzwa makali ili kutodhuru mwili. Chanjo hutengenezwa kwa vimelea hai vilivyopunguzwa makali au vikiwa vimekufa au sumu ya vimelea au moja ya vitu vilivyomo katika nyuso za vimelea.

  Chanjo hufanya kazi vipi?

  Chanjo inapoingizwa kitaalam katika mwili husababisha uchokozi katika mfumo wa kinga, hivyo kinga hutoa mjibizo kwa kutiririsha askari mwili ambao hutambua kimelea kutoka nje ya mwili, hivyo hukiangamiza na kinga ya mwili hutunza kumbukumbu.

  Mwili utakapokumbwa na kimelea hicho kwa mara nyingine mfumo wa kinga hukiangamiza kwa haraka sana na kwa urahisi zaidi.

  Ni magonjwa gani yanayopatiwa chanjo?

  Magonjwa yanayopatiwa chanjo ni kifua kikuu, ugonjwa wa kupooza mwili, kifaduro, dondakoo, pepopunda na surua.

   Pia, kwa sasa kuharisha kunakosababishwa na kirusi cha rota na homa ya mapafu (nimonia) pia kunapatiwa chanjo.

  Chanjo na utunzaji wake


  Kwa kawaida, chanjo huhitaji joto maalum ili kuweza kuhifadhi ubora wake tangu kiwandani mpaka siku ya kutolewa.

  Chini ya Wizara ya Afya ya Tanzania kupitia  EPI katika mfumo unaoitwa ‘cold chain’, kitengo hiki husimamia na kuhakikisha ubora unatunzwa mpaka siku ya kutumika kwa chanjo.

  Chanjo huhifadhiwa katika masanduku maalum ndani yake huwa na mfumo wenye jotoridi tofauti tofauti kuanzia katika sehemu ya juu kuwa na joto la juu.

  Katika kitako joto huwa jotoridi la chini, hivyo uhifadhi wa chanjo hutegemeana na chanjo yenyewe joto kiasi gani itahifadhi ubora.

  Aina za chanjo na zinavyotolewa

  Nchini Tanzania,  chanjo zinazopatikana ni Bacille callimete-Guerin (BCG),polio ya mdomoni (OPV), deptheria-pertusisi-tetanus-hepatatis (DPT-HB), surua na antitetanus toxoid kwa wajawazito.

  Pia, kuna mbili mpya zilizoanza kutumika hivi karibuni  ambazo ni za homa ya mapafu (nimonia) na kuhara kunakosababishwa na kirusi cha rota. Utoaji wa chanjo hizi nchini ulizinduliwa mwaka 2013.

  Mtoto anapozaliwa hupewa BCG na OPVo, BCG humkinga mtu asipatwe na  kifua kikuu kikali na hutolewa kwa kuchomwa chini ya ngozi, OPVo hutolewa kwa njia ya matone ya mdomoni humkinga mtu asipatwe na ugonjwa wa kupooza.

  Baada ya wiki nne tangu kuzaliwa, mtoto hupewa  DPT-HB-1 na OPV-1 hutolewa kwa pamoja kwa awamu tatu, awamu ya pili ni baada ya wiki nane na ya mwisho baada ya wiki 12.

  DPT-HB hutumika kukinga magonjwa manne ambayo ni  kifaduro, dondakoo, pepopunda na homa ya ini. Hutolewa kwa njia ya sindano katika msuli wa paja la kulia.

  Chanjo ya surua hutolewa baada ya miezi  tisa na humkinga mtoto na ugonjwa wa surua hutolewa kwa njia ya sindano ya msuli wa paja.

  Pia, zipo chanjo nyingine kama vile ya kuzuia  homa ya manjano, chanjo ya mafua makali yanayosababishwa na virusi.

  Kuna madhara yatokanayo na chanjo?

  Yapo madhara machache yanayotokana na chanjo, kama vile homa, mauimivu na uvimbe sehemu ilipopitia sindano, kichefuchefu au kutapika na mzio. Madhara haya si makubwa kuusumbua mwili.

  Ushauri

  Watalaamu wanaeleza kuwa kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni vizuri jamii ikashiriki katika kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa hospitalini na nyumbani wanapata chanjo zote kufutana na mtiririko uliowekwa na wizara.

  Pia, kinamama wajawazito wahakikishe wanapata chanjo ya pepopunda na kwa wale wote wasiopata chanjo wafike katika huduma za afya ili wapate chanjo


  By Richard Edward

  Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
  Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.