January 16, 2016

NDOA NI KATI YA MUME NA MKE - WAANGLIKANA.


Kanisa la Kianglikana duniani limesisitiza kwamba ndoa ni kati ya mwanamume na mwanamke na likasimamisha ushirika wa jimbo la Marekani lililotambua ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Jimbo hilo la Marekani, ambalo kwa Kiingereza hujiita Episcopal Church, sasa halitaruhusiwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kanisa hilo.

Viongozi wa kanisa la Kianglikana duniani, waliokutana Canterbury, wamesema kanisa hilo lilikiuka Imani inayofuata na waumini wengi wa kanisa la Kianglikana kuhusu ndoa.

Marufuku hiyo ya muda ambayo imepewa jimbo hilo a Marekani inalenga kuzuia kugawanyika kabisa kwa kanisa hilo kutokana na tofauti kuhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Ndoa hizo zimekuwa zikipingwa sana na majimbo ya kanisa hilo barani Afrika.

Uamuzi wa kusimamisha uanachama wa jimbo hilo la Marekani ulifanywa katika mkutano ambao umeeleza kuwa "mkali sana".
Askofu wa sasa wa jimbo hilo la Marekani Michael Curry amesema uamuzi huo "utasababisha uchungu mwingi". 

Mzozo kuhusu ndoa za jinsia moja ulianza kutokota baada ya kutawazwa kwa Kasisi Gene Robinson, aliyekuwa ametangaza hadharani kuwa mpenzi wa jinsia moja, kuwa askofu wa dayosisi ya New Hampshire ya jimbo hilo la Marekani mwaka 2003. 

Hatua hiyo ilizua mgawanyiko mkubwa miongoni mwa viongozi na waumini wa kanisa hilo duniani.

Source: Bbc Swahili

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.