January 25, 2016

REGINALD MENGI: WENYE ULEMAVU MTANGULIZENI MUNGU NA MTAFANIKIWA.


Dar es Salaam. Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi amewashauri watu wenye ulemavu kumtanguliza Mungu mbele kwa kila jambo wanalolifanya ili waweze kupata mafanikio.

Mengi alitoa ushauri huo jana katika hafla ya chakula aliyoiandaa maalumu kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Daimond Jubilee ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Mwaka Mpya.

Alisema wakifanya hivyo, Mungu atawabariki na kutoa mwanga bora wa mafanikio kwa kile wanachokifanya ikiwa ni sehemu kujitafutia riziki ili kujiendesha kimaisha.

“Hakuna linaloshindikana kama ukimuomba Mungu. Hivyo nawaomba ndugu mshirikisheni Mungu kwa kila jambo mnalolifanya,” alisema Mengi.

Alisema anachukizwa na kitendo cha baadhi ya watu wanaopenda kuita walemavu badala ya watu wenye ulemavu.

Mengi aliwataka watu wenye ulemavu kutoitika endapo wakiitwa ‘mlemavu’ kwani wananyanga’nywa utu wao.

“Huwa napata shida nikisikia mkiitwa hivi. Jamani watu wenye ulemavu ni binadamu kama wengine hivyo lazima tuwaheshimu,” alisema Mengi.

Aliwahimiza Watanzania kuliombea Taifa ili liwe na mshikamano sanjari na kumshukuru Rais John Magufuli kwa jitihada zake za kuwajali watu hao na kuwaweka katika nafasi mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Ummy Khamis alimshukuru mwenyekiti huyo kwa jitihada zake za kuwa karibu nao sanjari na kuwapa misaada mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Mbali na hilo, Khamis alisema bado watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa mitaji hali inayosababisha baadhi yao kuishia kuwa ombaomba mitaani.

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.