February 25, 2016

BEIJING YAIPITA NEW YORK KWA MABILIONEA.

Jiji la Beijing limelipita jiji la New York katika kuwa na idadi kubwa ya mabilionea, ripoti mpya ya shirika la Hurun kutoka Uchina inasema.

Mabilionea 100 kwa sasa wanaishi katika jiji hilo kuu la Uchina, wakilinganishwa na mabilionea 95 wanaoishi New York, ripoti hiyo inasema.

Jiji la Shanghai, kitovu cha kiuchumi nchini Uchina, limo nambari tano.

Waligundua kwamba Beijing imepata mabilionea 32 wapya tangu mwaka jana, na kuiwezesha kupita New York ambayo ilipokea mabilionea wanne wapya pekee.

Kwa ujumla, Uchina pia imeipita Marekani kwa kuwa na mabilionea wengi zaidi duniani.

Hata hivyo Wamarekani bado wanatawala katika orodha ya mabilionea 10 wakuu zaidi katika orodha hiyo ya Hurun.
Uchina ina mabilionea 568 baada ya kuongeza mabilionea 90 nayo Marekani ina mabilionea 535.

Mabilionea wa Uchina kwa pamoja wana utajiri wa $1.4 trilioni (£1.01 trilioni), ambao ni sawa na mapato ya jumla ya Australia.
Mtu tajiri zaidi Uchina bado ni Wang Jianlin, ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa $26bn (£18.8bn).

Mmarekani tajiri zaidi ni Bill Gates aliye na $80bn, akifuatwa na Warren Buffett mwenye utajiri wa $68bn.

Nambari tatu inakaliwa na tajiri wa mavazi kutoka Uhispania Amancio Ortega aliye na utajiri wa $64bn. Ripoti hiyo ya Hurun inasema kwa sasa kuna mabilionea 2,188 duniani, ambayo ni rekodi mpya.

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.