February 13, 2016

MADHARA YA KUCHAPA WATOTO

http://timheaven.blogspot.com/

Adhabu ya kuchapa watoto kwa dhumuni la kukanya na kufundisha imekuwa ni njia mojawapo ya malezi kwa familia na shuleni kwa nchi nyingi duniani ukiachia baadhi ya majimbo ya Marekani na nchi za ulaya. Wataalamu wa saikolojia wanahusisha adhabu ya kuchapa na tabia zao ukubwani ukiachia mbali uvunjaji wa haki za binadamu na watoto.

Nchi 37 duniani zimekataza kabisa watoto kuchapwa,iwe na mwalimu,mlezi hata mzazi mwenyewe na nchi 113 zinazuia adhabu ya kuchapa watoto mashuleni,lakini kwa nchi zinazobakia ikiwemo Tanzania adhabu ya kuchapa watoto kwa wazazi ,walezi na hata mashuleni ni ruksa


Kuchapa Watoto ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu na Watoto

Kutokana na sheria za haki za watoto duniani “Kuchapa mtoto ni ukatili” na zinashauri serikali duniani kuzuia aina hii ya adhabu kwa watoto.

Kutokana na haki za binadamu “Kila mtu ana haki ya kupata ulinzi juu ya mwili wake” na mtoto ni bianadamu pia. Kwa nchi nyingi kama si zote duniani, kumpiga na kumsababishia maumivu mtu mwingine ni kosa la jinai,kwanini kumsababishia mtoto maumivu iwe kwa sababu nyingine yoyote isiwe kosa? Haya ni mambo yanayotakiwa kuangaliwa na kufanyiwa mabadiliko kama tamaduni nyingine zisizotakiwa katika karne hii kama ukeketaji wa wanawake na ukatili kwa wanawake.

Madhara ya Uchapaji Watoto

Kuchapa watoto kunaathiri tabia zao ukubwani,Utafiti unaonesha kuwa adhabu ya uchapaji watoto ina madhara hasi(hasara) zaidi kuliko chanya(Faida). Watoto wanaochapwa mara nyingi wanakuwa na tabia za kuchapa wengine mbeleni katika maisha yao na inahusihwa pia na ukatili kwa wengine.

Sababu 5 za Kuacha Kuchapa Watoto


1. Zinawafundisha Watoto Wenyewe Kuwa na Tabia ya Uchapaji

Utafiti unaonesha kuwa watoto wanaochapwa utotoni wanajenga tabia ya kuwa makatili na wachapaji wakiwa wakubwa na watu wazima. Majambazi na wauwaji wengi wamegundulika kuwa walikuwa mojawapo ya watoto walionyanyaswa au kufanyiwa ukatili wakiwa wadogo. Ifahamike tabia za watoto zinajengwa kwa kiasi kikubwa kwa kuiga wazazi au wakubwa wao wanachofanya hasa wakiwa katika umri mdogo.

2. Inatia Hofu Kwa Watoto na Kuwafanya Wakose Upendo

Mtoto anapochapwa hujenga hasira,kukata tamaa na hisia za kisasi na kukosa upendo.

Watoto wengi wanapochapwa huhisi wameonewa na humchukia aliyewaadhibu hata kama ni mzazi wao. Adhabu za aina hii zikiwa zinatolewa kwa muda mrefu huweza kuwajenga watoto wasio na upendo kwa wengine na hata wao wenyewe.

Hasira za utotoni zinafukiwa ndani na zinakuja kulipuka wakiwa wakubwa,usishangae kwanini watoto wako wamekuwa na tabia za ajabu wakati uliwafundisha maadili mzuri.

Pia wanajifunza kuwa ni sawa mwenye nguvu kumuonea asiyenazo na inawajenga kuamini kuwa mwenye nguvu ni wakuogopwa na wanajifunza kukubali kuonewa na kunyanyaswa.

3. Zinakata Muunganiko wa Upendo kati ya Mzazi na Mtoto

Si asili ya binadamu au kiumbe yeyote kumpenda mtu anayemuumiza. Adhabu za kuchapa hata kama zinaonekana kufanya kazi nzuri,madhara yake ni makubwa kwa siku za mbele kwani matokeo unayoyaona yanatokana na hofu pekee na ni ya muda mfupi.

4. Inawafanya Wazazi Kutojifunza Njia Nyingine za Malezi

Wazazi ambao wamekua katika mfumo huu wa kuchapa kama njia ya malezi wanakosa nafasi ya kujifunza njia nyingine ambazo zina matokeo mazuri,sababu hii ni njia pekee ambayo imekuwa ikitumika na wanayoijua. Ni wakati sawa wazazi wakaangalia njia nyingine.

5. Inawafundisha Watoto Kukubaliana na Uonevu

Watoto wanajifunza kuwa ni sawa kwa mwenye nguvu kumuonea asiyenazo na inawajenga kuamini kuwa mwenye nguvu ni wakuogopwa na wanajifunza kukubali kuonewa na kunyanyaswa.
Utamaduni wa Kuchapa Watoto ni Budi Kukomeshwa.

http://timheaven.blogspot.com/
Kumsababishia binadamu mwingine maumivu kwa sababu yoyote ile ni ukatili na unyanyasaji ambao ni lazima tuukomeshe. Sisi wenyewe tumeathirika na unyanyasaji toka enzi za ukoloni na utumwa ambapo aina hizi za adhabu zilitumika sana,inashangaza kama na sisi bado tunatumia kwa watoto wetu wenyewe.

Hali ni mbaya sana mashuleni hasa shule za msingi ambapo watoto wanachapwa viboko kwa wingi na bila kipimo maalumu. Nguvu zinazotumika katika utoaji wa adhabu kwa watoto ni kubwa sana na inatumika kwa viumbe visivyo na msaada wowote wa kujitetea.

Watoto unafanyiwa ukatili mkubwa mashuleni na ni muhimu kila mmoja wetu achukue hatua dhidi ya ukatili huu. Ni wakati sasa wa kufanya utafiti na kutumia majibu ya tafiti juu ya malezi bora katika kuelimisha na kulea watoto wetu ambao ni taifa la kesho.


By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.