• Isikupite Hii

  February 13, 2016

  VALENTINE 2016: JUA YAFUATAYO KABLA YA KESHO  Siku ya Valentine. Ni siku maalum ya kuoneshana upendo. Iwe ni mama kwa mtoto, mtoto kwa mama, ndugu jamaa na marafiki. Kuonesha unamjali. Unamthamini.
  Haimaanishi kwamba siku nyingine huwa hatuoneshani upendo lakini siku hiyo moja imetengwa maalum. Kama vile zilivyo sikukuu nyingine za Krismasi na nyinginezo, siku hiyo huwa kuna vitu vinafanyika ili tu kuonesha utofauti.


  Utakuta watu siku hiyo wanapendeza, wanatembea sehemu mbalimbali za starehe pamoja. Si kwamba siku nyingine hawawezi kufanya starehe, siku hiyo inakuwa spesho tu kwa watu wote kuweza kuisherehekea pamoja na kuleta dhana nzima ya sikukuu.

  Lakini katika ulimwengu wa wapendanao, kuna maana zaidi kama mtaifanya siku hiyo kuwa muhimu kwa ajili ya kujadili mustakabali mzima wa penzi lenu. Nimekuwa nikipokea meseji nyingi kutoka kwa wasomaji mbalimbali, wakilalama kutojua hatima ya penzi lao.

  Kuna ambao husema wanaishi bila kujua kesho yao ikoje. Wanaishi katika penzi bubu. Kwamba yeye mpenzi wake anamuita pale tu anapomhitaji faragha na baada ya hapo, mawasiliano hakuna. Anampotezea hadi siku ambayo atamhitaji tena faragha.

  Wapo ambao wanaishi kwenye manyanyaso yasiyokuwa na mwisho. Wengine wanakutana na vizingiti vya wazazi katika kufanikisha azma yao ya kufunga ndoa. Kila wakiamua kulifikisha suala la uchumba kwa wazazi, baadhi ya wazazi wanapinga uhusiano wao.

  Wengine wanasumbuliwa na suala la kutofautiana dini. Kila upande una msimamo wake kuhusu suala la imani. Wameshalijadili mara kadhaa na kuona linawasumbua hivyo kuliweka kiporo. Wanaona bora kuachana nalo ili wao waendelee ‘kuinjoi’ maisha ya uhusiano wao.
   
  Wapo wanaoteseka kwamba wenzi wao hawarejeshi upendo kama wanaoutoa wao. Utasikia mtu anakuambia, mpenzi wake hamjali. Hana muda wa kuzungumza naye. Hamuulizi ameamkaje wala ameshindaje kwa zaidi hata ya siku tatu.

  Kila siku yeye ni mtu wa kuumia moyoni kwani kila siku ndiye ambaye ana jukumu la kumuuliza mpenzi wake, vipi umeamkaje? Vipi umeshindaje na mambo mengine mengi yanayoashiria kujali na kuthamini. Asipofanya yeye mwenzake hana habari, kisingizio kikubwa huwa ni ubize wa kazi.
   
  Mpenzi wake akitaka kujua kwa nini hamjali, jibu ni moja tu; ‘nipo bize bwana.’ Marafiki zangu, siku kama ya kesho ni vyema, mkatenga muda mzuri, mkakaa pamoja katika eneo tulivu. Si lazima muende katika sehemu ya gharama sana, hapana.

  Mnaweza kukaa sehemu ambayo si ya gharama. Mkala na kunywa vinywaji ambavyo mna uwezo navyo. Kukiwa na utulivu, anzeni sasa kuzungumzia mustakabali wa penzi lenu. Mfanye tathmini. Mjue mmetoka wapi na wapi mnakotaka kuelekea.

  Kama umeona unaishi katika uhusiano ambao hauna mbele wala nyuma, utumie muda huo kumueleza mwenzako ukweli kwa lugha rafiki.Akueleze ukweli msimamo wake kwako na uone kama kweli ana dhamira ya dhati ya kuwa na wewe au anakupotezea muda wako. Hakuna sababu ya kufichana.

  Kama unaona mwenzako hana muelekeo mzuri na wewe na ukamueleza ukaona bado hana dalili za kubadilika ni vyema ukaanza kumuepuka na subiri utampata mwingine atakayekuthamini.


  By Richard Edward

  Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
  Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.