March 26, 2016

Ijue kwa ufupi historia ya pasaka ya kiyahudi.

pasaka ya kiyahudi
Jina la Pasaka limetokana na neno la Kiebrania "פסח" (tamka: pasakh) lenye maana ya "kupita juu, kukaa juu ya (kama mlinzi)" katika kitabu cha Biblia cha Kutoka 12:23.

Humo imeandikwa ya kwamba Mungu "atapita" juu ya milango ya nyumba za Wanaisraeli huko Misri katika usiku kabla ya kutoka kwao, na kuzuia maovu ambayo Wamisri waliathiriwa nayo.

Tarehe ya Pasaka ya Kiyahudi

Pasaka ina tarehe kamili katika kalenda ya Kiyahudi inaanza Nisan 15. Husheherekewa kwa siku saba yaani hadi Nisan 22. Siku ya kwanza na ya mwisho ni sikukuu hasa. 


Katika nchi ya Israel siku hizi mbili ni siku za kupumzika kazi. Wayahudi wengine, hasa nje ya Israel, husheherekea siku 8.

Kwa sababu kalenda ya Kiyahudi ni kalenda ya mwezi tarehe zake hubadilika katika hesabu ya kalenda ya Gregori yaani kalenda ya kawaida ya kimataifa. 


Kwa jumla Pasaka ya Kiyahudi inasheherekewa wakati wa miezi Machi au Aprili kwa sababu Nisan ni mwezi wa kwanza wa majira ya kuchipua.

Asili ya Pasaka

Katika Biblia, kitabu cha Kutoka, sura ya 12, kuna taarifa juu ya kutoka kwa Wayahudi katika Misri wakati wa Musa mnamo mwaka 1200 KK.

Taarifa ni kwamba Musa alitumwa na Mungu kuwaondoa Wanaisraeli katika hali ya utumwa huko Misri na kuwaongoza kwenda nchi ya ahadi. 


Lakini mfalme wa Misri mwenye cheo cha Farao alikataa, hivyo Mungu alituma mapigo dhidi ya Misri ili Farao alazimishwe kukubali.

Pigo la mwisho tena kali mno lilikuwa kifo cha kila aliyezaliwa kama mtoto wa kiume wa kwanza katika Misri. Hapo Wanaisraeli waliambiwa kuchinja mwanakondoo na kupaka damu yake milangoni kwao ili malaika akipita kuua watoto wa kwanza asiguse watoto wa Wanaisraeli.

Baada ya pigo hilo Farao alikubali Wanaisraeli watoke.

Tendo hilo la kuwaweka mababu yao huru linakumbukwa na Wayahudi kote duniani katika siku zinazoanza Nisan 15.
Sherehe ya Pasaka

Sherehe ya Pasaka inaanza masaa ya jioni kabla ya siku yenyewe, kwa sababu katika kalenda ya Kiyahudi mwanzo wa siku si usiku kati wala macheo bali wakati wa machweo jioni inayotangulia.

Maandalizi ya sikukuu ni pamoja na kufanya usafi mkubwa kabisa katika nyumba. Hakuna kitu kilichochachuka kinachobaki katika nyumba kufuatana na Kutoka 12:20, yaani kitu chochote chenye nafaka au unga wake ulioguswa na maji, hata punje yake kama vile mkate, keki au spagetti. 


Tendo hili ni la kukumbuka jinsi Wanaisraeli walipaswa kukimbia Misri haraka bila muda wa kutengeneza mikate ya kawaida yaliyochachuka. Kwa hiyo wanawake wao walioka mikate yasiyochachuka ambayo yamekuwa chakula cha Pasaka hadi leo. Mikate hii huitwa "matze".

Familia na marafiki hukutana kwa chakula cha pekee wakizunguka meza ya Seder (seder = "utaratibu") yenye vyakula vya pekee.

Kati ya vyakula hivyo, mboga chungu inakumbusha uchungu wa utumwa, matunda ya kupondwa yenye rangi ya kahawia-nyekundu yanakumbusha udongo wa matofali ambayo Wanaisraeli walipaswa kutengeneza, maji ya chumvi yanakumbusha machozi huko Misri, mayai ni ishara ya matumaini, na vingine.

Vyote huliwa katika utaratibu (=seder) maalumu pamoja na masomo na sala kutoka vitabu vya Haggada vinavyoshikwa na wote mezani. 
 


By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.