Featured Posts

May 25, 2016

EPUKA UVIVU KWA KUFANYA HAYA

EPUKA UVIVU KWA KUFANYA HAYA
Pengine wewe ni mmoja wa wale wenye kupenda kweli kweli kupiga hatua. Hauridhiki na hali uliyo nayo na unahitaji zaidi, hata hivyo ni kama umekata tamaa hujui uanzie wapi kwani unajiona wazi bado upo nyuma sana vitu vingi. Yaani kama unahitaji kupiga hatua basi itakuchukua muda mrefu sana, na pengine kwa ugumu huo na ukubwa wa kazi ya ziada unayotakiwa kufanya unajihisi kuishiwa nguvu.

Soma: Epuka Chuki Kwa Kufanya Haya.

Nataka nikupe moyo, sio wewe peke yako wengi tumepitia huko. Hata hivyo njia rahisi ya kuondokana na hizo hisia ni kufikiria kinyume cha hizo hisia. Inawezekana kushinda hizo hisia na ukajikuta unasonga mbele na mambo yako. Jinsi ya kushinda ni kama ifuatavyo:

1. Usijilinganishe na watu wengine ambao tayari wanaweza. 

Ni kweli kuwa muhimu kuangalia wengine waliopiga hatua zaidi yako ili kujifunza mbinu walizotumia, makosa yao na labda mambo gani wewe unaweza kuiga, hata hivyo kosa unalofanya ni kuwaangalia hao watu kwa upande mmoja tuu wa mafanikio yao na kuona "wanakutisha". Kumbuka hata wao nao walikua na muda ambapo walikuwa kama wewe , yaani wanaanza. Badala ya wewe kuwaogopa na kutishwa na mafanikio yao , usitupie macho kwa mafanikio yao kwa tamaa , bali kama shule kwako na uthibitisho kuwa hata wewe ukiweka juhudi na ukashinda hali uliyo nayo sasa, utafika mbali.

2. Kumbuka ulipoanza kusoma A, E mpaka Z? Kumbuka enzi hizo hata kujumlisha hujui? Basi maisha ndio hivyo, kuwa mambo makubwa huhitaji kujengwa kidogo kidogo. Na hakuna namna ya kufika kwenye ukubwa bila kupitia udogo. Hivyo anza kidogo kidogo. Ni kweli hautoona mafanikio mara moja, ila jua kuwa baada ya muda hivyo vidogo vidogo unavyovifanya vitajenga kitu kikubwa. Na hapo ndipo utakapofikia mbali huko unakotamani kufika.

3. Jiwekee utaratibu wa kuchambua malengo yako yaani katika kila lengo lako kuu mfano Kuwa mfanyabiashara, uwe na malengo madogo madogo yanayokuja kujenga hilo wazo kuu.Kwa kadri unavyotimiza vijimalengo vidogo vidogo , ndivyo unavyokaribia lengo lako kubwa.

Soma: Wivu Adui Kazini.

4. Jiwekee taratibu ya kupima mafanikio yako madogo madogo na kujipongeza. Usisubiri mpaka lile lengo kuu lifikiwe. Unajua kuwa jambo kubwa kubwa huundwa na mambo madogo madogo unayoyafanya na kufanikiwa. Jipe moyo , unaweza, na utaweza.
 


By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.