June 10, 2016

IFAHAMU HISTORIA YA MJI MTAKATIFU NA MPANGO WA MUNGU KWA MWANADAMU TANGU ASILI

IFAHAMU HISTORIA YA MJI MTAKATIFU NA MPANGO WA MUNGU KWA MWANADAMU TANGU ASILI
Tangu Ibrahimu hadi kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kuna kipindi kinachokadiriwa kufikia miaka 2000, ambacho kinajumuisha historia ya Wayahudi. Kipindi hiki cha miaka 2000 kimegawanyika katika nyakati tofauti kama ifuatavyo:

2100 BC(takribani miaka 4100 iliyopita) Mwanzo 17:4-5

Mungu anamuahidi Ibrahimu uzao mwingi
Ibrahimu aliishi kwenye kipindi cha takribani mwaka 2100 BC-Kabla ya Kristo, katika nchi ya Uru wa Wakaldayo.Leo hii nchi ya "Uru wa Wakaldayo " inaitwa nchi ya IRAQ. Mungu akamwambia Ibrahimu atoke kwa jamaa zake (yaani atoke Iraq kwa lugha ya sasa) aende Kanaani, ambayo baadaye ndiyo ikawa nchi ya Israel. Tofauti na watu wengi wa kipindi chake, Ibrahimu alimwamini Mungu mmoja wa kweli. Mungu akamhesabia haki Ibrahimu kwa imani, akamfanya kuwa baba wa taifa kubwa Israel.

2000 BC (takribani miaka 4000 iliyopita) Mwanzo 25:24

Kuzaliwa kwa Yakobo
Yakobo mtoto wa Isaka mwana wa Ibrahimu alizaliwa katika nchi ya Kaanani. Yakobo jina lake lilibadilishwa na kuwa Israel. Alikuwa na watoto 12 ambao kwao ndiyo hayo makabila 12 ya Israel yanaitwa

1910 BC (zaidi ya miaka 3910 iliyopita) Mwanzo 37:28

Yusufu akauzwa na ndugu zake kwa wa Misri
Kaka zake Yusufu walikuwa na wivu kwa mdogo wao Yusufu, wakamuuza kwa wa Misri. Baada ya kuuzwa Misri Yusufu alikuja kuwa mtu mkubwa na akawa msaidizi wa Farao. Baba yake na kaka zake Yusufu wakatoka Kaanani kuja Misri kutafuta chakula kutokana na baa la njaa katika nchi ya Kaanani.

1446BC (zaidi ya miaka 3446 iliyopita) Kutoka 13:1-22.

Kutoka Misri kwa wana wa Israel kunaanza
Baada ya kutumikishwa kwa miaka 400, Wayahudi, wakiongozwa na Musa, waliondoka Misri kuelekea nchi ya Kaanani, ambayo baadaye ikawa nchi ya Israel. Nchi ya Kaanani ndiyo nchi waliyokuwa wakiishi mwanzo kabla njaa haijatokea na wao kwenda Misri. Kwa hiyo hapa wakaanza kurudi kwenye nchi waliyoondoka kwa miaka 400 nyuma kama familia. Musa na Wayahudi wenzake walitangatanga jangwani kwa kipindi cha miaka 40 kabla ya kufika katika mipaka ya nchi ya Kaanani.

1406 BC(zaidi ya miaka 3406 iliyopita) Yoshua 1:1-9

Israel ikaanza kujitanabaisha yenyewe kama nchi
Baada ya Musa kufa, Yoshua aliwaongoza Wayahudi kuelekea Kaanani na kuanza kuishinda nchi, wakaanzisha taifa la Kiyahudi la Israel kwa mara ya kwanza katika historia.

1400BC (zaidi ya miaka 3400 iliyopita) Waamuzi 2:16-18

Katika kipindi hiki Israel ikawa inatawaliwa/kuongozwa na Waamuzi, na sio Wafalme.
Kutoka mwaka 1400 BC hadi takribani mwaka 1050 BC, Israel haikuwa inatawaliwa na Mfalme. Watu wa Israel walimfikiria na kumtazama Mungu kama mfalme wao. Kwa hiyo badala ya mfalme wa dunia, Israel ikawa inaongozwa na Waamuzi, huku Mungu wa baba zao akiwa ndiye mfalme wao.

1050 BC (Zaidi ya Miaka 3050 iliyopita) 1 Samweli 11:15, 1 Samweli 15:11

Sauli akawa mfalme wa kwanza wa Israel
Baada ya takribani kipindi cha miaka 350 cha kutawaliwa na kuongozwa na Waamuzi, watu wa Israel wakadai kuwa na mfalme kama nchi zilizowazunguka zilivyokuwa na wafalme wao. Kwa kutaka kwao mfalme, watu wa Israel wakaanza kukengeuka na kwenda mbali na kuacha imani waliyokuwa nayo kwa Mungu kama mfalme wao. Sauli akawa mfalme wa Israel na akatawala kwa kipindi cha takribani miaka 40.

1010 BC (Miaka 3010 iliyopita) 1 Nyakati 10:14.

Daudi akawa mfalme wa Israel
Daudi akawa mfalme wa Isarel mnamo mwaka 1010 BC na akatawala kwa miaka 40. Tofauti na Sauli, mfalme wa kwanza wa Israel aliyemtangulia, Daudi alishika na kufuata amri za Mungu. Alifanya makosa, lakini aliyatubia makosa yake. Mfalme Daudi Alitafuta kumpendeza Mungu daima. Alitanua wigo wa Israel na akatawala mipaka ya jirani

970 BC (Miaka zaidi ya 2970 iliyopita) 1Wafalme 1:34-37, 1Wafalme 6:1-10:

Sulemani akawa mfalme wa Israel, akajenga Hekalu la BWANA.
Sulemani, mwana wa Daudi, akawa mfalme kati ya mwaka 970 BC. Yeye pia alitawala kwa miaka 40. Sulemani akajenga Hekalu kwa heshima ya BWANA, Mungu wa Israel. Sulemani alibadilika, akageuka akamwacha Mungu na kuanza kuabudu miungu mingine.

926 BC (Miaka zaidi ya 2926 iliyopita) 1Wafalme 11:31-36:

Katika kipindi hiki, Israel ikawa ufalme uliogawanyika (Divided Kingdom)
Muda mfupi baada ya utawala wa mfalme Sulemani, Israel iligawanyika. Kukawa na Ufalme wa Kusini ambao uliitwa Yuda,ufalme huu ulijumuisha mji wa Yerusalemu na hekalu. Na pia kukawa na ufalme wa Kaskazini ambao uliendelea kuitwa Israel.

721 BC (Miaka zaidi ya 2721 iliyopita) 2Wafalme 18:13:

Katika kipindi hiki, Waashuru waliushinda ufalme wa kaskazini wa Israel.
Utawala wa Ashuru waliushinda ufalme wa kaskazini wa Israel kati ya mwaka 721 BC. Waashuru waliwatesa wengi. Waliwalazimisha Wayahudi wengi (kabila 10 kati ya kabila zote 12 za Israel) kutoka nje ya Israel na Waashuru wakaleta wageni ndani ya Israel.

621 BC (Miaka zaidi ya 2621 iliyopita) Sefania 2:13

Babeli ikaushinda Ninawi(Utawala wa Ashuru):
Mji Mkuu wa Utawala wa Ashuru , Ninawi-ulishambuliwa kwa ushirikiano wa Wababeli, Waamedi na Wageni wa nchi.Kama ilivyoelezwa na nabii Nahumu katika Biblia, Ninawi ulikuwa uharibiwe kwasababu ya matendo maovu ambayo utawala wa Ashuru waliwatenda Wayahudi na watu wengine.

605 BC (Zaidi ya miaka 2605 iliyopita) Yeremia 27:20

Babeli yaonyesha shinikizo lake kwa Yuda:
Utawala wa Babeli chini ya utawala wa mfalme Nebukadneza, ulifanya jitihada kutaka kuongeza himaya yake na kuanza kuulazimisha Yuda uwe chini yake. Nebukadneza aliwachukua Wayahudi wengi kama mateka na kuwapeleka Babeli ili kuhakikisha anaitiisha Yuda yote.

597 BC (Zaidi ya miaka 2597 iliyopita) 2Nyakati 36:20

Babeli yaishambulia Yuda:
Majeshi ya Wababeli yaliishambulia Yuda na kuchukua mateka zaidi wa Kiyahudi kwenda Babeli. Ezekieli, mmoja kati ya mateka, akawa nabii wa Mungu akiwa huko Babeli uhamishoni. Ezekieli alifafanua kwamba Mungu anaruhusu Babeli kuiadhibu Yuda kwa sababu watu wa Yuda wamekuwa si waaminifu kwa Mungu.

Itaendelea....

Mungu akubariki, kwa jina la Yesu Kristo.


By Richard Edward

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.