Featured Posts

July 12, 2016

ASKOFU GWAJIMA AKAMATWA NA JESHI LA POLISI BAADA YA KUTUA UWANJA WA NDEGE.

Hatimaye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye amekuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa alikamatwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.

Baada ya Askofu Gwajima kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.

Akizungumzia kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno alisema askofu huyo aliwasili saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Soma: Polisi Wamuwinda Askofu Gwajima Kwa Masaa 7 Bila Mafanikio, Sababu Iko Hapa.

Otieno alisema mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

"Ni kweli tulimkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji alidai kuwa alikuwa nchini Japan," alisema Otieno. 

Mwanasheria wake Peter Kibatala alisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi saa 4.45 asubuhi kwa mahojiano mafupi na aliruhusiwa kuondoka baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.

"Askofu Gwajima amehojiwa leo (jana) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri chochote kitakachoendelea," alisema Kibatala bila kueleza mahojiano yalivyokuwa.

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.