August 1, 2016

KANISA LA T.A.G LAIPONGEZA SMZ KWA KUDUMISHA AMANI.

KANISA la Tanzania Assembles of God limeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kudumisha amani katika kipindi chote kabla na baada ya uchaguzi mkuu, hatua ambayo imejenga imani kubwa kwa viongozi waliopo madarakani.

Hayo yalisemwa na Askofu wa Kanisa hilo, Dk Barnabas Mtoka wakati akihubiri katika ibada maalumu ya kuiombea Zanzibar na wananchi kuwa salama zaidi kwa kuepuka vurugu za kisiasa.

Alisema kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu wakati wote ni nafasi nzuri kwa wananchi kufanya kazi zao ikiwemo za kujiletea maendeleo.

"Kanisa la Assembles of God limefurahishwa na juhudi zilizooneshwa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kudumisha amani, utulivu katika kipindi chote wakati wa harakati za kampeni hadi kuelekea katika uchaguzi," alisema.

Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto, Moudin Castico alisema Tanzania ndiyo kimbilio la amani kwa nchi nyingi katika bara la Afrika zikiwemo za kusini mwa jangwa la Sahara.

Alisema suala la kuimarishwa amani kamwe halitofanyiwa mzaha kwa kutoa nafasi kwa watu wachache kuhubiri chuki na kusababisha uhasama kwa wananchi.

Castico alisema wapo baadhi ya watu nia yao kuona kwamba wananchi wa Zanzibar wanasambaratika kwa ajili ya kukidhi malengo na matarajio ya kisiasa ya kulazimisha kuwepo madarakani.

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 

Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.