September 25, 2016

Hasara za kulipiza kisasi - Mwalimu Christopher Mwakasege. (2)

Hasara ya Tatu "UNAMZUIA MUNGU KUKUPIGANIA"
Unaweza ukashangaa, lakini ndivyo ilivyo! Ukiamua kulipa kisasi juu ya tatizo ulilonalo unamzuia Mungu asikusaidie kulitatua.Mungu hawezi kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana".

Neno "ipisheni" limeandikwa kwa sababu kulipa kisasi "kunazuia" ghadhabu ya Mungu isipigane upande wako! Tena si hivyo tu lakini ukilipa kisasi unaingilia kazi ambayo si yako! Ni kazi ya Mungu maana anasema "Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana" Ikiwa kisasi ni juu ya Mungu kulipa, basi huhitaji wewe kulipa. Je, tunakwenda pamoja katika hili?


Hatua yako ya kulipa kisasi inazuia mkono wa Mungu kukupigania kwa hiyo ipishe ghadhabu ya Mungu kwa kutokujilipizia kisasi!

Hasara na Nne "UNAJICHUMIA DHAMBI!"
Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo mabaya uliyofanyiwa. Huwezi kulipa kisasi bila ya kumchukia huyo unayejilipizia kisasi kwake. Na Biblia inasema hivi:

"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).

Umeona hilo! Chuki huzaa kisasi, na huzaa dhambi ya kuua! Na

Isaya 59:2b inasema; "dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia".


Kwa hiyo kama umekwisha lipa kisasi au umekusudia moyoni mwako kulipa kisasi ni muhimu utubu ili Mungu akusamehe na mawasiliano yako na Yeye yawe mazuri.

HATUA TANO MUHIMU KATIKA KUSAMEHE
Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:

"Hapa mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. ...... Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa,si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu" (Yohana 1:1, 14, 12, 13).

Yesu Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha mapya.Imeandikwa kwamba, "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya" (2Wakorintho 5:17)

Utu mpya unazaliwa ndani yako, maisha, mawazo, matendo, maneno, yanatakiwa kubadilika Yesu Kristo aingiapo ndani yako. Pia, kusamehe kwako kunabadilika kunakuwa kupya. Lakini utaona kwamba watu wengi waliozaliwa mara ya pili, na kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao, bado wanaendelea kusamehe kama zamani.

Biblia inasema "ya kale yamepita, tazama!yamekuwa mapya"(2Wakorintho 5:17).

Kwa maneno mengine ni kwamba kusamehe kwako ulivyokuwa unafanya zamani, hakuhitajiki tena, tazama! Kusamehe sasa ni kupya. Tabia ni mpya.Zamani ulisamehe lakini bado ulikumbuka makosa uliyofanyiwa. Tena ulisamehe si kwa ajili yako bali kwa ajili yake aliyekukosea na wakati mwingine ulitaka uthibitisho kwanza kuwa kosa hilo halitarudiwa na ndipo usamehe. Ni lugha ya kawaida kusikia mtu akisema 'nasamehe lakini sitasahau'.

Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe, ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Kwa kuwa imeandikwa hivi:

"Yeye asemaye yakuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda" (1Yohana 2:6)

Wewe unayesema kwamba una Kristo ndani yako, basi inakupasa kuenenda kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani katika mwili.Kwa kuwa Kristo alisamehe na kusahau, basi na wewe inakubidi kusamehe na kusahau.


Hatua tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo na amani na jirani zako na ndugu zako. Na pia, zitafungua milango mipya ya uhusiano wako na Mungu utakaoinua huduma yako katika kumtumikia Mungu. Na zaidi ya yote zitakuweka huru na magonjwa mengi yanayokusumbua.