September 25, 2016

Hasara za kulipiza kisasi - Mwalimu Christopher Mwakasege. (3)

1. Fahamu kuwa si wewe bali Kristo.
"Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20)

"basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3)

Mistari hii michache ni baadhi tu ya ile inayotufunulia mambo yaliyofanyika ndani yetu tulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wetu.Si wewe unayeishi, bali ni Kristo aliye ndani yako. Na uhai ulio nao sasa, baada ya kuzaliwa mara ya pili, unao katika imani ya Mwana wa Mungu.Soma tena mstari huu:-

"..... Kwa maana mlikufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu."

"Kwa maana mlikufa." Utu wako wa kale, na mtu wa kale ndani yako alikufa siku ulipompokea Kristo maishani mwako. Kilichofuata ni uzima wa Kristo, katika utu mpya ukidhihirishwa katika maisha yako.Sasa unaweza kuelewa kwa nini Yesu Kristo alisema awachukiae ninyi, amenichukia mimi. ( Yohana 15 :18)

Mtu akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.Mtu akikutukana, akikusemea mabaya, akikupiga, fahamu kuwa si wewe anayekufanyia hayo, bali Kristo aliye ndani yako!Kuthibitisha haya Biblia inasema:

"Vita hivyo si vyako ni vya Bwana" (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na wazo hilo katika roho yako, chukua hatua ya pili ifuatayo:

2. Mpende adui yako Umuombee
"Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ...." (Mathayo 5:43, 44)

Jambo ambalo liko wazi ni kwamba hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo, "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanae ..." (Yohana 3:16)

Kilichomfanya Baba Mungu kumtuma Yesu Kristo duniani ni Upendo. Alitupenda sisi mno, alitupenda upeo wakati bado tulipokuwa tungali wenye dhambi. Na kuudhihirisha upendo huo, Yesu Kristo alizaliwa duniani na kufa masalabani ili sisi tupone.

Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na upendo, kusameheana hakupo. Palipo na upendo wa kinafiki, pia pana kusameheana kinafiki. Kusameheana hakuonekani siku hizi, katika ndoa, kati ya ndugu, kati ya majirani, kati ya watu wa Mungu, KWA SABABU UPENDO WA WENGI UMEKWISHA POA!

Watu siku hizi wanafanya kile ambacho Yesu Kristo aliwaambia wasifanye. Yesu alisema, " Wapendeni adui zenu." Lakini, unaona katika watu wa Mungu, chuki imejaa, ndoa zinaharibika kwa sababu ya chuki, undugu unakufa kwa sababu ya chuki. Na ni hao wanaosema kuwa wameokoka na Yesu Kristo yumo ndani yao. Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.

Yesu Kristo anakuambia watu wa dunia wanawapenda wanaowapenda na kuwachukia wanaowachukia, lakini wewe si wa dunia hii, wapende hata wale wanaokuchukia na ili kuonyesha kuwa unawapenda kweli, uwaombee! Kwa nini Yesu Kristo, alisema "Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi?"

"Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je? Nao hawafanyi kama hayo?" (Mathayo 5:45- 47).

Ulipompokea Kristo, ulipokea upendo mpya ndani yako, unaokuwezesha kufanya mambo ambayo mtu wa kale aliyekuwa ndani yako asingeweza kufanya. Mtu mpya ndani yako ana upendo mpya. Upendo huu mpya, una tabia mpya, na mambo mapya.

"Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu; upendo hautakabari; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli huvumilia yote; huamini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote"(1Wakorintho 13:4 - 8).

Upendo huu umo ndani yako, na ndio unaokufanya uwe kiumbe kipya. Ni upendo ulio hai (Warumi 5:5) Ni upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi. Kwa upendo huu, Bwana Yesu anataka uwapende adui zako, na kuwaombea pia ili wasamehewe na Mungu juu ya makosa waliyoyafanya.

Kwa upendo huu fanya yale ambayo ulikuwa huyafanyi zamani. Kama ulikuwa husalimiani na adui yako, chukua hatua ya upendo, msalimie na ikibidi mtembelee nyumbani mwake. Kula pamoja naye, furahi pamoja naye, na omba pamoja naye.

Kuna watu wengine hawasalimiani wala kutembeleana na wazazi wao, au baba au mama, kwa sababu ya mambo yaliyofanyika zamani ambayo hawakuyapenda. Sasa, chukua hatua waandikie barua, na uwatembelee kwa maana upendo wa Kristo umekuweka huru, na chuki na kinyongo.

Kumbuka unayafanya hayo kwa ajili yako mwenyewe ili maombi yako yakubaliwe mbele za Mungu. Nafahamu kwa jinsi ya mwili, na kwa kutumia akili ya kibinadamu hatua hizo ni ngumu kuchukua. Ni kweli, lakini kumbuka si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako. Na unayaweza yote (pamoja na kuwapenda adui zako) katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)

Upendo unavunja nguvu za uadui. Usimuone jirani au ndugu ni adui tena. Kama vile wewe ulivyo kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa jicho la upya huo waone adui zako kuwa ni rafiki. Anza uhusiano mpya nao. "Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi" (Luka 6:27,28)

3. Samehe na Kusahau:
Wakati fulani nilikuwa mahali nikifanya semina ya neno la Mungu. Mtu mmoja akanifuata na akaniambia anataka nimuombee. Nikamuuliza; "Nikuombee nini?"
Akasema; "Mimi shida yangu ni kwamba naona imani yangu ni ndogo na haikui, na maombi yangu hayajibiwi. Kwa hiyo naona nina shida katika maisha yangu ya kiroho, uniombee". Inawezekana hata wewe una shida ya namna hiyo, kwa hiyo tafakari kwa makini maneno haya. Niliahidi kumuombea baadaye kwa maana muda ulikuwa umekwisha. Siku moja nilipokuwa ninaomba kwa Mungu juu ya shida yake, Bwana akanijibu katika roho yangu kuwa:

"Mtu huyo ana matatizo ya ndoa na kuna jambo lililomuudhi. Yeye anafikiri amesamehe, lakini bado ana uchungu moyoni mwake. Mwambie asamehe na kusahau na shida yake itakwisha". Nilipowasiliana naye juu ya jambo hili, alikubali kuwa, ni kweli mwenzie amekuwa akimkosea mara kwa mara katika ndoa yao. Lakini alisema amekwisha msamehe.

Nikamuuliza; "Je! mbona basi kila mkikosana unakumbusha makosa ya nyuma?Akajibu; "Ni kweli, sasa nifanyeje wakati naona kila wakati makosa aliyonifanyia nyuma yakinijia kichwani?Hili ni tatizo la wengi. Na hujikuta wanasema wamesamehe kumbe bado. Msamaha si jambo la akili ni hatua ya rohoni. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo wako.

"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii hata mara saba, bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21, 22)

"Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana tuongezee imani" (Luka 17:4,5).

Mistari hii inatuonyesha jinsi kukua kwa imani, kunavyohusiana sana na kusamehe. Wanafunzi walimwambia Bwana Yesu, awaongezee imani. Kwa kuwa walifahamu kwamba, kwa uwezo wao wasingeweza kusamehe kama Kristo anavyotaka. Ni kweli kabisa. Kama vile unavyohitaji imani katika kuomba, vile vile katika kusamehe na kusahau unahitaji imani. Ulipompokea Kristo ulipokea kiasi cha imani (Warumi 12:3)

Na ili iongezeke unahitaji kusoma neno la Mungu na kulitenda. Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. (Warumi 10:17). Imani ni ya rohoni na kusamehe ni kwa rohoni. Unawezaje kusamehe na usiyakumbuke uliyofanyiwa? Hilo ndilo tatizo kubwa alilokuwa nalo yule mtu aliyeniambia niomuombee. Na wengi pia wana tatizo la namna hii, na limekwamisha uponyaji na majibu mengine ya maombi yao, wameombewa mara nyingi, lakini bila mafanikio.

Kusamehe na kusahau ni kitendo cha imani ambacho ni budi kionekane kwa njia ya matendo ya mtu. Kusamehe ni uamuzi wa mara moja na kusahau ni vita vya imani. Sasa, utaniuliza, Ndugu Mwakasege, utawezaje namna hiyo? Kabla sijakujibu, na mimi nakuuliza swali. Siku ulipotubu dhambi zako, ulikuwa na uhakika gani ya kuwa Mungu amekusamehe wala hazikumbuki dhambi zako tena? Utasema kwa kuwa ukitubu Mungu anasamehe. Ni sawa kabisa. Hata mimi nakubaliana na hilo.

Lakini, je! Unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu ambacho anajua huwezi kukifanya? Hapana hata kidogo. Bwana wetu si dhalimu! Anafahamu kuwa WEWE MWENYEWE HUWEZI, LAKINI YEYE KWA KUWA YUMO NDANI YAKO ATAKUWEZESHA KUSAMEHE NA KUSAHAU.

Unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13) Ukiisha amua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo katika kinywa chako. Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)

Na hayo maneno ndiyo yamtiayo mtu unajisi (Mathayo 15:18 - 20) Usitafakari wakati wo wote ule, kosa ulilofanyiwa; mawazo mabaya yanapokujia juu ya kosa ulilofanyiwa, fahamu kuwa ni shetani na nafsi yako tu.

Biblia inasema mpingeni shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7) Na wala msimpe nafasi (Waefeso 4:27) Mwambie shetani aondoke na mawazo yake, kwa kuwa hilo kosa umelisamehe na kulisahau.

Na wakati huo utafakari nini? "Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI YAYO" (Wafilipi 4:8)

"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili; bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na TUKITEKA NYARA KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakorintho 10:3 - 5)

Kusahau ni vita vikali vya imani vinavyopiganwa katika mawazo yako. Unaposhinda vita hivi, unajikuta umepiga hatua kubwa ya imani! KWA HIYO KUMBUKA:Unasamehe kwa ajili yako Mwenyewe. Na unasahau makosa uliyokosewa kwa ajili yako mwenyewe. Kumbuka hili kila wakati, unamsamehe aliyekukosea na kuyasahau aliyokukosea kwa ajili yako mwenyewe.

Na kila wakati wazo likija kukukumbusha kosa hilo likatae kwa Jina la Yesu. Na USIKUBALI KULISEMA TENA MAISHANI MWAKO.