July 22, 2017

Itambue nguvu iliyo ndani ya ukweli.

Ukweli ni silaha ya mafanikio, watu wengi tumekuwa wajanja wajanja na kudiliki kusema uongo au udanganyi katika shughuli zetu za kila siku ili mradi tu tuweze kufanikisha kile tunachokita. Lakini tukumbuke kuwa wahenga walisema ya kuwa "njia ya mwongo ni fupi" hawakukosea, hata kama dili zako hizi za undanyifu unaona zinafanikiwa ukae ukijua kuwa ipo siku utaumbuka na kujikuta katika hali ya taabani bila msaada na hakuna ataekuamini tena.

Ni muhimu sana kujikita katika ukweli wa jambo lolote unalolifanya, je unafikiri ni kwa nini ni vyema kusema ukweli wakati wote? Ebu tuangalia katika nyaja hizi kadhaa;-

Katika familia
Familia yoyote ile yenye amani, furaha na upendo, huchangiwa na ukweli ndani yake, kama wewe baba ni muongo, ni rahisi sana kupoteza imani uliyojijengea kwa mke na hata kwa watoto wako, mfano mzuri ni pale wewe baba unapotoa ahadi kwa wanao ya kuwa wakifaulu vizuri darasani utawanunulia zawadi, lakini baada ya kutambua kuwa wamefaulu ukasema tena hutoi zawadi uliyoahidi, huo ni sawa na uongo kwa sababu umeshindwa kutimiza ahadi yako, hii moja kwa moja inakuwa imepunguzia imani kwa watoto wako ya kukuamini kwa kile uanchokisema hata kama hawatakwambia.

Ni vyema ukasimamia kwenye ukweli wa yale uyanenayo wakati wote,kwa kufanya hivyo utaendelea kulinda thamani yako.

Katika biashara 
Hapa sasa kuna changamoto kubwa itokanayo na kusimamia kwenye ukweli, mfano utakuta mtu anauza bidhaa ambazo anajua kabisa ni feki, lakini hataki kumweka wazi mteja wake kwa sababu anahofia ya kuwa pengine ataacha kununua hiyo bidhaa kwa kumwambia ukweli.

Ndugu yangu kumbuka kuwa kwa kufanya hivyo ndio utafanikiwa kumuuzia bidhaa hiyo feki mteja wako na utajawa na furaha kweli, lakini furaha hiyo ni ya muda tu, usitarajie mteja huyo kama atarudi tena kununua bidhaa hiyo  kwako hata kama utaleta bidhaa halisi(yaani original) siku nyingine.

Sasa kama umempoteza mteja wako naye akafaniwa kuwajulisha rafiki zake ya kuwa wewe ni bingwa wa kuuza bidhaa feki, hakika kitakuwa kilio cha kukosa wateja na hautashangaa biashara yako itakapokufa ghafla kwa sababu uhai wa biashara ni wateja.Kuwa makini sana ndugu, daima simamia kwenye ukweli tu hata wengine wakikucheka kwa vile wao wanafanikiwa, hayo ni mavuno ya muda tu wala yasikutishe.

Katika matumizi ya mtandao
Hatua za teknolojia zinakua siku hadi siku, huku huduma nazo zikizidi kuwa bora zaidi hasa za matumizi ya mtandao yaani internet, dunia sasa inaonekana kama kijiji, mawasiliano yamezidi kuwa bora kuliko wakati wowote uliopita, lakini mawasiliano haya yamejawa na ukweli ndani wake uliojikita katika msingi wa kuaminiana.

Hivi leo hata biashara nyingi zinafanyika duniani kote kwa njia ya mawasiliano, mtu yuko Tanzania anaagiza gari Japan kwa mtu ambae hata hamfahamu lakini biashara inafanyika kwa sababu ya kuaminiana. Hapa ndo tunapotambua kuwa dunia ni kijiji kwa matumizi haya bora ya teknolojia hizi, lakini hapa hapa na mataperi nao wanapenyeza lakini safari yao bado ni fupi.

Ndugu yangu dunia ya sasa imejawa na ukweli mtupu ambao ndo mtaji wa chochote unachokita, na kila mtu mtaji huu amepewa na mwenyezi Mungu, unachotakiwa ni kujiuliza wewe mwenyewe ndugu yangu hili swali, Je mtaji huu ninautambua? Kama nimeutambua ninanufaika nao vipi? Simamia kwenye ukweli ndugu yangu ili uweze kunufaika na tunu hii adimu kabisa katika safari yako ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.

Acha njia za mkato kwa kuwa mdanganyifu na muongo hatafika popote katika dunia ya sasa.

Makala hii imeandika na Emmanuel Natulu, mhamasishaji na Mtalaamu wa maswala ya upimaji ardhi.
Barua pepe: nnatulu2009@gmail.com

By Chief Hope 

Jiunge Na Tim Heaven Sasa! 
Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari mbalimbali juu ya muziki, mahusiano, mafanikio afya nk.