January 23, 2017

Mambo haya yatafanya moyo wako uwe na nguvu wakati wote.

MAMBO HAYA YATAFANYA MOYO WAKO UWE NA NGUVU WAKATI WOTE
Tarehe 24 Septemba ni siku ya saba ya moyo duniani, kauli mbiu ya siku hiyo ya mwaka huu ni "moyo wako una nguvu kiasi gani."
Mwaka 1999, shirikisho la moyo la kimataifa (World Heart Federation) liliamua kuchukua jumapili ya mwisho ya mwezi Septemba kuwa siku ya moyo duniani, ili kutoa mwito kwa watu kuzingatia madhara ya magonjwa ya moyo kwa afya ya binadamu, na kupendekeza watu wafuate tabia nzuri za maisha ili kukinga dhidi ya magonjwa hayo. Kuanzia siku ya kwanza ya moyo duniani mwaka 2000, siku hiyo ya kila mwaka ina kauli mbiu tofauti.

Hivi sasa magonjwa ya moyo ni moja ya vyanzo vikubwa vya vifo vya watu duniani. Takwimu husika zilizotolewa na shirikisho linalohusika na mambo ya moyo duniani zinaonesha kuwa asilimia 33.3 ya vifo vya watu duniani vinatokana na magonjwa ya mishipa ya damu ya kwenye moyo. Takwimu husika pia zimeonesha kuwa, asilimia 80 ya wagonjwa waliokufa kutokana na magonjwa hayo wako kwenye sehemu na nchi zenye mapato ya wastani au ya chini, na idadi ya watu waliokufa kutokana na magonjwa hayo bado inaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye tatizo la uzito kupita kiasi na wanaovuta sigara kwenye sehemu na nchi hizo.
 

Soma:Jikinge na shambulizi la moyo(Heart Attack)
 

Wataalamu wanasema, kiwango cha juu cha mafuta yaliyoko kwenye damu, uzito wa kupita kiasi, kuvuta sigara na upungufu wa mazoezi ya viungo ni vyanzo vikubwa vitakavyosababisha magonjwa ya mishapa ya damu ya kwenye moyo. Kuacha tabia mbaya za maisha, kula chakula chenye mafuta madogo na kufanya mazoezi ya viungo, kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupatwa na magonjwa hayo.

Wataalamu wa shirikisho linalohusika na mambo ya moyo duniani wanasema, utafiti umeonesha kuwa, kufanya mazoezi ya viungo, kula chakula bora, na kuacha tabia ya kuvuta sigara kunaweza kupunguza kwa asilimia 80 ya hatari kupatwa na magonjwa ya moyo au ugonjwa wa kiharusi, pia kunasaidia kufanya moyo wako uwe na nguvu zaidi.

Kufanya mazoezi ni muhimu kabisa kwa afya ya moyo. Utafiti umeonesha kuwa, kukimbia mbio kwa saa moja au zaidi kila wiki kunaweza kupunguza kwa asilimia 42 hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo; kutembea kwa kasi kwa nusu saa kila siku kunaweza kupunguza kwa asilimia 18 hatari ya kupatwa magonjwa hayo na pia kunapunguza kwa asilimia 11 hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.

Wataalamu wanasema, watu wakiacha kufanya mazoezi ya viungo, hatari yao kupatwa na tatizo la uzito wa kupita kiasi, ugonjwa wa kisukari na shinikizo kubwa la damu, itaongezeka na pia hali hiyo itaweza kusababisha kupungua haraka kwa uwezo wa moyo kufanya kazi. Kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara kunasaidia kupunguza hatari ya mabadiliko ya mishipa ya damu kuwa miembamba, kunasaidia kupunguza kiasi cha mafuta mwilini, kupunguza shinikizo la damu, na kusaidia kudumisha kiwango cha sukari ya damu kiwe cha kawaida.
Chakula chenye uwiano pia ni muhimu kwa afya ya moyo. Chakula hicho ni pamoja na kula matunda mengi, mboga, michele, nyama isiyo na mafuta, samaki na maharange na vyakula vingine bila mafuta au vyenye mafuta ya kiasi kidogo.

Aidha, kuacha tabia ya kuvuta sigara pia kunasaidia kudumisha nguvu ya moyo wako. Takwimu husika zinaonesha, watu wasiovuta sigara kwa wastani wanaishi kwa miaka minane zaidi kuliko watu wanaovuta sigara. Kupumua hewa zinazochafuliwa na moshi ya sigara kunaweza kuongeza asilimia 25 ya hatari kupatwa na magonjwa ya moyo, hata kupumua hewa kama hiyo kwa muda mrefu pia kunatoa athari mbaya kwa mfumo wa mishipa ya damu ya kwenye moyo na kuongeza hatari ya kutokea ghafla kwa magonjwa ya moyo.

Wataalamu wanasema, kudhibiti chanzo kikubwa cha hatari kunasaidia kukinga dhidi ya magonjwa ya moyo na kiharusi, na kudumisha nguvu na uwezo wa moyo kufanya kazi.
 

Soma:Njia tano za kutunza lips zako
 

Takwimu husika zinaonesha, magonjwa ya moyo na kiharusi yamekuwa vyanzo vikubwa kwa vifo vya binadamu, kwa wastani watu milioni 17.5 wanakufa kutokana na magonjwa hayo kila mwaka.