January 20, 2017

Unazijua sala muhimu unazopaswa kusali kila siku!!

 UNAZIJUA SALA MUHIMU UNAZOPASWA KUSALI KILA SIKU!!
Leo tutajifunza sala muhimu tunazopaswa kusali kila siku katika maisha yetu. Je unajua ni sala gani hizo? Karibu tuende pamoja tuweze kuzifahamu sala hizo. 

Upendo. 

Maisha yetu sisi binadamu yanadai upendo na wala siyo chuki. Kila mtu anahitaji upendo na kuthaminiwa kama binadamu katika maisha yake. 

Isikupite Hii: Upendo Ni Nini?

Upendo ni amri kutoka kwa Mungu ambapo mimi na wewe tunaalikwa tupendane bila kujali tofauti zetu mbalimbali tulizonazo kwa mfano, dini, vyama vya kitume, kisiasa, rangi, ukabila nakadhalika. Bila upendo dunia itakua siyo sehemu salama kuishi kwa kila mmoja wetu hapa duniani. 

Upendo ndio unaleta maendeleo hapa duniani, watu wachache wanaojitoa kwa moyo kwa ajili ya maisha ya watu wengine ndio wanafanya dunia inakuwa bora kama unavyoiona leo. Dunia isingekuwa kama hivi unavyoiona leo kama siyo upendo wa watu walioamua kufanya kitu kwa faida ya wengine na huenda waliojitoa kwa ajili ya upendo wao hata leo hawako duniani lakini mimi na wewe tunaalikwa kushiriki matunda ya upendo huo. 

Isikupite Hii: Hasara Za Kulipiza Kisasi - Mwalimu Christopher Mwakasege. (3)

Hivyo basi, dunia ili iweze kukua tunahitaji upendo kila mmoja ajitoe kwa kile alichonacho kuifanya dunia kuwa bora na tuache kuwa na ubinafsi kwani ubinafsi huleta udhaifu hapa duniani. 

Kusamehe. 

Katika maisha ya binadamu tunapaswa kusamehe kila siku ili uweze kuondoa fundo au uchungu ulioumbika ndani ya moyo wako. Kusamehe ni sala muhimu unayopaswa kusali kila siku ili uweze kuachilia mambo yaliyojaa moyoni. Kama binadamu kukoseana ni hali ya kawaida inayomkuta kila mtu na hakuna aliye mkamilifu hivyo njia pekee ni kujiweka wakfu katika kusamehe kila siku. 

Maisha yako hayawezi kuwa na furaha kama unaendelea kuwabeba watu moyoni. Muasisi wa msamaha ambaye ni Mungu mwenyewe anatualika sote mimi na wewe tuweze kusameheana hata saba mara sabini katika maisha yetu. Msamaha ni tendo la hiyari linalotoka ndani ya mtu, kuamua kusamehe kwa moyo ili uwe na amani ya moyo. Tuache kubebana katika mizigo ya kutosameheana na tusiendelee kukaa kiadui na kuendelea kuishi na majeraha katika nafsi zetu. Hivyo basi, ndugu msomaji, tunaalikwa kusamehe ili nasi tuweze kusamehewa. 

Kuwaombea wenzetu mazuri. 

Imekuwa ni desturi ya watu wengi kuwaombea mabaya wenzao na kuona faraja pale anapomwona mwenzake amepatwa na matatizo katika maisha yake. Hatuwezi kuendelea kwa kuombeana mabaya na kufurahia maisha ya jirani yako yakienda vibaya. Tunaweza kuendelea kwa kutakiana mema katika vile tunavyovifanya na vinavyofanya dunia yetu kuwa sehemu bora ya kuishi kwa kila mmoja wetu. 

Isikupite Hii: Sehemu Nne (4) Muhimu Za Kuchota Baraka Katika Maisha Yako

Chuki haina nafasi katika ulimwengu bali chuki huleta mauti. Tukiishi katika maisha ya wivu hatutoweza kufika mbali katika maendeleo kwani wivu ni ujinga unaomfanya mtu apende kumwona mwenzake abaki pale pale alipo wala kutopenda kumwona mwenzake akipiga hatua moja. Hivyo basi, ni vema kuishi katika upendo na kuwaombea wenzetu mazuri na kuwasaidia kuwaonyesha njia sahihi ya kupenda na siyo kufurahia wanapoanguka. 

Unyenyekevu. 

Tunapaswa tuwe na moyo wa unyenyekevu na wala siyo moyo wa kujikweza. Watu wamekuwa ni watu wa kujikweza katika jamii zetu kwa mambo mbalimbali. Anayejikweza atashushwa chini na anayejishusha atapandishwa juu haijalishi wewe ni nani na una cheo gani hupaswi kujikweza na kuwadharau wengine kwa kile ambacho unafanya. Unapaswa kumheshimu kila mtu kwani kila mtu ana nafasi yake hapa duniani na dunia haijengwi na mtu mmoja bali ushirikiano wa binadamu. Tunaalikwa tuishi katika falsafa ya ufagio ambayo ni unyenyekevu. 

Isikupite Hii: Unazijua Njia Mungu Anavyoweza Kunena Na Wanadamu

Chochote unachofanya fanya kwa unyenyekevu kama unatoa huduma ya utabibu basi toa kwa unyenyekevu mpaka mgonjwa ahisi kupona kabla hata hajatibiwa. Kuna faida kubwa sana katika maisha yetu kama kila mmoja wetu ataishi kwa unyenyekevu na kutoa huduma bora katika falsafa ya ufagio ambayo ni unyenyekevu. 

Hatua ya kuchukua; 

Ishi katika falsafa ya unyenyekevu, upendo na acha tabia ya kujiona wewe unastahili zaidi kuliko wengine. Kujiona wewe unastahili zaidi kuliko wengine mara nyingi huzaa wivu na ubinafsi. Kama ulikuwa siyo mtu wa kusamehe nenda sasa kamsamehe yule aliyekukosea ili uondoe uchungu au fundo lililoumbika ndani ya moyo na wasamehe wale waliokukosea. 

Isikupite Hii: Hatua Tano Za Uhakika Za Kutatua Tatizo Lolote Unalokutana Nalo

Kwa hiyo, tukitaka tuweze kuishi kwa upendo, kusameheana, kuishi katika falsafa ya unyenyekevu. Tuache kuishi kwa majivuno na kujikweza kwa wengine na kuanza kujiona wewe unastahili zaidi kuliko wengine. Tuache kuangalia tofauti zetu tulizonazo bali kila mmoja aishi kutimiza kusudi lake duniani na tuendelee kuwa sehemu ya mabadiliko tunayoyataka kuyaona hapa duniani.