• Isikupite Hii

  January 19, 2017

  Unawafurahisha vipi wazazi kipindi cha uhai wako?

   UNAWAFURAHISHA VIPI WAZAZI KIPINDI CHA UHAI WAKO!!
  Nawazungumzia wazazi na yale ambayo kila mmoja anapaswa kumfanyia mzazi wake aliyefanya jitihada za kumleta hapa duniani kisha kumlea hadi kufikia hapo alipo sasa.

  Kabla hatujasonga mbele na mada yetu ya leo hebu nikusimulie hadithi ya kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Tino ambaye huko nyuma alikuwa na maisha magumu sana huku mama yake akiishi kwa tabu huko kijijini kwao Shinyanga.

  Isikupite Hii: Mambo Yatakayo Kusaidia Kama Umeachana Na Mwenzi Wako

  Mwanzo mwa mwaka jana Mungu akamuwekea mkono wa Baraka, mambo yakaanza kumnyookea lakini wakati anajipanga kwenda kumjengea nyumba mama yake sambamba na kumfanyia mambo mengine ili aishi kwa furaha, yule mama akaugua ghafla na kufariki.

  Lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa Tino huyo, alijua thamani ya mzazi wake huyo lakini wakati akijiandaa kumfanya ajisikie kuwa amezaa, Mungu akakatisha ndoto zake.

  Wakati Tino akiumia kwa kushindwa kumpa furaha mama yake akiwa hai, wapo watu ambao hawajui kabisa thamani ya wazazi. Wamezaliwa, wakalelewa hadi wakakua na kuwa na maisha yao lakini leo hii wanajiona wao ndiyo wao, wazazi wao wamewasahau kabisa kana kwamba wamejileta wenyewe kisha wakajikuza wenyewe.

  Mimi nadhani ni wakati wako wewe msomaji kujitathmini upya na kuona umewafanyia nini wazazi wako katika kipindi cha uhai wao ili waweze kujivunia uwepo wako.

  Maisha yako ya raha mustarehe hayawezi kuwa na maana kama wazazi wako watakuwa wanaishi kimaskini. Kama ulikuwa hujui,

  Unawafanyia nini wazazi wako kipindi hiki wakiwa hai? 

  Wengi ambao waliwatelekeza wazazi wao baada ya kupata vijisenti leo hii wanaishi maisha ya ajabu sana, si ajabu yamesababishwa na laana za wazazi wao. Unataka hilo likupate ndiyo uanze kujuta?

  Isikupite Hii: Fanya Haya Mtaishi Muda Mrefu Kwenye Mahusiano.

  Usisubiri hilo, kama umejaliwa kuwa na wazazi wako mpaka leo na Mungu amekujaalia kufanya kazi na kuwa na kipato, hata kama siyo kikubwa sana, wakumbuke wazazi wako.

  Kumbuka wakati wewe ‘unawapotezea’ wazazi wako walio hai, wapo ambao wanatamani wazazi wao leo hii wangekuwa hai ili wawafanyie mambo makubwa

  Kwa nini? Kwa sababu wanajua umuhimu wao, wanajua bila wao wasingekuwa hivyo walivyo leo! Wewe hulijui hilo?

  Hili si jambo la kutumia nguvu kubwa sana kukufanya uelewe. Kikubwa hapa ni kwamba, tuwakumbuke wazazi wetu, tuhakikishe wanaishi maisha wanayostahili kuishi.

  Wafanyie kila unaloweza zuri ili kesho ukiwa umeondoka duniani, wazidi kukuombea. Pia wakitangulia wao, ubaki na amani kwamba hukuwatenga bali ulijitahidi kuwafanya wajivunie uwepo wako.