May 30, 2017

Mbinu 7 za kushinda usaili (interview) ya kazi.

mbinu za kushinda usaili (interview)
Umepata barua au simu kuhusu usaili. Zingatia yafuatayo;

1. Hakikisha umepata taarifa za kutosha
Mara nyingi upatapo barua au simu inayokuita kwenye usaili,mtu yeyote hujawa na furaha au msisimko wa ajabu.Ni ruksa kufurahi lakini kumbuka kuchukua taarifa muhimu(hususani kama habari hii inakujia kwa njia ya simu) kuhusu mahali utakapofanyiwa usaili(anuani,namba ya chumba,gorofa ya ngapi nk),muda na kama usaili huo utakuwa na watu zaidi ya mmoja au la.Taarifa kama hizo zitakusaidia katika kujiandaa.
   
Fanya uchunguzi kuhusu shirika/kampuni husika: Kabla ya kwenda kwenye usaili hakikisha kwamba umefanya uchunguzi wa kutosha kuhusu kampuni au shirika husika(research).Wanashughulika na nini,wateja wao ni kina nani,linamilikiwa na nani,lilianzishwa lini na kwa malengo gani.

Kama unamjua mtu au rafiki ambaye aliwahi kufanya kazi katika shirika au kampuni hiyo,mtumie ili kupata taarifa za ndani zaidi.Ufahamu wako kuhusu kampuni au shirika utawaonyesha wanaokufanyia usaili shauku uliyonayo kuhusu kampuni/shirika. Kumbuka tu kutojifanya unajua kupita kiasi.Bakia kwenye kiwango kinachostahili.

2. Mavazi na muda
Jambo mojawapo gumu linalomkabili mtu anayejiandaa kwa usaili ni uamuzi wa nguo gani za kuvaa. Jambo zuri ni kwamba una muda wa kujiandaa na pia kuchunguza. Cha kwanza unachotakiwa kufanya ni kuchunguza kuhusu utamaduni wa mavazi wa kampuni au shirika husika.Wanavaaje wafanyakazi wake?Kama ni kampuni ambayo kila mtu anavalia suti,basi jitahidi kwamba siku ya usaili na wewe uvae suti(hata kama ni ya kuazima).Lakini ukishindwa kupata suti usihofu; unachotakiwa kufanya ni kuvaa nadhifu.Jaribu kuepuka nguo zenye rangi kali au za kuwakawaka.

Epuka manukato makali au yanayonukia kupita kiasi.Kumbuka kuna watu wengine hawapatani na manukato makali.Usiwatibue.
 

3. Suala la muda.
Hakikisha unafika sehemu ya usaili mapema.Napendekeza ufike japo dakika kumi hivi kabla ya usaili.Hiyo itakupa muda wa kupumua,kuyasoma mazingira na kutuliza mawazo na akili yako.

4. Salamu, bashasha na tabasamu
Tofauti na wengi tunavyodhani,usaili huanza mara tu unapoingia kwenye ofisi husika. Katibu Muhtasi(secretary) au mtu wa mapokezi(receptionist) unayekutana naye kwanza huwa ni mtu muhimu wa kwanza unayekutana naye.Msalimie kwa heshima na tabasamu inayostahili.

Mara nyingi yeye huwa ndiye anayesimamia zoezi lote la usaili.Pendekezo lake ni muhimu wakati wa kufanya uchaguzi.Heshima hiyo na tabasamu mpe kila mtu utakayekutana naye katika ofisi hiyo.Kwa sababu huwajui,usifanye makosa.Usipomsalimia mtu na kisha ukakutana naye kwenye chumba cha usaili ni wazi kwamba utakuwa umeshaanza kujuta.

5. Sikiliza / Jiongoze kwa makini
Wakati wa usaili ndio umewadia. Huu ni muda wa maswali na majibu. Jambo la kwanza la kuzingatia ni kitu ambacho wenzetu wa magharibi wanakiita “body language”.Mwili wako huongea hata bila ya wewe kutamka neno.Hakikisha kwamba body language yako inaonyesha kwamba una nguvu za kutosha,una shauku na kampuni/shirika husika,upo tayari,unajiamini na upo makini. Keti kiheshima.

Siri muhimu ya kuweza kujibu maswali vizuri ni kusikiliza kwa makini.Lisikilize swali vizuri.Usipoelewa usisite kusema kwamba hujaelewa au ungeomba ufafanuzi zaidi kabla hujajibu.

Usisahau kutabasamu inapobidi na usione haya sana kuwaangalia wasaili wako machoni. Pamoja na kwamba kuna mila na desturi ambazo zinakataza wadogo kuwaangalia wakubwa moja kwa moja machoni,zipo nyakati ambazo mila hizo zinaweza kukuangusha au kukufanya uonekane kama mtu unayeficha kitu fulani wakati wewe unachofanya ni kitendo cha heshima!Kuwa makini ili kutofautisha mazingira.

6. Uliza maswali
Kutegemea na mtu au watu wanaokufanyia usaili,huwa inatokea(mara nyingi mwisho mwisho wa masaili) ukapewa nafasi ya kuuliza swali au maswali kama unayo. Ikitokea hivyo basi uwe tayari. Maswali kama vile ni lini watafanya uamuzi wao wa mwisho wa kuajiri,lini utegemee kusikia kutoka kwao ni muhimu.Unaweza pia kuuliza kama ukiajiriwa utakuwa unafanya kazi chini ya nani na katika kitengo chenye watu wangapi nk.Kwa ufupi usisite kuuliza maswali kama utapewa nafasi hiyo.
  
7. Shukrani na hitimisho
 Hatimaye usaili umefikia mwisho.Washukuru wasaili wako. Omba business card zao na kisha baadaye waandikie(barua ya kawaida au hata barua-pepe) ukiwashukuru kwa muda wao na kuwahakikishia kama kuna kitu hakikueleweka wakati wa usaili basi wasisite kuwasiliana nawe kwa ufafanuzi zaidi.

Kwa kumalizia labda nikukumbushe kwamba unapofanya maandalizi kwa ajili ya usaili yafanye kawaida tu na sio kwa shauku inayovuka mipaka. Kumbuka kuwa wewe.Usiige wala kujaribu kujifanya kuwa mtu mwingine.Ni muhimu pia kukumbuka kwamba pamoja na maandalizi yote,yaweza kutokea usipate hiyo kazi.Hilo likitokea,usikate tamaa. Endelea kutafuta,endelea kujiboresha zaidi.Roma haikujengwa kwa siku moja.