July 25, 2017

Kukataliwa kwako leo usife moyo, kesho watakutafuta.

 KUKATALIWA KWAKO LEO USIFE MOYO,KESHO WATAKUTAFUTA
Katikati ya mwaka 2009, Brian Acton akiwa ni mtaalamu na msomi katika masuala ya uhandisi wa programu za kompyuta (software engineer) ambaye hakuna mtu aliyehitaji kumpa ajira katika kipindi hicho. 

Licha ya kwamba alikuwa ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa miaka mingi baada ya kufanya kazi na makampuni makubwa ya kiteknolojia kama vile Yahoo na Apple kabla hajaachana nao mwaka 2007, Brian alishindwa kabisa kupata nafasi katika kampuni chipukizi zilizokuwa zikiingia kwenye soko la teknolojia kwa wakati huo mojawapo ikiwa ni twitter mwezi Mei na baadae facebook ukiwa mwezi Agosti mwaka 2009. 

Mitandao yote miwili ya twitter na facebook alimnyima kabisa Brian nafasi ya kuwa mmojawapo wa wahandisi katika kampuni zao, kitu ambacho kilimfanya Brian kuumia sana lakini hakukata tamaa pamoja na kukataliwa na mitandao hiyo.

Isikupite Hii: Anza Mwaka 2017 Kwa Kujiwekea Malengo Haya

Baada ya kukosa nafasi ya kujiunga katika makampuni makubwa mawili aliyokuwa ameweka nia ya kufanya kazi nayo ambayo ni facebook na twitter, Brian aliungana na mwenzake aliyekuwa wakifanya kazi pamoja katika kampuni ya Yahoo hapo nyuma, Jan Koum, ambapo waliweza kutengeneza “application” iliyoweza kutawala na kupata umaarufu mkubwa duniani katika upande wa kutuma ujumbe mfupi (messaging). 

Ndio. Huyu ndiye Brian Acton mmoja wa waanzilishi na waendelezaji wa mtandao wa WhatsApp. Mwaka 2014 facebook waliweza kurudi kwa Brian na Koum kuomba nafasi ya kununua App hiyo ambapo waliweza kuwalipa kiasi cha $19 bilioni ikiwa ni fedha taslimu na pia kwa njia ya kugawana hisa. Hii imemfanya Brian kuwa na utajiri unaofikia 5.1 bilioni akiwa ni miongoni mwa mabilionea wakubwa ndani ya taifa la Marekani na duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes hadi hivi sasa. Huku mshirika mwenzake Jan Koum akiwa na utajiri unaofikia $8.2 bilioni hadi sasa.

Nini unachotakiwa kujifunza kupitia ujumbe huu mfupi. Kuna mambo 4 ya kujifunza kupitia hali halisi aliyopitia Brian Acton:

1: Usivunjike Moyo Unapokataliwa.

Jambo muhimu unalopaswa kulifahamu katika suala la kutafuta mafanikio ni kushikilia ndoto yako katika kila hali, haijalishi utapitia katika kipindi au hali gani inayoweza kukufanya ushindwe kusimama na kuendelea mbele. Unachopaswa kufahamu ili ndoto yako ifanikiwe inahitaji kiwango cha furaha na amani ndani yako kila wakati, unaporuhusu kukata tamaa unakuwa umeruhusu moyo wako kuvunjika na kushindwa kuendelea mbele na huo utakuwa ni mwanzo wa kushindwa kufanikiwa kwako. Usiruhusu hali yoyote ile kuja katika maisha yako na kukupotezea furaha na amani ambavyo huwa kama sumaku na chaji ya kukusukuma katika kuelekea mafanikio ya ndoto yako.

Isikupite Hii: Njia 5 Zitakazokupa Kipato Kupitia Mitandao Ya Kijamii.

Kumbuka unapokata tamaa unaruhusu hali ya kushindwa, hebu fikiri kama Brian Acton angekata tamaa baada ya kukataliwa kujiunga kwenye kampuni ambazo ilikuwa ni ndoto ya maisha yake ingekuwaje? Lakini pamoja na kukataliwa Brian hakukata tamaa akaamua kutumia hali hiyo kama changamoto ya kumfanya afikiri zaidi kitu gani cha kufanya, na hatimaye akaja na wazo jipya la kutengeneza application ya WhasApp akiwa pamoja na mwenzake walioacha kazi pamoja Yahoo, Jan Koum.

2: Kukataliwa kunaweza kuwa ni fursa ya pili ya kufanikiwa kwako.

Hii inatusaidia kujua kumbe tunauwezo mkubwa ndani yetu. Najaribu kufikiri kwa upande wa pili kama Brian Acton angekubaliwa kujiunga na kampuni ya twitter au facebook leo hii tungepata wapi kuwasiliana kwa haraka na kuweza kusaidiana kwa kupitia mtandao wa WhatsApp. Nataka uelewe kuwa si kila mahali unapopita na kukataliwa ndio umefika mwisho wa kutokufanikiwa kwako. Ni vyema zaidi wakati mwingine ujifunze kutazama changamoto zinazokuijia au kukataliwa huko kama fursa ya kufuata ndoto zako ulizonazo kwa muda mrefu. Brian alipata akili na ubunifu ukaongezeka zaidi baada ya kukataliwa, hii ni wazi kukataliwa huko kulikuwa ndio fursa ya yeye kufanikiwa na kufanya mambo makubwa hapo badae.

Isikupite Hii: Njia 10 Muhimu Unazotakiwa Kuzifuata Kama Unataka Kuwa Millionea.

Leo hii tunaona matajiri wengi zaidi ya Brian walipitia kukataliwa ndio ukawa mwanzo wao wa kutoka na kufanikiwa kimaisha. Hebu mtazame Jack Ma mmiliki wa Alibaba alikataliwa mara 30 katika kampuni mbalimbali ikiwemo KFC na badae akakataliwa kujiunga na chuo kikuu cha Harvard mara 10 na aliwahi kufeli mtihani wa chuo na kushindwa kuendelea mbele kimasomo, lakini leo hii Jack Ma ni bilionea na tajiri mkubwa duniani. Unachopaswa kufahamu ni kujifunza kupitia hali yoyote unayopitia sasa na kuheshimu mawazo na nia ya dhati ya kufuata ndoto zako. Hupaswi kushindana na watu wanaokudharau leo hii, huku ukweli ni kuwa una mtaji mkubwa wa kuanzia uliomo ndani yako. Amua kusimama hadi uone matokeo makubwa katika ndoto yako na hapo ndio mwanzo wa kuheshimiwa na waliokukataa unaanza kuchipuka.

3: Tafuta mtu wa kukusaidia kuongeza nguvu ili kuleta matokeo makubwa.

Kikubwa unachotakiwa kufahamu ni kuwa unatakiwa kuelewa ni nani unayeweza kuendana nae katika njia moja ili akusaidie kuleta matokeo makubwa katika ndoto zako na kuishangaza dunia. Brian baada ya kukosa nafasi ya kujiunga na kampuni ya twitter na facebook aliamua ndani ya mwaka huo huo kumfuata rafiki yake waliyekuwa wakifanya kazi pamoja kwa jina Jan Koum. Baada ya Brian kuungana na rafiki yake Koum ndio walipoweza kuushangaza ulimwengu na kuja na “application” iliyopindua ulimwengu katika upande wa ujumbe mfupi, WhatsApp.

Isikupite Hii: Anza Siku Yako Kwa Furaha Kwa Kufanya Haya Mambo Nane (8)

Leo hii mamilioni ya watu duniani wanatumia mtandao wa WhatsApp katika kuwasiliana hii ni kwa sababu ya watu ambao waliamua kutokukata tamaa na kuamua kuzifuata ndoto zao hadi walipoona matokeo makubwa yakitokea. Jiulize una ndoto gani uliyoikatia tamaa baada ya watu kuinuka na kukuvunja moyo hata kuacha kuifuata ndoto yako tena? Nakusihi usikate tamaa bali amua kuifuata na kuiishi ndoto yako hadi uone matokeo makubwa yakitokea katika maisha yako. Jifunze kutafuta mtu wakuambatana nae katika kufanikisha malengo na ndoto yako uliyonayo hasa pale unapopitia katika wakati mgumu, kumbuka mmoja anaua makumi mkiwa wawili mtaua maelfu.

4: Ukiongeza bidii na ufanisi kwa kile unachofanya amini waliokukataa watakutafuta.

Ndio. Hii ni wazi kabisa ukitaka wanaokudharau wakutafute hapo badae ni wazi unahitaji uweke muelekeo wa kudumu (focus- concentration) kwenye kile unachokifanya kama sehemu ya kutimiza ndoto zako. Usiruhusu kutumia vibaya muda wako katika ushindani na magomvi au kuweka visa kwa sababu umefanyiwa hila au ubaya wa aina yoyote, jifunze kuutazama ubaya kwa hali chanya kwa ajili ya kukupa hatua mpya na kutengeneza misuli ya mafanikio maishani mwako. Unahitaji kuushinda ubaya kwa wema ili kuongeza hatua za mafanikio na spidi ya kufika kule unakoelekea. Jifunze kuona hali ya kuchekwa na kudharaulika kama sehemu muhimu inayokuja kwenye maisha yako kukusogeza (kuku-push) kwenye hatima njema ya kufanikisha ndoto yako.

Isikupite Hii: Sehemu Nne (4) Muhimu Za Kuchota Baraka Katika Maisha Yako

Facebook baada ya kuona WhatsApp inakuja kwa kasi na inaleta ushindani mkubwa katika soko la teknolojia ya mitandao ya simu, hata kuona hali ya kuja kupoteza watu wengi katika soko lake alilotawala kwa kipindi kirefu, hali hii ilimfanya mmiliki wa facebook, Mark Zuckerberg kuamua kurudi kwa Brian Acton yule waliyemkataa mwanzoni na kwa sasa akitaka mwenyewe kufanya nae biashara. Nataka nikuambie bidii na ufanisi wa Brian Acton baada ya kukataliwa ndio uliomfanya mmiliki wa facebook kurudi nyuma na kuona kunahitajika busara ya kuungana na Brian kuliko kupoteza watumiaji wengi wa mtandao wake. Ukiongeza bidii na ufanisi utafanya makubwa na kusababisha waliokukataa hapo mwanzo kurudi kwako na kuomba urafiki kwa upya. Kikubwa endelea kufanya unachofanya hadi ulete matokeo yatakayokutambulisha katika dunia na kuwafanya adui zako kurudi nyuma na kukuzingatia.