July 24, 2017

Kanuni 7 za kuishi na watu vizuri.

 KANUNI SABA (7) ZA KUISHI NA WATU VIZURI
1. Epukana na biashara au na shughuli zisizo halali. 
Unapofanya shughuli au biashara isiyo halali inakuondolea uaminifu kwa jamii inayokuzunguka.

Kwa mfano, kama mtaani au kazini kwako unakuwa mtu usiyeeleweka kwa kuwa watu wanajiulizauliza kile unachofanya na wasipate majibu, hiyo si jinsi au njia nzuri ya kuishi na watu.

Vile vile biashara hizo zinaweza kukusababishia matatizo kama ya kufunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani endapo utakutwa na kosa.

2. Jifunze kutokuwa mchoyo au uwatakie watu wengine mambo mema.
Baadhi ya watu waliofanikiwa huwa hawapendi maendeleo ya wengine. Wanapoombwa msaada ni wagumu kutoa.
Mfano kwa baadhi ya wanafunzi shuleni wakiojaaliwa kuwa na uwezo kiakili huwa hawapendi kutoa msaada kwa wenzao. Hata maofisini kuna baadhi ya watu wasiopendi maendeleo ya wenzao kwa kumsemea mambo yasiyo ya kweli
kwa bosi wao.

3. Epukana na lugha ya ubinafsi, mfano: mimi, changu, n.k.
Badala yake tumia chetu, sisi n.k. Lugha hizo si nzuri katikati ya jamii inayokuzunguka. Unapokuwa na tabia hiyo inakujengea chuki miongoni mwa wanaokuzunguka. Ni vizuri kushirikiana vifaa vya ofisini, shuleni na katika maeneo mbalimbali na jamii.

Inawezekana wakati mwingine mtu anakuwa na lugha hiyo ya ubinafsi kutokana na mazingira yaliyopo. Mfano wewe ni msafi na wenzake unaoishi nao, kufanya kazi nao au kusoma nao wanakuwa na tabia ya uchafu. Kama umeshajaribu kuwabadilisha bila mafanikio, ni vizuri kutumia busara ya kununua vitu kama vyako na kuwapa vile ambavyo una uwezo navyo.

Hii itakusaidia kila mtu kutumia kifaa chake, mfano vikombe maofisini - kila mtu ana usafi wake, vioo kwa akina dada, chanuo za kuchania nywele na mfano wa vitu kama hivyo. Jitahidi kutokuonyesha hali hiyo kwa gharama yoyote ile.


Thamini utu wa mtu bila kujali uwezo au nafasi yake katika jamii. Kumbuka kwamba siku hazifanani, kwani waweza kupokea msaada mkubwa wa kimawazo au wa hali kutoka kwa mtu usiyemtarajia.

Watu wengine wanapotoa msaada kwa wenzao hujisahau na kuanza kutangaza au kumnyanyapaa yule aliyemsaidia huku akiona ni sawa.

Mfano rahisi unakuta labda kuna watu wengine wamewapokea ndugu zao au watu ambao hawana uwezo na kuishi nao nyumbani kwao. Kutokana na kuishi naye basi ufadhili unageuka kuwa mateso kwa kuwa kila kazi ataifanya huyo aliyesaidiwa au kila mara atakuwa anatumwa maeneo ya mbali mara nyingine pasipo hata na nauli.

Si vibaya kumtuma wala si vibaya kusaidiwa na mtu kama huyo, ila isivuke mipaka kwani itakujengea picha mbaya kwa wanaokufahamu pamoja na huyo unayemsaidia atakapoamua kuondoka kwako.

4. Epukana na tabia ya kugombeza, kutukana au kudharau wengine.
Iwapo watu walio chini yako wamekosea au wamefanya kinyume na ulivyotarajia; jaribu kuwaelekeza kwa upole bila kutumia jazba au hasira. Usiendekeze lugha za matusi, dharau au ugomvi, kwani huweza kushusha hadhi yako na hata utu wako.


Isikupite Hii: Zijue Dalili 4 Za Mpenzi Mkorofi.

Watu wengine wamejiendekeza katika tabia ya kupenda kugombagomba ovyo hata bila sababu, wengine hudiriki hata kutukana au kudharau wengine.

Hii ipo sana maofisini. Mabosi walio wengi hujisahau kuwa nafasi wanazokalia ni za muda tu, hivyo hudharau wale walio chini yao kwa kuwasemasema ovyo na kuwatukana pasipo sababu ya msingi.

Hata kwa upande wa baadhi ya wanawake na wanaume wawapo nyumbani kwao huwa na tabia hiyo kwa watoto wao, wafanyakazi waliowaajiri au ndugu wanaoishi nao.


Isikupite Hii: Mambo 6 Yatakayo Weza Kukutopotezea Heshima Yako.

Ni vizuri kuacha tabia hiyo, kwani inakuondolea heshima na kukufanya udharaulike.
 

Pia wakati mwingine utakuta wenye mali si wasemaji, lakini wale wanaowaachia majukumu kidogo ndiyo wanaokuwa na tabia hizo mbaya katika jamii. Gombeza pale inapostahili lakini isiwe mazoea, kamwe usitukane wala kuleta dharau kwa wengine. Huo ni utovu wa nidhamu.

5. Jifunze kuvumilia mienendo ya imani ya dini nyingine.
Watu wengine wana tabia ya kudharau au kutothamini misimamo ya wengine ya kiimani. Utamkuta mtu anakashifu hadharani dini za watu wengine kwa kutumia vigezo visivyokuwa na maana.

Suala hili katika jamii yetu inayotuzunguka limekuwa likileta mizozano na wakati mwingine watu huamua kupigana. Mnapokuwa watu wenye imani za dini tofauti katika ofisi zenu, vyuoni au hata kwenye mikusanyiko mbalimbali, jaribu kuvumilia kila hatua ambayo kwako unaiona ni kinyume na maadili yako. Ukishindwa hali hiyo ni vizuri uondoke na kuwapisha wenyewe waendelee.

Kwa mfano, kwenye msiba labda wewe ni wa madhehebu fulani, hivyo umekwenda kwenye msiba wa imani tofauti na yako, ni vizuri kufuata taratibu zilizopo mahali pale, na kama unajiona huwezi basi ili kuepusha shari ondoka eneo hilo uwaachie wenyewe ili usionekane ni kituko.

Ni vizuri ukae kimya uwaachie wenyewe waendelee na ratiba na shughuli zao kuliko kuanza kupayuka ovyo au kukosoa katika msiba huo. Tulia wakimaliza shiriki nao kwenye msiba ndivyo maisha yalivyo.

6. Usiwe mkali kwa watu, jenga uhusiano mzuri.
Ukali ni hulka ambayo huwafanya watu wawe mbali na wewe na hata kusababisha kukosa marafiki. Unaweza kukuta mtu ana nafasi nzuri katika jamii lakini hakuna mtu mwenye mazoea naye kutokana na ukali wake. Mfano katika ofisi mwajiri unakuwa mkali kiasi kwamba wafanyakazi wako wanakosa uhuru wa kujieleza kwako wanapokuwa na matatizo yao binafsi au ya kiofisi.


Isikupite Hii: Kanuni Saba (7) Za Kuishi Na Watu Vizuri

Unapokuwa na uhusiano mzuri na watu; hali hiyo inakufanya kukubalika, kuheshimika, kupendwa na jamii inayokuzunguka. Mfano mwalimu anapokuwa karibu na wanafunzi wake, huweza kuvuta hisia zao za usikivu na hatimaye kufanya vema katika masomo yao.

7. Uwe mwangalifu sana na mwanamke/mwanaume asiyekuwa wako.
Siku zote mazoea na watu wa jinsia tofauti na ya kwako lazima yawe na mipaka. Kuna watu ambao hawawezi kutawala hisia zao hata wanapokuwa na wenzao ambao tayari wana familia zao.


Isikupite Hii: Kama Wewe Ni Mke Wa Mtu Jiepushe Na Haya

Hii inajitokeza sana shuleni, vyuoni, maofisini na hata maeneo ya kuishi; unakokuta msichana au kijana anakuwa na mazoea yaliyopitiliza na mume au mke wa mtu, hali inayoweza kusababisha mtafaruku kati ya pande husika.

Wakati mwingine unakuta wanawake/wanaume waliooa au kuolewa wanakuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa zao, hali inayosababisha kutoelewana baina yao na wenzi wao; wakati mwingine hata kusababisha kuvunja ndoa zao.