July 14, 2017

Kutana na Ramesh Babu kinyozi anayemiliki magari 75. (+video)

Unaweza ukaona ni kitu kama cha kushangaza au haiwezekani lakini huu ndio ukweli, binadamu anapoamua kujikubali na kuthamini kile anachokifanya anauwezo mkubwa sana wa kufika mbali kimafanikio kuliko anavyofikiri. 

Ukweli huu unakuja kujidhihirisha wazi, kwa kijana Ramesh Babu ambaye anavuna utajiri wa kutosha kutokana na kunyoa tu. Mfanyabiashara Leonard Willoughby aliwahi kusema; ‘siku utakayoanza kuishi kwa kuifuata mipango yako unayopanga, kila kitu katika maisha yako kitabadilika kabisa.’ Inawezekana watu wengi wanaufahamu msemo huo, lakini Ramesh Babu aliyatendea kazi maneno hayo.

Babu ambaye ni kinyozi bilionea pekee nchini India, anasema aliuchukua ushauri wa Willoughby na kuamua kuutendea kazi tangu siku ya kwanza alipousikia na kwamba maisha yake yalianza kubadilika.

Kwa mujibu wa Jarida la ‘Your story’ la nchini India, Babu amefanikiwa kuvuka vizingiti kadhaa vya umaskini hadi kufikia kuwa mmoja wa watu maarufu nchini humo akiwa na uwezo wa kununua gari aina yoyote anayoitaka. 

Asema kuwa mwaka 1994 alinunua gari lake la kwanza aina ya Maruti, lakini aliendelea na kuhifadhi fedha kidogo kidogo alizokuwa anazipata hadi mwaka 2004, alipoanzisha kampuni ya kokodisha magari, ikiwa na magari saba wakati huo.

Hadi kufikia mwaka jana, kinyozi huyo amenunua magari 75 kati ya hayo matano ni ya kifahari yakiwemo, Mercedes, BMW, Audi, mabasi kumi na lile analolipenda liitwalo Rollsw Royce. Pamoja na utajiri huo mkubwa alionao Babu, bado anaendelea na kazi yake ya kinyozi.