July 14, 2017

Makosa 5 yanayokufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa.

1. Umekuwa ukipoteza muda sana.
Hili ndilo kosa ambalo umekuwa ukilifanya na ndilo linalokufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Umekuwa ukiishi sana kwa kupoteza muda. Kumbuka, muda ndiyo kila kitu katika maisha yako ya mafanikio. Unapokuwa unatunza muda wako vizuri, unakuwa unajiweka katika nafasi nzuri ya kufanikiwa tofauti na ambavyo ungekuwa unapoteza muda. Watu wengi wenye mafanikio ni watu wa kujali sana muda wao kila siku. Kama unataka kubadilisha hali ya maisha uliyonayo, jifunze pia kutumia muda wako vizuri.

2. Umekuwa ukijiwekea malengo mengi sana.
Kati ya kosa ambalo watu wengi wamekuwa wakilifanya na linalowazuia kufikia mafanikio makubwa ni kujiwekea malengo mengi ambayo inakuwa ni vigumu kuyafikia yote kwa pamoja. Ili uweze kufikia mafanikio unayoyataka ni muhimu sana kujiwekea malengo machache ambayo unaweza ukayatekeleza kwa urahisi. Unapokuwa una malengo mengi ile nguvu ya uzingativu inakuwa inapungua kwako na utajikuta hakuna unachokifanya juu ya hayo malengo yako. Chagua malengo machache na muhimu kisha anza kuyatekeleza na utafanikiwa.


3. Umekuwa ukiishi maisha bila kujilipa wewe kwanza.
Mara nyingi umekuwa ukifanya kazi na umekuwa ukijipatia kipato, ambapo haijalishi ni kikubwa au kidogo kiasi gani lakini umekuwa ukifanya kosa hili la kutokujilipa wewe kwanza. Hili ni kosa ambalo limekuwa likikurudisha nyuma bila wewe kujijua. Unaposhindwa kujilipa wewe unakuwa unapoteza pesa ambayo ingeweza kukusaidia katika kuwekeza kwa baadae, ambapo pesa hiyo ingekuwa nyingi. Katika suala la kujilipa wewe kwanza, mara nyingi unashauriwa kujilipa kwa kutenga asilimia kumi ya kipato chako. Hiyo ni pesa halali ya wewe mtafutaji ambayo ni lazima ujilipe.


4. Umekuwa ukiishi maisha ya kuogopa sana.
Kuna wakati ili tuweze kufanikiwa katika maisha yetu tunalazimika kujitoa mhanga na kuhakikisha malengo yetu yanatimia. Wengi huwa tunakosea kwa kujikuta ni watu wa kuogopa hata kwa vitu vidogo ambavyo tusingepaswa kuviogopa na tumekuwa tukikwama kutokana na kuogopa sana. Watu wenye mafanikio makubwa duniani, ni watu siku zote wa kujitoa mhanga, ambao hawaogopi kitu ni watu wa kufanya na kusubiri matokeo makubwa kwa kile walichokipanda. Utafafikia ngazi kubwa ya mafanikio ikiwa utavaa roho ya ujasiri itakayokuwezesha kufanikiwa na sio kuogopa.


5. Umekuwa ukiishi kwa mitazamo hasi sana.
Hautaweza kufanikiwa kwa chochote kile kama maisha yako yatakuwa yanaongozwa na mitazamo mingi sana hasi, ikiwa ni pamoja na kukosa tumaini, hamasa na kujiona hufai kwa kile unachokifanya. Umekuwa ukikosea sana katika safari yako ya mafanikio hasa pale unapojiona hasi, badala ya kujiangalia kwa mtazamo chanya ili uweze kufanikisha mambo yako. Hili ni kosa ambalo umekuwa ukilifanya mara kwa mara katika maisha yako na kwa sehemu limekuwa likikurudisha nyuma. Kwa vyovyote vile unavyoyaona maisha yako ndivyo yatakavyokuwa. Ukijiona huwezi, hutaweza kweli na ukijiona unaweza utaweza kweli na kufikia ndoto zako.