July 31, 2017

Mama kijacho/mpya unavyoweza kuwa mlezi bora

Kuwa mama si kitu rahisi kama watu wengi wanavyodhani. Kuna mambo mengi yanayopaswa kuzingatiwa ili kuwa si tu mama bora bali pia mlezi sahihi wa familia.

Yapo makosa mengi yanayofanywa na mama wapya katika malezi. Mengi ya makosa haya hufanyika kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya malezi.

Makosa kama haya yakiepukwa, mama humudu kulea mtoto wake katika mstari ulio sawia.

Pamoja na kuwa kufanya makosa ni njia mojawapo ya kujifunza, lakini wakati mwingine ni vyema kuepuka makosa.
Angalia makosa yanayofanywa na mama wapya katika malezi:

Kujilazimisha kurudia kwenye hali ya kawaida kwa haraka
Kosa kubwa linalofanywa na akina mama wengi waliojifungua kwa mara ya kwanza, ni kujilazimisha kupona ili waendelee na maisha yao ya kawaida.

Wengi wetu hutafsiri, kitendo cha kujifungua kama kutua mzigo. Hivyo hujilazimisha kukaa kwa muda mfupi kabla ya kurudi kwenye majukumu ya kawaida ya kila siku.

Kama wewe ni mama uliyetoka kujifungua mtoto wako wa kwanza, hakikisha unaupa mwili wako muda wa kutosha wa kupumzika, na hivyo kurudi kwenye hali yake ya kawaida taratibu.
Kukata kucha za watoto wao wakati wakiwa macho

Wakati nilipopata mtoto wangu wa kwanza, hili lilikuwa kosa jingine nililokuwa nikilifanya. Nilikuwa sifahamu kuwa ni rahisi sana kumkata kucha mtoto akiwa amelala. Kama wewe ni mama nafikiri unaelewa ilivyokuwa vigumu kumkata mtoto kucha akiwa macho, si ajabu ukaishia kumkata. Lakini kwa mtoto anayeanza kupata akili, unapomkata kucha akiwa macho, kuna hatari ya kufanya majaribio akiwa peke yake.
Kujishusha

Hili ni kosa jingine linalofanywa na akina mama wapya. Mara nyingi hujiona kama wasiojua kitu. Na pia hujilaumu kwa kila kosa wanalofanya kwa watoto wao. Ni kweli kabisa kwamba ni vigumu kujifunza umama, lakini jinsi unavyokuwa karibu na mtoto unajikuta ukijiongezea kujiamini. Na unapojiamini kwenye malezi, moja kwa moja unamweka hata mwanao kwenye nafasi nzuri ya kukuamini na kukupenda zaidi.

Kuwaweka pembeni waume zao

Nilifanya kosa hili wakati nilipopata mwanangu wa kwanza. Lakini baada ya mume wangu kulalamika kuwa namweka pembeni, niligundua kuwa kumbe na yeye ana nafasi yake kama mzazi kwa mtoto pia.

Hili nililifanya bila kukusudia kwani nilipojifungua tu ghafla nikajikuta nakuwa karibu zaidi na mtoto wangu kuliko mtu yeyote, jambo hilo pia lilichangia kumnyima nafasi mume wangu kuwa karibu na mwanawe. Kwa bahati nzuri ni rahsi sana kurekebisha tatizo hili, ni kumruhusu tu mumeo kuwa karibu na mwanawe, ikiwezekana kumpa nafasi hata ya kumbadilisha nguo pamoja na huduma nyingine.

Hawaulizi maswali

Mara nyingi akina mama wapya wanakuwa wagumu sana kuuliza, licha ya ukweli kuwa wanahitaji kujua vitu vingi sana. Wao hudhani kuwa maswali yao huonekana ya kijinga jambo ambalo si kweli.

Kuuliza maswali kuhusiana na kumhudumia mtoto, ndio hasa maana ya malezi. Na madaktari wa watoto wako kwa ajili hiyo. Uliza kila usichofahamu kuhusiana na malezi ya mtoto wako. Hii itasaidia kukujenga na kukuweka kwenye mstari wa mama bora.
Wanaogopa kuomba msaada

Pamoja na kuwa kuomba msaada pale unaposhindwa vitu Fulani hususani katika uleaji wa mtoto ni njia nzuri ya kujifunza, wamama wengi wapya hili hulionea haya. Jambo hili hupelekea kufanya vitu kinyume nyume au kufanya makosa yanayoweza kuathiri hali ya mtoto.
Kwa mfano unyonyeshaji wa mtoto. Kuna taratibu maalum zinazotakiwa kufuatwa na mama wakati wa unyonyeshaji. Hivyo ni muhimu mama kupata msaada wa maelekezo ya jinsi ya kunyonyesha.

Mara nyingi utokaji wa maziwa hutofautiana kutoka kwa mama mmoja hadi mwingine. Wapo wanaowahi kutokwa na maziwa lakini wapo wengine wanachelewa. Pia katika utokaji wapo wenye kutoa maziwa mengi, huku wengine yakitoka kidogo kidogo.

Ni vyema kuomba msaada wa maelekezo kwa wataalamu ili unyonyeshaji wako uwe wa tija.Pamoja na kuwa hakuna mama mkamilifu, unapaswa kujitahidi kuwa mama mzuri.