July 21, 2017

Ndizi hupunguza maumivu ya hedhi.

Kuna matunda mengi yenye faida mwilini. Mojawapo ni ndizi mbivu ambazo wataalamu wa afya wanasema huweza kupunguza tatizo la wanawake kupata maumivu wakati wa hedhi.

Tovuti sayansi inayojihusisha na masuala ya tafiti za vyakula inaeleza kuwa iwapo mwanamke anapata hedhi na kupata maumivu ya tumbo, anaweza kupata nafuu iwapo atapendelea kula ndizi mbivu. 

Imeeleza kuwa ndizi mbivu zina vitamini B6 kwa wingi hurekebisha kiwango cha sukari na kupunguza madhara kwa mtumiaji, huku madini ya chuma, yanayopatikana kwa wingi yakizuia upungufu wa damu, kutokana na kufanya kazi ya kuzalisha chembechembe za damu mwilini.

Tunda hili pia hutibu na kupambana na tatizo la kupanda na kushuka kwa shinikizo la damu, kwa sababu lina kiwango kikubwa cha madini ya potasiamu huku likiwa na chumvi (sodium) ndogo.

Kituo cha kuangalia ubora wa vyakula nchini Marekani kijulikanacho kama Center for Food Safety and Applied Nutrition (CFSAN) kimelitaja tunda hilo kuwa ni bora katika kurekebisha shinikizo la damu, kuwasaidia kina mama kupunguza maumivu wakati wa hedhi na kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya kupooza.