July 20, 2017

Wewe pia ni sababu ya ongezeko la watu maskini nchini!

Je! Wajua kwamba na wewe pia ni sababu ya ongezeko la watu maskini?

Ni ajabu, na inashangaza sana kwamba tukienda kununua bidhaa mbalimbali kwenye maduka makubwa (supermarket) au malls kama vile Mlimani city au Uchumi huwa hatulalamiki wala hatuombi wapunguze bei ya bidhaa japo bidhaa hizo huwa na bei kubwa sana.

Lakini sisi hawa hawa tunapoenda kununua bidhaa kwa wafanya biashara wadogo wadogo kariakoo na sehemu nyingine kwa machinga ama nyanya na mboga mboga, kwa wauza magenge huwa tunalalamika sana tukiomba watupunguzia bei.

Kumbuka wafanyabiashara wadogo wadogo hawafanyi biashara ili wajenge maduka makubwa mengine au wanunue magari, bali wanafanya biashara ili wapate kitu cha kuingiza kinywani, wapeleke watoto shule na kuendesha maisha yao ya kila siku. 

Tunapo walalamikia hawa wafanyabiashara wadogo wadogo huku tukiwataka watupunguzie bei huwa tunawaumiza na kuwazidishia umaskini mara dufu.