October 14, 2017

Sayansi yaonesha kwa nini baba ni muhimu katika malezi.

Wapendwa akina baba, watoto wenu wanawahitaji katika malezi yao kama vile wanavyowahitaji mama zao! Kwa miongo kadhaa, wanasaikolojia na watafiti walidhani kuwa mahusiano kati ya mama na mtoto yalikuwa muhimu katika maisha mtoto zaidi ya mahusiano ya mtoto na baba yake. 

Tafiti zao zililenga kujifunza uhusiano hayo na ndiyo maana tulifanywa kuamini kuwa mtoto anapata tabia kutoka kwa mama yake, akiwa na tabia nzuri, mama husifiwa na akiwa na tabia mbaya, mama hulaumiwa.

Hivi karibuni tafiti zimeanza kupata taarifa tofauti kabisa juu ya umuhimu wa baba katika malezi. Mwili wa baba, kama ulivyo wa mama unazo hisia zinazoshabihiana na zile za mama katika malezi ya mtoto. Hivyo basi uwepo wa baba una athari karibu sawa na uwepo wa mama katika malezi ya watoto. Matatizo ya kitabia, msongo wa mawazo, utumiaji wa madawa ya kulevya, matatizo mengi ya kisaikolojia kwa ujumla wake yote haya ni mfano wa baadhi ya matatizo yatokanayo na kumkosa baba na si kwa kumkosa mama katika maisha ya mtoto. 

Hii ina maanisha kuwa mtoto aliyelelewa bila ya baba ama baba asiyejishughulisha na malezi anayo nafasi kubwa kuingia katika mojawapo ya hatari tulizozianisha hapo juu!

Zipo sababu kadhaa za kitafiti zinazowafanya akina baba wengi hasa Afrika kutoshiriki malezi ya watoto wao. Kwa mfano tafiti zilizofanywa mwaka huu na ‘mtandao wa kuhamasisha ushiriki wa akina baba kulea’, Men Care Campaign/State of the World’s Fathers, umebaini kwamba mojawapo ya pingamizi za ushiriki wa akina baba katika kulea ni wanawake. 

Tafiti hizi zinasema kuwa akina wanapaona nyumbani kama eneo la miliki yao na baba hapaswi kuwaingilia katika mamlaka walizonazo juu ya mambo hapo nyumbani, ikiwa ni pamoja na malezi. 

Tafiti hizi zimebaini pia kuwa akina mama hasa Afrika huwakatalia waume zao kujihusisha na shughuli za malezi kwa kuhofia kuonekana wachawi kwani jamii haiamini mwanaume anaweza kumsaidia mkewe kazi za aina hii bila ya kulishwa ‘limbwata’ au ‘juju’.Tamaduni na mazoea yaliyopo katika jamii kuwa baba hawezi kulea wala kujishughulisha na kazi za nyumbani pia huwa changamoto kwa akina baba katika malezi. 

Tafiti hizi zinawanukuu baadhi ya akina baba ambao husaidia kazi za malezi na zingine za nyumbani kwa kujificha na kamwe hawakubali kuwa wao hufanya kazi hizi pindi wanapokuwa katika mazungumzo na rafiki na ndugu zao.

Pamoja na pingamizi hizi, bahati nzuri sayansi ya biolojia inampa baba sababu nzuri za yeye kujihusisha na malezi ya watoto. Pamoja na Taarifa tulizokupa hapo juu, zipo tafiti kwa mfano zimebaini kuwa uwepo wa baba katika wiki ya kwanza ya maisha ya mtoto humsaidia baba kuongeza uzalishaji wa homoni zinazomsaidia kuwa mtu mwenye mapenzi na watu, na kuwa michezo ya baba na watoto wake pia inawasaidia watoto kupata ongezeko la homoni hii.

Makala haya yameandaliwa wataalamu wa makuzi toka asasi ya C-Sema.